Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mapanki yameonyesha ukaidi wa watawala
Mapanki yameonyesha ukaidi wa watawala
By Habari Tanzania | Published  08/22/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

AMA kweli binadamu ni kiumbe tata! Nadhani ni utata huu ambao Mwenyezi Mungu alimuumba nao uliosababisha Mungu mwenyewe amwekee amri ya kutomuabudu Mungu mwingine wakati akijua kuwa Mungu ni yeye peke yake.

Sakata la vichwa na mifupa ya samaki, maarufu kama mapanki, lililoibuliwa na filamu ya Darwin’s Nightmare, iliyotengenezwa na Mfaransa, Hubert Sauper, linauweka wazi utata huu wa mwanadamu aliojaliwa na Mungu, kiasi cha Mungu kuutilia shaka na kuamua kuuwekea amri ya kwamba usimwabudu Mungu mwingine!

Msomaji akifuatana na mimi vizuri atauona utata huu katika maelezo yangu hapa chini.

Ziwa Nyanza, ambalo madalali wa Kizungu waliamua kulibatiza jina la Victoria, kwa madai kuwa wao ndio waliolivumbua, ni ziwa lililojaliwa samaki wengi wa aina mbalimbali ambao utamu wao hauishii kuelezwa kwa maneno tu, bali pia kwa vitendo vinavyojitokeza hivi sasa katika ukanda wote wa ziwa lile.

Na katika aina zote za samaki wanaopatikana katika ziwa lile, ni samaki wa aina mbili tu ambao wenyeji wa ukanda wa ziwa tunaamini kuwa si samaki wa asili wa ziwa lile.

Tunasema hawa ni samaki wahamiaji, na inawezekana walihamia wenyewe kutoka katika vyanzo vya maji yanayokuja katika Ziwa Nyanza au walipandikizwa kutoka kwingineko. Hii inatokana na kutokuwapo historia ya uhakika kuhusu samaki hawa. Na hawa samaki wahamiaji ni dagaa na sangara.

Samaki aina ya dagaa, pamoja na ugeni wao, ni samaki ambao hawajasababisha mabadiliko yoyote katika ziwa lile hadi leo, pengine kutokana na umbo lao dogo. Na badala yake wamewanufaisha sana wananchi wa kipato cha chini kwa maana ni kitoweo cha bei poa kuliko vitoweo vya aina zote vinavyopatikana maeneo yale, na papo hapo kutoa ajira, hasa kwa vijana wanaokwenda kuwanunua kwa wavuvi na kwenda kuwachuuza vijijini.

Ujio wa samaki aina ya sangara katika Ziwa Nyanza kidogo ulivuta hisia za watu. Kwanza, alionekana ni samaki mwenye umbo kubwa kuliko samaki wa aina zote wa asili ziwani mle, na pili, alikuwa na mafuta yasiyo ya kawaida yaliyokuwa yanasababisha shombo kiasi kwamba akipikwa katika nyumba moja, mtaa mzima unajaa shombo la sangara.

Kadiri muda ulivyokwenda, sangara wakaanza kuwa kero, hasa baada ya kukaribia kuwatokomeza samaki wa aina nyingine kwa kuwala huku wao wakizaliana kwa kasi ya ajabu na kuzidi kuongezeka kila kukicha.

Wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyanza walikuwa wamefikia mahali hawataki tena kitoweo cha samaki kwa sababu ya kuwa na aina moja tu ya samaki (sangara), ambayo ndiyo iliyokuwa inapatika kirahisi na kwa wingi, ambayo lakini kwa sababu ya kuwa na mafuta mengi kupindukia, inakinaisha haraka.

Kwa kweli sangara walikuwa wameanza kuwa tatizo, ambapo baadhi ya wakazi wa maeneo ya Ziwa Nyanza walikuwa wameishaanza kulitumia kusimangana, mfano: “Ni mgeni gani huyo ambaye kaja na zawadi ya sangara?” Watu walikuwa hawajui wafanye nini ili kuwadhibiti sangara ambao walikuwa wanaelekea kuwa tishio badala ya neema!

Kule Kenya, kwa mfano, kutokana na kukosa ubunifu wa mbinu za kugeuza kero kuwa faraja, nasikia kulikuwapo mpango wa kupandikiza mamba ziwani ili waweze kuwala sangara kama njia ya kudhibiti ongezeko lao sambamba na kuzuia kutoweka aina nyingine ya samaki ziwani humo.

