Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  RAS Kagera amtetea Kayungi
RAS Kagera amtetea Kayungi
By Habari Tanzania | Published  08/23/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) imeamua kumtetea Afisa wa Maliasili na Utalii, Japhet Kayungi, anayedaiwa kunyanyasa wananchi wanaovua au kununua samaki wilayani Bukoba.

Barua ya utetezi inayothibitisha wanayokanusha, iliyotumwa Tanzania Daima kwa njia ya Fax jana, ilisema: “Baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara ya samaki wanamchukia Ndugu Kayungi kwa sababu yeye anafuatilia sana wale wanaofanya shughuli za uvuvi kinyume cha sheria, kanuni na taratibu.

“Hivyo basi, lengo la madai hayo ni kumchafulia jina na kumkatisha tamaa katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda rasilimali za nchi yetu zilizoko ndani ya Ziwa Victoria,” ilisema sehemu ya taarifa ya RAS iliyosainiwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, George Katomero.

Taarifa ya Katomero, imetoka siku chache wakati Afisa wa Ikulu, akitoa maelezo kuwa ufanyike uchunguzi juu ya watendaji wenye mwelekeo wa aina ya Kayungi, wanaovuka mipaka katika utendaji wao na wachukuliwe hatua stahili katika suala hili la uvuvi wa samaki.

Kilichoripotiwa na Tanzania Daima Agosti 3, 2006, ni mahojiano kati ya wakazi wa Wilaya ya Bukoba, waliosononeshwa na utaratibu wa kuwasulubu, waliodai anautumia Kayungi na kwamba Bukoba sasa samaki wanauzwa katika mifuko myeusi, kama bangi kuepuka Kayungi asiwaone.

Maelezo ya wananchi yalionesha kuwa sasa hivi wanatamani enzi za mkoloni ambako samaki walivuliwa na kuliwa kwa uhuru, badala ya sasa ambapo samaki imegeuka mali ya Wazungu na Watanzania wanabakiziwa mapanki kwa uwakala unaofanywa na wazawa wachache waliogeuka miungu watu.

Walisema Kayungi ana mahakama yake na anafunga watu hadi miezi mitatu kwa kukutwa na samaki katika eneo la Kemondo, ila taarifa ya RAS ilisema: “Maafisa uvuvi wanapofanya doria hufanya kwa kushirikiana na vyombo vya dola, polisi na Idara ya Mahakama. Wahalifu wa sheria za uvuvi ambao hukamatwa wakati wa doria hizo hufikishwa mahakamani (Mobile Court) mara wanapokamatwa na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria na kupelekwa gereza la Bukoba Mjini na si vinginevyo. Hakuna jengo lolote linalotumika kama gereza huko Kemondo.”

Katomero alisema katika taarifa hiyo kuwa wamefanya uchunguzi huko Kemondo na kubaini kuwa wavuvi na wafanyabiashara ya samaki hawasumbuliwi, isipokuwa: “Usumbufu unatokea pale watu wanapotaka kufanya biashara hiyo kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za serikali kama kuuza samaki wadogo ambao huvuliwa kwa kutumia zana za uvuvi zilizozuiliwa kisheria, nyavu zenye macho chini ya inchi 5 na makokoro. Hawa hukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.”

Ingawa Tanzania Daima iliandika jina moja tu la Kayungi, RAS amemtaja mtumishi huyo kwa majina yote mawili na cheo chake kuwa ni Nahodha Mkuu (Principal Skipper), ambaye ni mwajiriwa wa Wizara ya Maliasili na Utalii na kitu walichopinga wananchi ni wazawa kufanya kazi sawa na wanyampara wa enzi za mkoloni.

Taarifa hiyo ilimaliza kwa kutoa vitisho dhidi ya Tanzania Daima kwa kuchapisha habari hizo: “Kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera imethibitisha madai hayo si ya kweli, inakutaka uchapishe taarifa hii ya kukanusha madai yaliyotolewa kwenye gazeti lako la tarehe 3 Agosti, 2006. Jambo hili lisipotekelezwa, ofisi hii itachukua hatua zaidi za kisheria dhidi ya gazeti la Tanzania Daima.”


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.