VIONGOZI katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, wametakiwa wafanye vikao vya kikatiba mara kwa mara ili wananchi waeleze kero zao.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Meya wa Manispaa ya Temeke, Jerome Bwanausi, wakati wa ziara yake ya siku moja katika Kata ya Chamazi.
Bwanausi alisema katika vikao hivyo viongozi pia wanatakiwa watoe taarifa za mapato na matumizi ili wananchi wajue kazi zinazofanywa kutokana na kodi wanazolipa.
“Vikao vya kikatiba vinatakiwa kufanyika kila baada ya miezi mitatu, jambo ambalo husaidia wananchi kueleza matatizo yanayowakabili ili viongozi nao waweze kuyatafutia ufumbuzi matatizo yao mara moja,” alisema.
Aliwataka viongozi wa kata hiyo kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kujiletea maendeleo.
“Chamazi haitaweza kujengwa kukiwa na makundi, itajengwa watu wakiwa katika umoja,” alisema.
Meya Bwanausi aliwahahakishia wananchi hao kuwa watapata umeme ifikapo Septemba, mwaka huu.
Aliwataka wananchi hao kutokaidi fidia za miti kwenye maeneo yatakayoathiriwa na ujengaji wa nguzo za umeme.
Wakazi wa kata hiyo waliomba watengenezewe barabara katika mitaa.
Pia waliomba wawekewe matuta katika barabara kubwa ya lami inayopita katika kata hiyo ili kupunguza ajali.
Kwa upande wao, watendaji wa kata walilalamikia kutopewa nauli za kwenda na kutoka kwenye vikao vya wananchi. Meya aliahidi kulifikisha suala hilo katika vikao vya manispaa.