WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema wakuu wa wilaya waliopangwa katika maeneo ya wafugaji, mbali ya kuwa na kazi zao za kila siku, wana kazi ya ziada ya kuhakikisha wanawabana wazazi ambao wanawatorosha mabinti zao kutoka shule ili waozwe.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Lolkisale mjini hapa juzi, Waziri Mkuu alisema wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanawakamata wazazi wenye tabia hiyo, pamoja na wanaume wote wanaooa wanafunzi au wanaokataa kupeleka watoto shule.
“Ninasema ma – DC hawa wana kazi kubwa ya kukamata watu wote wanaokataa kupeleka watoto shule au kuwatorosha shule na kuwaoza, wakiwamo wanaume wanaowatia mimba wasichana wanaosoma. Ninawaomba muwaache wamalize shule…msiwaoe kabla hawajamaliza shule,” alisisitiza.
Lowassa alisema amefurahia ziara yake katika kata hiyo, kwa vile amelazimika kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa matatu ya Shule ya Sekondari ya Irkisale. “Nataka shule hii ianze kupokea wanafunzi mwakani, kwa hiyo nitarudi Januari mwakani kuja kuizindua,” alisema.
Ili kuongeza kasi ya ujenzi wa shule hiyo, Waziri Mkuu alichangia sh milioni tano na mabati 500. Aliahidi kuboresha ujenzi wa barabara katika kata hiyo iliyopo jimboni kwake, kwani ni ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi. Pia aliahidi kufuatilia ujenzi wa barabara kutoka Tukusi hadi Kilimatinde.