Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete atoa msimamo mkali
Kikwete atoa msimamo mkali
By Habari Tanzania | Published  08/24/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Irene Bwire, Arusha

RAIS Jakaya Kikwete ametoa pointi 10 kama dira za uongozi kwa wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya wanaohudhuria semina elekezi.

Semina hiyo inafanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, Arumeru mkoani Arusha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo jana, Rais Kikwete aliwataka wawe wabunifu, wafuate taratibu na sheria za nchi, wawe tayari kuacha “legacy” na zaidi ya yote wajue kila kitu katika maeneo wanayoongoza.

Aliwataka watumie madaraka yao vizuri, wawe mfano wa kuigwa kwa tabia na mwenendo, na wawe na uhusiano mzuri na watu wanaowaongoza.

Pia aliwataka wawe na moyo wa kujituma, wafufue moyo wa kujitolea miongoni mwa wananchi, wasimamie vizuri halmashauri, wasimamie kilimo, elimu, huduma za jamii na hifadhi ya mazingira.

Alisema wao kama viongozi, wana jukumu la kulea watu wanaowaongoza.

“Uongozi ni kazi, hata ukikutana na watu wabishi au wauliza maswali, ni lazima ukubali kuwa watu wa aina hiyo wapo… ni sehemu ya watu wako na aulizaye ataka kujua,” alisema.

Kuhusu kuzingatia taratibu za nchi na sheria, Rais Kikwete aliwataka wakuu wa mikoa wawatumie ipasavyo makatibu tawala wa mikoa na wilaya ili kupata ushauri wa kisheria katika masuala mbalimbali na hivyo kuepusha ukiukaji sheria.

“Ombi langu kwenu ni kuwataka watawala wawe ni wawezeshaji, na si wakwamishaji na wacheleweshaji,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na washiriki wa semina hiyo.

Alisema watendaji ambao ni wacheleweshaji, wakwamishaji, wasio na uamuzi au wazito wa kutoa uamuzi, hawana nafasi katika awamu ya nne, hivyo wapishe njia ili kazi ya kuleta maendeleo isikwame.

Ili kutokwamishwa na wasaidizi wao, aliwataka wakuu hao wawe na uhusiano mzuri na wenzao ofisini na hata wananchi wanaowaongoza.

“Muwe na uhusiano mzuri na wenzenu, mkiwa na uhusiano mbaya mtakwamishwa… ujuaji, ukaidi na ujeuri havisadii katika kujenga kazi za nchi hii,” alisisitiza.

Rais Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wa semina hiyo, aliwataka washiriki watumie madaraka yao vizuri, na si kuwadhulumu au kuwaonea watu.

Pia aliwataka wawe wepesi wa kusikiliza shida za watu kwani kwa kufanya hivyo watapunguza idadi ya malalamiko yanayofika ngazi za juu.

“Ukianza kusikiliza matatizo ya watu, matatizo yanayoenda ngazi za juu yatapungua… tuwe na moyo wa kujituma, tuwe wachapakazi na tuepuke umangimeza.

“Nawaombeni mkafufue moyo wa kujitolea miongoni mwa wananchi badala ya wao kuendelea kusubiri serikali ifanye kila kitu. Katika baadhi ya mikoa wenzetu walijua maana ya kujitolea na sasa wamefika mbali,” alisema.

Aliwataka wakasimamie vizuri halmashauri zao, na si kuwa watazamaji tu.

Alisema mfumo wa Serikali Kuu unahusiana na Serikali za Mitaa, lakini kila moja ina mipaka na dhima yake.

Alisema: “Kila mmoja akijua mipaka yake, hakuna jinsi mtaingiliana au kugombana.

“Nataka muwe na wajibu wa kuhakikisha halmashauri zinatimiza wajibu wake. Sisemi mkawaingilie kupanga taratibu zao au kuajiri watu, lakini nasema jukumu la ma-DC katika halamashauri ni ‘eyes on, hands off’,” alisema.

Alisema kama watendaji wakuu wa wilaya, wana jukumu la kukemea na kukosoa tabia mbaya za watendaji.

“Ukiona mganga mkuu anatumia gari la wagonjwa kutamba nalo mitaani, lazima ukemee ili lirudi katika kituo cha afya linakostahili kuwepo… au fedha za kujenga hospitali zinatumika kulipa waganga, huwezi kuangalia tu, kazi yako kubwa ni uratibu,” alisema.

Rais Kikwete aliwataka viongozi hao kwa ujumla wasimamie vizuri kilimo ili kuleta mabadiliko katika maisha ya mwananchi wa kawaida.

“Tumeazimia kuleta modenaizesheni ya kilimo na bila msuli, kilimo hakiendi. Tumeanza na ASDP (Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo), lakini bila ma-RC na ma-DC kujua vizuri utekelezaji wake, ASDP haitatekelezeka,” alisisitiza.

Kuhusu usimamizi wa elimu, Rais Kikwete aliwataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya waingize katika mipango yao, ujenzi wa nyumba za walimu, kwani bila kufanya hivyo, shule nyingi zinazojengwa hazitakuwa na walimu.

“Tulianzisha Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na mwisho wa mpango huo ni mwaka 2007, kwa hiyo mwaka 2008 itakuwa balaa kama hatuongezi madarasa zaidi ili kukabili mfumuko huo wa wanafunzi.

“Tuanze kupanga sasa shule zao au madarasa yao watakayotumia na njia nyepesi ya kuanzia ni kuangalia wanafunzi wa darasa la sita mwaka huu ni wangapi. Hakuna haja ya kushikana mashati kama ilivyokuwa mwanzoni mwa mwaka huu,” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu huduma za afya na maji, Rais Kikwete aliwataka wakuu hao kuwa makini zaidi katika kusimamia maeneo hayo. Pia aliwataka waweke mkazo katika kampeni dhidi ya UKIMWI kwani kiwango cha asilimia saba cha hivi sasa kiko juu.

Aliwataka wawe makini na suala la kuhifadhi mazingira kwa sababu linatishia usalama wa maisha ya baadaye.

“Tusipojiangalia, tutawaachia watoto wetu jangwa… bonde la Ihefu tumeondoa mifugo zaidi ya 300,000 na sasa naambiwa majani yameota na maji yameanza kurudi. Naamini katika miaka miwili ijayo, Ruaha itaanza kutiririka kama ilivyokuwa zamani. Ni uamuzi mgumu, lakini ilibidi uchukuliwe…,” alisema Rais Kikwete.

Semina hiyo ya siku tano inaendelea leo ambako mada tano kuhusu nafasi na majukumu ya wakuu wa mikoa, makatibu tawala, na wakuu wa wilaya katika utendaji wa serikali itawasilishwa na Dk. Chrisant Mzindakaya; Hifadhi na Uboreshaji wa Mazingira Tanzania (Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Abubakar Rajab); na uzingatiaji wa kanuni na sheria katika matumizi ya fedha za serikali- changamoto ya hesabu katika Serikali za Mitaa (Ludovick Utoh – Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali).

Nyingine ni ‘nidhamu na matumizi ya fedha za serikali’ itakayowasilishwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bibi Blandina Nyoni; na ‘taratibu za manunuzi’ ya Dk. Ramadhani Mlinga; Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Manunuzi (PPRA).

Mwandishi wa habari hizi, Irene Bwire, ni Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.