TANZANIA imekabidhiwa uenyekiti wa taasisi ya siasa, ulinzi na usalama, ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kutokana na jukumu hilo, Rais Jakaya Kikwete, amezitaka wizara na idara zinazohusika na masuala ya ulinzi na usalama kuanza maandalizi ya kufanikisha jukumu hilo.
Alitoa wito huo jana wakati wa chakula cha usiku alichoandalia ujumbe wa Tanzania walioshiriki mkutano wa 26 wa kawaida wa SADC uliomalizika juzi mjini Maseru, Lesotho.
“Nimeona tule pamoja chakula cha usiku kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyofanya katika mkutano huu, tumekabidhiwa jukumu kubwa la kuongoza taasisi hii nyeti kwa miezi 12 ijayo.
“Nataka tuutambue wajibu huu na tujipange sasa na kuona namna gani tutawaongoza wenzetu katika SADC katika kipindi hicho,” alisema.
Alisema kuwa ni vema kwa wadau hao kujipanga sasa kwa kuwa hawawezi kujua nini, na wapi kutatokea nini.
Na kuongeza kuwa tayari taasisi ina pakuanzia ambapo alizitaja Malawi, Zimbabwe, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama nchi za kuanzia jukumu hilo.
Taasisi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndiyo hasa ‘moyo’ wa SADC. Kazi yake kubwa kwa nchi zinazounda utatu wa taasisi hiyo, ni pamoja na kushughulikia matatizo ya nchi mwanachama.
Hii ni dhima kubwa kwa Rais Kikwete kukabidhiwa nje ya mipaka ya Tanzania tangu aliposhika madaraka ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba, 2005.
Rais aliwaeleza wajumbe waliohudhuria mkutano huo ambao ni kutoka Wizara ya Ulizi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Wizara ya Usalama wa Raia; Idara ya Usalama wa Taifa; na Uhamiaji, kwamba katika umoja wao, wao ndio kiungo muhimu katika kufanikisha dhima hiyo.
Hata hivyo, alisema kwa Tanzania kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo, hakuiondolei wajibu wake wa kushiriki katika majukumu mengine ya kawaida ya SADC, lakini katika kipindi cha miezi 12, ufanisi wa taasisi hiyo chini ya uenyekiti wa Tanzania ni jambo ambalo halina mjadala.
Tanzania imekabidhiwa uenyekiti wa taasisi hiyo kutoka Namibia. Makamu mwenyekiti ni Angola. Na mjumbe wa tatu ni Namibia.
Akihitimisha mkutano wa 26 wa SADC, Waziri Mkuu wa Lesotho na Mwenyekiti wa SADC, Pakalitha Mosisili, alimpongeza Rais Kikwete kwa kukubali kwake kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.
Alisema kuwa taasisi hiyo ni muhimu kwa kuwa uendelevu wa mazingira ya ulinzi, usalama na mustakabali wa kisiasa ni mambo yanayopewa kipaumbele.
Mwenyekiti huyo wa SADC alisema kuwa jumuia haina shaka na uongozi wa Tanzania katika taasisi hiyo, na hasa kwa kuzingatia kuwa nchi hizo tatu zina uzoefu wa kutosha.
Alisema kuwa masuala yote yanayohusu siasa, ulinzi na usalama na mambo mengine yanayohusu SADC, yatachukua ajenda muhimu za jumuiya.
Aliwaomba viongozi wengine wakuu wa nchi na serikali kutoa ushirikiano wa kutosha.
Katika hatua nyingine, Tanzania imesaini Itifaki ya Fedha na Uwezeshaji, na Itifaki ya uwezeshaji kwa wananchi wa SADC kwenda nchi nyingine ndani ya jumuiya hiyo bila vikwazo.
Itifaki hizo mbili zilisainiwa na Rais Kikwete ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.
Lengo la itifaki ya fedha na uwezeshaji ni kuchangia uanzishwaji wa soko la pamoja katika SADC, kwa kuendeleza na kukuza ushirikiano kati ya nchi wanachama katika nyanja za fedha na uwekezaji.
Sera zinazoainishwa katika itifaki hiyo ni pamoja na kujenga uchumi wa jumuiya kwenye viashiria vya kiuchumi vyenye mwelekeo unaofanana, kuainisha sera za kodi na fedha, kuhakikisha ukuaji wa akiba na uwekezaji ndani na nje ya jumuia, kushirikiana katika masuala ya kibenki na asasi zisizo za kibenki na kushirikiana katika menejimenti ya shughuli za asasi za kifedha kimaendeleo.
Hata hivyo si nchi zote wanachama wa SADC zilizosaini itifaki hii, kwa maelezo kwamba zile ambazo hazikusaini zilihitaji kufanya majadiliano zaidi na mabunge na wanasheria wao.
Itifaki hizo pia zinalenga kuwawezesha wananchi katika nchi wanachama wa SADC kusafiri bila vikwazo na kuondoa viza.
Hata hivyo, bado sheria za uhamiaji katika nchi hizo zitapaswa zifuatwe.
Baada ya Rais Kikwete kusaini itifaki hizo, kitakachofuata sasa ni kuzifikisha bungeni ili zijadiliwe na ikiwezekana, ziridhiwe.