MKAZI wa Tabata, Dar es Salaam, Wilson Bagila (30), anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mchumba wake, Elinora Masuka (30), siku chache kabla ya kufunga ndoa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Masindoki Masindoki, amethibitisha kuwapo kwa mauaji hayo, na kwamba mtuhumiwa anatafutwa.
Alisema Elinora ambaye alikuwa mfanyakazi katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam, aliuawa Agosti 19, mwaka huu, saa tano za usiku nyumbani kwa mchumba wake huyo, Tabata.
Alidai kwamba Elinora alikuwa mchumba wa Bagila, na kwamba walikuwa katika hatua za mwisho za kufunga ndoa.
“Kwa mujibu wa majirani, siku ya tukio Elinora alichelewa kurudi kutoka kazini, alirudi saa tano usiku, alipofika aligonga kwa muda mrefu bila kufunguliwa na mchumba wake.
“Baadaye alifunguliwa lakini, baada ya kuingia ndani kulisikika sauti za kuzozana ambazo ziliashiria ugomvi, lakini baadaye kukawa kimya.
“Baada ya muda ulisikika mlango ukifunguliwa na kufungwa,” alisema Masindoki.
Alisema huenda wakati huo ndiyo mtuhumiwa aliutumia kutoroka baada ya kufanya kitendo hicho.
“Baada ya siku mbili kupita, majirani walipata wasiwasi wakaamua kutoa taarifa polisi na baada ya kuvunjwa mlango walimkuta Elinora akiwa amekufa kitandani,” alisema.
Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa marehemu alikatwa shingoni na kitu chenye ncha kali. Sakafuni kulikutwa vipande vya chupa.
Kaimu Kamanda huyo alisema awali, Bagila alijitambulisha kwa majirani hao kuwa alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Leopard iliyopo katika Hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam.
Lakini baada ya polisi kufika katika ofisi hizo, viongozi walikana kumtambua. Wakafuatilia katika makao makuu ya kampuni hiyo jijini Arusha, ambako ilibainika kuwa aliwahi kuwa mfanyakazi wao. Ilidaiwa kwamba aliacha kazi mwaka 2003.
Bibi harusi huyo mtarajiwa alikuwa afundwe (Kitchen Party) Agosti 20, mwaka huu. Aliuawa siku moja kabla ya shughuli hiyo.
Marehemu alitarajiwa kuzikwa jana jijini Dar es Salaam