Mkazi mmoja wa Kijiji cha Hedaru wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro, George Mangage, (20) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi Hedaru wilayani Same.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Same, Bw. Fidelis Lamtei.
Alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na upande wa mashtaka ulioongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Wilaya hiyo, Bw. Mbwiga Mwampanda.
Awali, ilidaiwa kuwa katika siku na tarehe tofauti ya mwezi Septemba mwaka jana, mshitakiwa alimbaka mwanafunzi huyo na kusababisha ujauzito huo.
Mwanafunzi huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji mtoto wa kiume Mei 5, mwaka huu katika hospitali ya wilaya hiyo.
Ingawa mshtakiwa alikana shtaka katika hatua za awali, lakini Mwendesha Mashtaka, Bw. Mwampanda aliomba mahakama kutoa adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia mbaya ya kuwabaka wasichana.
Katika hukumu yake, hakimu Lamtei alitoa adhabu ya miaka 30 kwa kubaka.
Pia alihukumiwa miezi sita kwa kosa la kumkatisha masomo mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 15, ambaye jina lake limehifadhiwa. Adhabu zote zinakwenda pamoja.
Akitoa hukumu hiyo, hakimu Lamtei alisema mshtakiwa anastahili adhabu kali, kwa kuwa amekatisha maisha bora ya msichana huyo.
Aliwaonya vijana kujiepusha na tabia ya kufanya mapenzi na wasichana wenye umri wa chini ya miaka 18.
Mara baada ya hukumu hiyo, mlezi wa mwanafunzi huyo ambaye ni mtoto wa dada wa mke wake anayeishi Dar es Salaam, Bw. Hassani Doo, aliipongeza mahakama ya wilaya hiyo kwa kuitendea haki familia yake.
Bw. Doo alisema mara nyingi kesi za aina hiyo, zimekuwa zikiishia kwa washtakiwa kuachiwa huru, kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa kutosha na kueleza matumaini yake kwa serikali ya Awamu ya Nne imeonyesha dhamira ya kuondoa kero za wananchi.
SOURCE: Nipashe