Leo hii imepatikana njia nyingine ya kukabiliana na sangara, tena iliyo bora na yenye masilahi kuliko ile ya kutumia mamba, njia ya kutumia viwanda kuwasindika, watu wanaanza kulia eti wanalazimishwa kula mapanki! Utata wa mwanadamu huu!

Ikumbukwe neno mapanki halikuletwa na Darwin’s Nightmare, kama baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanavyodhania, hili ni neno lililotokana na watu kuuziwa mabaki ya sangara ambayo yanakuwa yameshatolewa minofu kule viwandani. Mabaki haya yamekuwa yakifananishwa na kichwa cha mwanadamu kilichonyolewa kwa mtindo wa panki, na hiyo ndiyo asili ya jina la mapanki.

Kusema ukweli, si kwamba watu wanalazimishwa kuyala haya mapanki, tatizo linatokana na mazoea. Watu walizoea, mfano, kwenda pale Mwaloni, jijini Mwanza na kukuta samaki wamerundikana huku wachuuzi wakiwakaribisha wateja kwa kuwabembeleza, wateja wakijipangia bei kwa kuchagua ni aina gani ya samaki wanunue na ipi waache.

Baada ya ujio wa viwanda vya kusindika samaki, mahitaji ya samaki yameongezeka. Na kwa vile samaki wanaohitajiwa viwandani ni sangara, yale mazoea ya watu kuwakuta sangara wamerundikana Mwaloni yametoweka. Moja kwa moja hii itakuwa imesababisha bei ya aina nyingine za samaki, hasa sato, kwenda juu.

Mikogo ya wateja kwa wauza samaki, makaribisho ya kubembelezwa na kugombaniwa, vyote vimetoweka na upepo! Kuna mabadiliko. Bei ya sato ikiwa juu njia mbadala ya kitoweo ni mapanki, kwa sababu sangara wanapelekwa viwandani.

Mapanki yapo na yanaliwa, yasingekuwapo Rais Jakaya Kikwete angeyajuaje? Ila tatizo hili la malalamiko juu ya mapanki linakuzwa na utaratibu wa serikali yetu unaoonekana kuwapendelea zaidi wenye viwanda, au tuseme kujali zaidi kinachoitwa masilahi, bila kujali ustawi na hatima ya wakazi wa eneo linalolizunguka ziwa.

Iwapo wananchi wangeachiwa waendelee kuvua bila kuingiliwa kama walivyozoea siku zote, sidhani kama kuna mtu ambaye angekuwa anayalalamikia mapanki. Kwa nini mtu alazimike kula mapanki wakati anaweza kujivulia samaki anaowataka?

Kitendo cha kuwazuia wavuvi wadogo wadogo kinachotafsiriwa kama jitihada za serikali kuvilinda viwanda vya samaki na kuwafanya wananchi walione ziwa kama vile si mali yao kwa vile ama limebinafsishwa au kuuzwa, ndicho kiini cha sakata la mapanki.

Tatizo jingine ni la kuwa na wawakilishi wasioyajua matatizo yanayowakabili wale wanaowawakilisha, kwa vile hao wawakilishi si sehemu ya jamii wanazoziwakilisha. Hebu fikiria; mtu aliyeishi ughaibuni kwa zaidi ya miaka 25 akarudi nyumbani kwa ajili ya kugombea ubunge, atalijuaje suala la mapanki?

Au mtu anayeishi jijini Dar es Salaam kwa kipato cha sh laki tatu au nne kwa siku, baadaye akaenda kugombea ubunge wa Bukoba Vijijini au Nkenge, anawezaje kudai kuwa yeye ni sehemu ya jamii ya wakazi wa Lubafu, Bukoba Vijijini, ambako wastani wa kipato cha mwananchi ni kama sh 50 kwa siku? Na kuna uwezekano gani wa mwakilishi huyu kuyajua mapanki?

Na ikitokea pengine mwakilishi (mbunge) anamiliki au ana hisa katika kiwanda cha kusindika minofu ya samaki, ni upande upi ataupa kipaumbele katika utetezi wake?

Wananchi anaowawakilisha au kiwanda cha samaki ambacho anajua kwamba anakimiliki au ana hisa au mwenye nacho, hataweza kuwajali wananchi.

