FAMILIA zaidi ya 24 zimeachwa bila makazi wilayani Iringa Vijijini, baada ya makazi yao kuchomwa moto na watu wanaodhaniwa kuwa ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtera.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Alhamisi wiki iliyopita katika Kitongoji cha Ladwa, Mbweleli Mtera, mkoani hapa.
Eneo hilo lilikuwa linakaliwa na wavuvi katika Bwawa la Mtera.
Mbali ya kukosa makazi, waathirika wa janga hilo wamekimbia kabisa eneo hilo, na kwa siku mbili wamekuwa wakiishi vichakani wakihofia usalama wao.
Hali hiyo imetokana na kuwapo tishio jingine kutoka kwa wanafunzi hao.
Kwa siku hizo, wamekuwa wakiishi bila chakula wala mahema, hali iliyoulazimu uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa kupeleka msaada wa kilo 200 za unga; na kilo 100 za maharage.
Habari zaidi kutoka kwa wakazi wa eneo hilo ambao hawakuwa tayari kutajwa majina gazetini, zilisema kwamba chanzo cha uhasama baina ya wanafunzi na wakazi hao ni wizi wa waya wa mota ya umeme unaotumiwa na shule kuvuta maji kutoka Mtera.
Waya huo wenye thamani ya sh milioni 1.5 unadaiwa kuibwa usiku wa Agosti 16; na siku iliyofuata wanafunzi walivamia kijiji wakitaka waelezwe aliyehusika na wizi huo.
Bila mafanikio, walirejea shuleni kwao wanakodaiwa kupanga mikakati ya uvamizi uliofanywa siku iliyofuata, kwa wanafunzi kuliteka eneo husika, na kuwaamuru wakazi kutoka ndani ya nyumba zao.
Inadaiwa kwamba, ingawa walitekeleza amri hiyo baada ya mabishano makali, wananchi walianza kutoka kwa kasi baada ya kushuhudia nyumba moja baada ya nyingine zikichomwa moto na kuteketea.
Siku iliyofuata, ghadhabu za wanafunzi zilikuwa maradufu, kwani kulitokea wizi mwingine wa pampu yenye thamani ya sh milioni 3.5, hali iliyowafanya kutoa vitisho zaidi.
Kwa hofu ya kutokea maafa zaidi, wananchi walikihama kijiji na kwenda kuishi vichakani bila kujali wanyama wakali.
Habari hizo zilifika wilayani na kuwalazimu maofisa wa serikali Wilaya ya Iringa Vijijini, akiwamo Mkurugenzi wa Wilaya, Tina Sekambo, kwenda eneo la tukio.
Mkurugenzi huyo aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, licha ya kuwapa pole na kusikitishwa na hali aliyoiona, aliwataka wahame kwa madai kwamba, wameishi katika eneo hilo kwa makosa kutokana na kuwa na karibu mno na ukingo wa Mto Mtera, moja ya vyanzo vya uzalishaji umeme nchini.
Kutokana na tukio hilo, walimu wawili, akiwamo Makamu Mkuu wa Shule, Oscar Ngusulu na fundi umeme wa shule hiyo, kuanzia juzi wanashikiliwa polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Iringa.
Mkuu wa Shule, Newton Maganga alikuwa safarini kikazi wakati wa tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa vile yuko nje ya mkoa kikazi.