MFANYABIASHARA maarufu nchini, Jacqueline Noni, amemchangia mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Tausi Ibrahim (17), sh 200,000 baada ya kusoma habari zake.
Tausi anasoma Shule ya Sekondari ya Manyara wilayani Monduli, Arusha.
Noni, alisema mwishoni mwa wiki kwamba ameguswa mno na msichana huyo baada ya kusoma habari za kujitokeza kwake mbele ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na kueleza matatizo ya ada yanayomsibu.
Tausi, alijitokeza kwenye mkutano wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na kueleza shida yake ya ada, na kisha Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya mkoani Arusha, Thomas Laizer, aliahidi kanisa kumsomesha hadi ukomo wa elimu yake.
Noni alisema baada ya msaada huo, msichana huyo sasa anapaswa afunguliwe akaunti ili wasamaria wema wamwekee fedha za kumsaidia.
“Namshukuru na kumpongeza Baba Askofu kwa msaada wa kumlipia ada, sasa walio karibu inabidi wamfungulie akaunti ili aweze kusaidiwa zaidi.
“Mimi naahidi kumsaidia sh 200,000, ingekuwa rahisi zaidi kwake kuzipokea kama angekuwa na akaunti, nawaomba walio karibu naye wamfungulie akaunti mapema,” alisema.
Noni alisema fedha hizo zitamsaidia Tausi katika matumizi na mahitaji mengine, hasa ikizingatiwa kuwa yeye kama msichana, ana mahitaji muhimu.
Tausi, akitokwa machozi, alimweleza Lowassa kwamba anakabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa ada.
“Nimehangaika sana kwa kukosa ada…sina baba (alishakufa) na mama yangu ni kilema, hawezi kuhangaika, niliposikia unakuja nikalazimika kutoroka shule kwa sababu mwalimu alininyima ruhusa ya kuja huku,” alisema Tausi huku akilia