Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mkurugenzi wa Jiji Mwanza alighushi?
Mkurugenzi wa Jiji Mwanza alighushi?
By Habari Tanzania | Published  08/21/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Jovin Mihambi, Mwanza

UUZAJI nyumba za serikali unazidi kuwachanganya viongozi mkoani Mwanza baada ya Kikao cha Baraza la Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitisha azimio likitaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Paul Baruti, akamatwe na kushitakiwa kwa kuuza nyumba tatu mali ya jiji hilo.

Uamuzi wa kikao hicho ulifikiwa mwishoni mwa wiki baada ya kutolewa hoja maalumu na Diwani wa Kata ya Kirumba, Richard Rukambura, iliyotaka kujadiliwa juu ya hatima ya nyumba za halmashauri hiyo zilizouzwa mwaka jana. Ziliuzwa kwa watumishi, akiwamo Baruti, bila kuhusisha Baraza la Madiwani. Baruti alihamishiwa Tanga.

Rukambura alisema licha ya suala hilo kujadiliwa kwa muda mrefu katika vikao, na baraza hilo kuagiza nyumba hizo zirejeshwe, agizo hilo halijatekelezwa.

Nyumba hizo inadaiwa ziliuzwa sh milioni 8 kila moja; kiasi ambacho ni chini ya thamani halisi.

Akichangia hoja hiyo, Diwani wa Butimba, Dismas Masunu, alisema kutokana na kuzungushwa zungushwa kwa muda mrefu na watendaji, kikao kinapaswa kutoa uamuzi mzito ili mali hizo za wananchi zirejeshwe.

“Nyumba hizi ni mali ya wana Mwanza, leo hatuwezi kukubali ziondoke hivi hivi, na kwa kuwa watendaji tumewaagiza kila mara katika vikao nyumba hizo zirejeshwe, na kutofanya hivyo, wanapaswa kuwajibika,” alisema Masunu.

Diwani Yahaya Nyehonge wa Kata ya Mirongo, alisema kwa kuwa Baruti alidanganya kuhusu uuzaji wa nyumba kwa kuandika barua kuwa nyumba hizo ni mali ya Serikali Kuu, anastahili kukamatwa na kushitakiwa.

“Kwa mujibu wa kifungu namba 28(1) cha kanuni za Serikali za Mitaa na Mamlaka za Miji na Maadili ya Madiwani za mwaka 2000, madiwani kupitia kikao chetu tunayo haki ya kumwajibisha,” alisema Yahaya.

Akichangia hoja hiyo, Diwani Fue Kandawala alisema nyumba hizo ziliuzwa kinyume cha utaratibu, huku Mwanasheria wa Jiji akiwapo.

Alisema kwa uzembe huo, mwanasheria huyo naye anastahili kushitakiwa.

Akijibu hoja za madiwani hao, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Emmanuel Kalobelo, alisema Baruti aliuziwa nyumba hizo chini ya utaratibu wa Serikali Kuu.

Alisema kutokana na kikao kuagiza nyumba hizo zirejeshwe, waliwasiliana na Wakala wa Majengo (TBA) ambaye alilipeleka suala hilo kwa Mwanasheria wa Serikali ili kupata ushauri juu ya hatua za kuchukua.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Diwani John Minja wa Kata ya Igogo, ambaye aliteuliwa kuongoza kikao hicho kushika nafasi ya Meya aliyekuwa safarini, alisema kikao hakina sababu za kungojea uamuzi wa Mwanasheria wa Serikali.

Alisema hawawezi kusubiri kwa kuwa nyumba ziliuzwa baada ya Baruti kudanganya kuwa si mali ya jiji, bali ya Serikali Kuu.

Kikao kiliazimia kuwa waliomo kwenye nyumba hizo wanapaswa kuhamishwa haraka. Kisha nyumba hizo ziwekwe chini ya ulinzi maalumu wa polisi na kukabidhiwa kwa mkurugenzi mpya.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.