KATIBU wa Chama cha Waishio na Virusi vya UKIMWI na Matumaini (CHAWAVUMA), Mkoa wa Kilimanjaro, Dickson Malle, amesema dawa za kuongeza muda wa kuishi kwa waathirika wa UKIMWI (ARV’s), hazina madhara kama mtumiaji atafuata masharti.
Akizungumza na Tanzania Daima Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Malle alisema kumekuwapo madai na taarifa kuwa dawa hizo zinawadhuru watumiaji.
Alisema dawa hizo ni nzuri, na zinawasaidia watumiaji, lakini huwa na madhara pindi mtumiaji anapokiuka masharti.
“Tumesikia malalamiko hayo, tulifanya utafiti wetu kwa watu tunaowafahamu ambao wanazitumia, tukagundua walioathirika ni wale wasiofuata masharti.
“Dawa hizi ni kali, zinahitaji mtumiaji apate lishe nzuri na afuate masharti-kila siku akiamka, anatakiwa anywe, na asiache hata siku moja mpaka siku anakufa.
“Masharti mengine ya hizi dawa kwa mwathirika, anapaswa kuacha kufanya ngono, kunywa pombe, kuvuta sigara, kufanya kazi nzito au mazoezi mazito,” alisema Malle.
Alisema kuwa kama mwathirika atafuata masharti hayo na kupata mlo safi, dawa hizo hazitamsababishia madhara.
Naye Meneja wa Mtandao wa Mashirika yanayopiga vita UKIMWI mkoani Kilimanjaro (KINSHAI), Veronica Shayo, alisema dawa hizo zinasaidia, isipokuwa watumiaji wengi wanakiuka masharti.
Alisema kuwa kama dawa zitatumika vizuri na kufuata lishe bora, waathirika wataishi vizuri.
“Inaonekana watu wengi wanaotumia na kupata matatizo ni wale wenye shida ya chakula,” alisema.
Tume ya Taifa ya Kupambana na UKIMWI (TACAIDS), imeshakanusha madai ya kwamba dawa hizo ni hatari kwa watumiaji.