Wilaya ya Kibondo imepongezwa kwa jitihada zake za kulinda, kutunza na kuboresha mazingira zinazoshirikisha ngazi zote za serikali za vijiji, watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali.
Pongezi hizo zimetolewa leo na waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais anayeshughulikia mazingira Bw. Mark Mwandosya wakati akizungumza na viongozi wa wilaya baada ya kupokea taarifa ya wilaya iliyosomwa kwake na mkuu wa wilaya luteni Kanal John Mzurikwao.
Amesema taifa liko katika changamoto nyingi za kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa kikamilifu bila kuathiri shughuli za kijamii na kuongeza kuwa wananchi wanahitaji sasa kuhamasishwa.
Mheshimiwa Mwandosya amesema mikakati iliyowekwa na wilaya hiyo ya kuwashirikisha wananchi kwa kutunga sheria ndogondogo za vijiji ni nzuri na inasitahili kuwa darasa kwa wilaya nyingine nchini.
Hata hivyo waziri Mwandosya ameulaumu mkoa wa Kigoma kwa kukithiri katika uchomaji moto horela katika mapori na kuongeza kuwa pamoja na juhudi za kupambana nalo ipo haja ya kuongeza kasi zaidi.
Ameelezea kusikitishwa na kitendo cha kupokelewa na moshi wa moto uliokuwa ukiwaka katika mapori yliyoko kandokando ya barabara kuu itokayo Kigoma hadi wilayani Kibondo.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais anayeshughulikia mazingira profesa Mark Mwandosya yuko wilayani Kibondo kwa ziara ya siku mbili kukagua shughuli za mazingira.