KAULI ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ya kutaka mikataba ya madini ipitiwe na kulipatia taifa faida zaidi, imetekelezwa.
Serikali imetekeleza kauli hiyo kwa kupitia na kurekebisha mikataba ya madini, ambayo chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu ilikuwa ikitajwa kuwa haiwezekani kufumuliwa.
Mabadiliko makubwa yameanzia katika Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Tulawaka, ambayo baada ya majadiliano na Rais Kikwete mwenyewe juzi, imekubali kutoa sh milioni 9,100 au dola milioni 7, kama kodi serikalini kwa mwaka.
Mbali na kiasi hicho, kila halmashauri ya wilaya ilipo migodi hiyo, itapatiwa sh milioni 260 sawa na dola 200,000 kwa mwaka.
“Nia ya serikali, kama ambavyo imekuwa ikielezwa mara kwa mara na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ni kuhakikisha kuwa nchi yetu (a) inanufaika ipasavyo na utajiri mkubwa wa madini, (b) inajenga mazingira endelevu ya uwekezaji, (c) inapata kodi ya 30% (corporate tax), (d) inapata maendeleo katika maeneo yanayochimbwa madini, na (e) inafaidika kwa kupata ajira na huduma mbalimbali zinazotokana na kuwepo kwa uchimbaji wa madini,” alisema Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha.
Dk. Msabaha aliyeambatana na naibu wake, Laurence Marsha, alisema juzi viongozi wa Barrick walikutana na Rais Kikwete na kukubaliana naye mambo saba, ambayo ni:-
Kuondoa katika mikataba kipengele cha nyongeza ya kivutio cha asilimia 15 kwenye salio la gharama za uwekezaji (15% additional capital allowance on unredeemed capital expenditure) na kulipa kodi ya US $200,000 (sawa na sh milioni 260) kila mwaka katika halmashauri za wilaya zenye migodi ya Barrick.
Nyingine ni kulipa US $ milioni 7 (sawa na sh bilioni 9.1) kila mwaka kwa Serikali Kuu hadi kampuni itakapoanza kulipa kodi (corporate tax) na kununua bidhaa za ndani ya nchi kwa kadri zitakavyopatikana; kutumia kampuni za ndani ya nchi na wazalendo katika kutoa huduma mbalimbali katika migodi.
Pia walikubaliana kushirikiana na serikali katika kutatua matatizo ya muda mrefu ya wachimbaji wadogo wadogo na kutafuta njia za kutoa elimu endelevu ya ufundi kwa Watanzania ili waweze kushiriki ipasavyo katika soko la ajira na katika ujenzi wa taifa.
Kuondolewa kwa kivutio cha nyongeza ya asilimia 15 kwenye salio la gharama za uwekezaji, kutaifanya serikali iweze kupata kodi ya asilimia 30 kutoka kwa wachimba madini hao ambayo haijapata kutolewa tangu waanze kuchimba madini hapa nchini mwaka 1997.
Kivutio hiki cha asilimia 15 kimekuwa kikitumiwa na kampuni za kuchimba madini kuonyesha kuwa zinapata hasara muda wote, hali inayozifanya zisilipe kodi kabisa, lakini sasa imefutwa.
Dk. Msabaha alisema pamoja na makubaliano hayo, bado kampuni za kuchimba madini zina jukumu la kuendeleza jamii zinapofanyia kazi ya kuchimba madini (social responsibility), hivyo zitapaswa kuwaletea maendeleo wananchi.
Makubaliano hayo yataiwezesha serikali na Kampuni ya Barrick Gold Mine kufanya marekebisho katika Mikataba ya Uendelezaji wa Madini (Mining Development Agreements - MDA). Huu ni mkataba unaokubalika kimataifa na Afisa mwandamizi wa serikali aliiambia Tanzania Daima baada ya mkutano na Dk. Msabaha, kuwa Rais Kikwete alijua kuwa palihitajika mabadiliko, lakini kuepusha vurugu zisizo za lazima, ilibidi mabadiliko hayo yasipandikizwe bali yawe shirikishi.
Alisema kama serikali isingezishirikisha kampuni za madini na kujadiliana nazo juu ya umuhimu wa kulipa kodi, ingeweza kuzua mtafaruku na migogoro mikubwa ambayo nchi ingeshindwa kuaminika kimataifa.
“Huwezi kubadili peke yako. Nchi haitapata wawekezaji kwa utaratibu huo kwani utajenga migogoro, utapata kesi na nchi itaongezewa riba kubwa katika mikopo ya kimataifa, hii inaitwa sovereign risk. Inaongezeka sana ukibadili mikataba bila utaratibu.
“Rais anastahili kupongezwa kwani mabadiliko haya yaliyofanyika yataliingizia taifa wastani wa sh bilioni 500. Amekuwa rais makini, mwenye kufikiri na kuweka mikakati na kwa kutumia ushawishi wa hali ya juu katika diplomasia ya uchumi, amewezesha mabadiliko kufanyika nao wakashawishika,” alisema afisa huyo.
Alisema katika nchi nyingine, mikataba inapobadilishwa kinakuwa chanzo cha kuvuruga uchumi wa nchi na anafarijika kuwa Tanzania imeweza kubadili mikataba hii bila kuathiri heshima ya nchi, kuitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa (Sovereign risk), na wawekezaji wataendelea kuamini kuwa ni nchi inayothamini mazungumzo (negotiation) katika kufikia makubaliano badala ya mabavu.
Afisa huyo alisema Rais Kikwete ameonyesha tofauti katika kipindi cha miezi saba tu, ameweza kumpiku Rais aliyemtangulia, Benjamin Mkapa na sasa anafanya waliyodhani hayawezekani. Pia aligusia mpango wa kupeleka vijijini sh bilioni moja kwa ajili ya kukopesha wananchi kuwa ni sehemu ya ubunifu wenye manufaa kwa Watanzania.
Kwa wabunge wa Kanda ya Ziwa, mabadiliko haya yatakuwa ni sherehe kwao kwani kimekuwa kilio chao cha muda mrefu, wakitaka serikali itenge fungu lenye kueleweka litumike kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yanapochimbwa madini.
Wabunge hao wamekuwa wakidai malipo hayo kama mrahaba, kwa maelezo kuwa wawekezaji hawawezi kufika mahala wakatoa fedha bila kubanwa na sheria.
Kwa mujibu wa Dk. Msabaha, makubaliano hayo yaliyofikiwa juzi kati ya Kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania, yatahusisha kampuni nyingine baada ya majadiliano na kampuni moja moja na baadaye yataingizwa katika sheria