Kinachoangaliwa ni masilahi kwanza, tuendelee.

Baada ya Rais Kikwete kuwahutubia wazee wa Jiji la Mwanza, katika hotuba iliyolenga zaidi kuishambulia filamu ya Darwin’s Nightmare, viongozi wa chama tawala mkoani Mwanza walihamasisha maandamano ya kuiunga mkono hotuba hiyo, huku wakimlaani vikali mtayarishaji wa filamu hiyo. Wakati huo huo, wabunge wa maeneo ya Kanda ya Ziwa waliokuwa kwenye mkutano wa Bunge Dodoma, nao wakawa wanayaunga mkono maandamano yale!

Kila nikifikiri, sidhani kama maandamano yale yalisukumwa na moyo wa uzalendo pamoja na mapenzi ya dhati kwa Rais, kwa kukiamini kile alichokizungumzia. Nashawishika kuamini kwamba yale yalikuwa maandamano ya funika kombe mwanaharamu apite.

Iwe isiwe, sehemu kubwa ya waandamanaji wale ndio wateja wazuri wa mapanki! Sasa unaweza kujiuliza, waliandamana kulaani nini na kupinga nini? Sina shaka na Rais Kikwete kutoyafahamu mapanki. Kutokana na nafasi aliyokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 20 na hii aliyopo hivi sasa, na ikizingatiwa kuwa yeye ni mtu wa pwani, sisiti kuamini kuwa mapanki ameyajua kwa kuelezwa tu.

Angekuwa anatokea Kanda ya Ziwa, ikitiliwa maanani huluka yake ya kujichanganya na watu, ningesema alishayaona. Lakini hali inavyojionyesha, Rais Kikwete ameelezwa kuhusu mapanki na wale waliotaka ayaelewe jinsi alivyoyaelewa na ayasemee jinsi alivyoyasemea na baadaye wapange maandamano ya kuunga mkono kauli zake!

Sanaa, kama ilivyo fasihi, ni kioo cha jamii, kupitia katika sanaa ya sehemu fulani ni rahisi kupata taswira ya mwenendo wa mambo wa jamii husika. Msanii wa muziki wa kizazi kipya wa hapa nchini, Joseph Haule maarufu kama Profesa J, ameimba wimbo unaoitwa ‘Ndiyo’ Mzee, wimbo unaobainisha ghiliba za wanasiasa na utata wa mwanadamu.

Baada ya kibao hicho, mwanamuziki huyo ametoa kibao kingine kinachoitwa ‘Kikao cha Dharura’. Kama kweli wanasiasa wetu ni wanafasihi wanapata ujumbe gani kupitia maudhui ya nyimbo hizo mbili? Je, nani angependa Rais Kikwete aitwe kwenye kikao cha dharura chenye lengo la kumsuta?

Sasa hivi eneo la Ziwa Nyanza (Victoria), halina tofauti na sehemu nyingine za migodi yenye kutoa madini adimu au visima vya mafuta mahali popote duniani, ndiyo maana likawa na mvuto kiasi cha Sauper kuamua kuja kulifanyia dokumentari.

Yawezekana akawa amefanya vile kwa lengo baya. Lakini ikitiliwa maanani uzoefu wa yanayotokea katika maeneo ya aina ile kwingineko katika nchi za dunia ya tatu, hatupaswi kung’ang’ania upande mmoja tu wa lengo baya.

Pengine badala ya kumlaumu mtayarishaji wa filamu hiyo, ingebidi tumshukuru, kwa sababu katuonyesha upungufu uliomo katika usindikaji wa minofu ya samaki ili tuufanyie kazi.

Nani angependa kuona eneo linalochangia masilahi ya taifa kwa kiwango kikubwa (kitakwimu?) kama inavyoelezwa, ligeuke kuwa uwanja wa maasi, kutokana na masilahi yanayopatikana kutowanufaisha wakazi wa eneo husika?

Kwa nini yanayotokea Niger Delta kule Nigeria au yaliyotokea kule Ogoni, kule kule Nigeria na kwingineko kwenye sehemu kama hizo, yasiwe fundisho kwetu na hivyo tukamuona huyu Mfaransa kama malaika aliyetumwa na Mungu kuja kutuamsha usingizini na kutuonyesha moto unaowashwa karibu na mapipa ya petroli ndani ya nyumba yetu?

