JESHI la polisi mkoani Kigoma limewakamata askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Watanzania (JWTZ) na mmoja anatafutwa, kwa tuhuma za mauaji ya mwananchi wa tarafa ya Kakonko, wilayani Kibondo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake, kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Patrick Byatao, aliwataja askari hao kuwa ni MT 76682 Hamad Hamisi, MT 55230 koplo Chacha Kisiri, MT 70099, koplo Joseph Giri, MT 76676 Abeid Makame na MT 74760 Kulwa Adam ambaye hajakamatwa.
Askari hao, ambao tayari wameshafikiswa katika mahakama ya wilaya ya Kibondo, wanatuhumiwa kumuua Nteze Bihombe kwa kumpiga wakimtuhumu kwa wizi wa simu ya mkononi aina ya NOKIA, yenye thamani ya sh. 120, 000, mali ya mmoja wa askari hao.
Alisema katika tukio hilo lililotokea Aprili 22, mwaka huu saa 11:30 jioni, watuhumiwa pamoja na marehemu na rafiki yake, Deogratius Rweyemamu, walikuwa wakinywa pamoja pombe katika klabu moja kijijini hapo, na ndipo simu hiyo ilipoibiwa na hivyo askari hao kuwatuhumu marehemu Nteze na mwenzake Deogratius na kuanza kuwashushia kipigo.
Pamoja na kipigo, Deogratius alifanikiwa kukimbia na kujisalimisha kituo cha polisi Kakonko, na mwenzake ambaye sasa ni marehemu, aliendelea kupigwa hadi alipofikishwa polisi.
Kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo marehemu, pamoja na kukiri kituo cha polisi kuwa aliiba simu hiyo, alifariki kesho yake wakati akipelekwa hospitali kwa matibabu.
Kamanda Byatao alisema jeshi la polisi linafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi, hivyo hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria.