Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wawekezaji wauziwa kijiji Bukoba
Wawekezaji wauziwa kijiji Bukoba
By Habari Tanzania | Published  08/23/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Rutami Cylidion, Bukoba

WATU zaidi ya 4,000 wakazi wa Kijiji cha Bubale, Tarafa na Wilaya ya Misenye, mkoani Kagera, hawana mahali pa kwenda kutokana na kijiji chao kuuzwa kwa wawekezaji katika mazingira ya kutatanisha.

Wananchi hao ambao wapo katika kijiji hicho tangu mwaka 1880, wameamriwa kuhama kijiji hicho, kuvunjwa kwa shule na zahanati ya kijiji, kwa madai kuwa ardhi kilipo kijiji ni mali ya wawekezaji wa ufugaji, wanaodai kuuziwa ardhi hiyo na ranchi ya mifugo ya Misenye, iliyo karibu na kijiji hicho.

Kilio cha wananchi hao kufurushwa na wawekezaji hao ambao hawakutajwa kwa majina, kimefahamika juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiijini humo na kuhudhuriwa na Mbunge wa Nkenge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala.

Akitoa taarifa ya mgogoro huo kwa mbunge huyo kwa niaba ya wananchi hao, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Paulo Mwikila, alidai kuwa kijiji hicho kilianzishwa mwaka 1880 na Ishenkandwa Lutaga, aliyehamia eneo hilo likiwa halina watu akitokea Kijiji cha Gabulanga, Kata ya Minziro.

Mwikila alisema kuwa hadi kufikia mwaka 1945, kijiji hicho kilikwisha kuwa na wakazi wengi, na kwamba baada ya kuona kimekuwa na wakazi, serikali ilikipatia usajili namba ZK/BK/13.

Mtendaji huyo alifafanua kuwa mwaka 1967, viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba walifika katika kijiji hicho wakiwa na viongozi kadhaa wa kampuni ya ranchi ya mifugo Misenye na kukaa kikao na viongozi kadhaa wa kijiji hicho.

Alisema kuwa katika kikao hicho walikubaliana kuwapatia eneo lipatalo maili 14 na wakakubaliana kwamba mpaka utakaotenganisha kijiji hicho na ranchi hiyo utakuwa ni Mto Kiboronga.

Alifafanua kuwa kikao hicho cha mwaka 1967 kilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo Dk. S. S. Madali aliyekuwa meneja wa NARCO, Gervas Ishengoma aliyekuwa meneja wa NAFCO, P. Kayanda aliyekuwa katibu Tarafa wa Misenye na viongozi kadhaa wa kijiji hicho cha Bubale.

Alisema kuwa cha kushangaza, mapema mwaka huu wameshangaa kuona watu wanaojiita wawekezaji wakifika kijijini humo wakidai kuwa eneo lote la kijiji ni mali ya ranchi ya Misenye na kuwa wameuziwa, ili waanze shughuli za ufugaji na kilimo.

Aliongeza kuwa kufuatia hali hiyo, wakazi wa kijij hicho sasa hivi wamesitisha shughuli za maendeleo, ikiwamo kusitisha ujenzi wa shule na kilimo wakisubiri muda wa kuondolewa kwa nguvu kama inavyodaiwa na wawekezaji hao.

Mwikila aliongeza kuwa hivi sasa wawekezaji hao ambao baadhi yao ni wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba wamefika katika kijiji hicho na kupewa ardhi ya kijiji hicho, ambapo tayari kaya 588 za vitongoji sita zimeamriwa kuondoka kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Alitaja vitongoji ambavyo tayari vimepimwa na watu hao na wakazi kuamriwa kuondoka kuwa ni Kisibo, Kazizi, Kaesharo, Kyengoma, Rwenkuba na Kakiri.

Akizungumzia malalamiko hayo, Dk. Kamala alisema kuwa ni kinyume cha sheria wakazi hao kuondolewa katika eneo lao ambalo tayari limekwisha kupatiwa usajili na serikali, na kwamba mwenye mamlaka ya kuwaondoa ni Rais peke yake.

Alifafanua kwamba hakuna mtu atakayeondolewa na wawekezaji hao hata kama eneo hilo wameuziwa na uongozi wa ranchi ya Misenye, na kuwa amewasiliana na Waziri wa Mifugo na Waziri wa Ardhi, na wote wamemhakikishia kuwa wananchi hao hawatahamishwa.

Dk. Kamala alisema kuwa sheria ya uwekezaji inataka wananchi kunufaika na uwekezaji na si kunyanyaswa na wawekezaji, na kudai kuwa kitendo kilichofanywa na wawekezaji hao na uongozi wa ranchi hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ameagiza kuwa wananchi waendelee na shughuli zao za uzalishaji na kwamba atakayewataka kuhama kijiji hicho wamweleze kwamba awasiliane na ofisi ya naibu waziri huyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.