Kwa vile tumewahi kuamka kabla ya moto haujayashika mapipa ya petroli, shukrani zetu ni kumlaumu aliyetuamsha kwa kutuharibia usingizi wetu! Utata wa mwanadamu!

Suala la ukahaba linalojitokeza katika filamu hiyo hivi kweli linahitaji kutushtua? Au tulirudishe katika lugha tuliyoizoea – uchangudoa. Hili si neno lililoletwa na Sauper, ni neno lililozoeleka katika majiji na miji yote ya nchi hii. Mzee Makamba, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anaweza kulitolea ushahidi hili, kwa sababu uchangudoa ni vita iliyomshinda akiwa mkuu wa mkoa.

Jambo jingine linalojitokeza kwenye Darwin’s Nightmare ni silaha. Mimi nadhani suala hili halihitaji jazba katika kulikabili. Kabla ya kumlaani Sauper, ningeishauri serikali imuite mtayarishaji huyo aje kulitolea uthibitisho, akishindwa kufanya hivyo tumlaani kwa nguvu zetu zote.

Maana, sasa itakuwa si minofu ya samaki tena, bali kuipaka Tanzania matope kwa kuionyesha kuwa ndiyo uchochoro wa kusababisha mvurugano na umwagaji damu katika nchi za Maziwa Makuu wakati yenyewe ikijigamba kuwa kisiwa cha amani. Lakini ikibainika kuwa mchezo huo upo, pengine bila ufahamu wa serikali, basi udhibitiwe.

wapo wanaojaribu kutushawishi tuamini kuwa sakata hili limesababishwa na mji wa Kisumu, kutokana na kile kinachoonekana kama ushindani wa kibiashara kati ya miji ya Kisumu na Mwanza.

Mimi nadhani ingetubidi tuwe waangalifu katika kulishughulikia suala hili ili kuepuka kujiingiza katika uhusiano mbaya na jirani zetu bila ulazima wa msingi kwa mambo yanayotuhusu sisi wenyewe. Tusije tukawa kama watu wa kabila moja mkoani Kagera, ambao hawaamini kwamba tatizo linaweza likajitokeza lenyewe, ila ni lazima liwe limeletwa au kutumwa na jirani! Na huu ni utata wa binadamu.

Kama nilivyosema awali, fasihi ni kioo cha jamii. Tamthilia ni michezo ya kuigiza inayobeba maana nzito juu ya mwenendo wa jamii. Mathalani, katika tamthilia ya Julius Caesar iliyoandikwa na Shake Speare, mnajimu mmoja alimtahadharisha Mfalme Julius Caesar kwamba ‘beware of the ides of march’, lakini kwa jeuri ya ufalme, Caesar akadharau na kuwaambia waendelee na safari yao, eti yule mnajimu alikuwa na ndoto za mchana.

Matokeo ya ukaidi na jeuri ya ufalme ni Caesar kujikuta akimlalamikia na kushangaa rafiki yake kipenzi, Brutus, alipokuwa anaongoza mashambulizi ya kumuangamiza Caesar, pale mambo yalipokuwa yamegeuka.

Kumbuka Brutus alikuwa kipenzi cha mfalme na aina ya wale ambao wangeitisha maandamano ya kuunga mkono kauli ya Caesar ya ‘pass he is a day dreamer’. Nisingependa Rais Kikwete naye aje kusema “hata wewe Brutus?”

Bunge limepitisha azimio la kuilaani Darwin’s Nightmare na mtayarishaji wake. Ungelikuwa utata pia kama lisingefanya hivyo. Kinachoangaliwa kwanza ni masilahi kabla ya kujua ni masilahi kwa nani. Sauper alaaniwe kwa kutaka kuvuruga soko la minofu ya samaki wetu. Samaki wauzwe, wenye kunufaika wanufaike, wenye kukosa wakose. Yakilipuka ya Ogoni, Niger Delta, wenye viwanda vya samaki watajitimkia na kwenda zao, huku nyuma wakituachia ziwa letu tupu na mapanki yetu. Wakati huo hakuna cha kiwanda wala samaki kusindikwa, kitakachokuwa kikiendelea pale!

Anayetahadharisha hayo yasitokee ndiye anayeonekana mbaya wa masilahi yetu! Hakika mwanadamu ni kiumbe tata.

prudencekarugendo@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.