UUZAJI wa shamba la Mbarali sasa umechukua sura mpya baada ya taarifa mpya kuvuja, kuwa rushwa imetembea katika vyombo vya serikali vilivyokabidhiwa majukumu.
Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), imetajwa kuhusika kwa karibu zaidi katika kufanya mchezo huo mchafu kwa shamba la Mbarali.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa PSRC imeshinikizwa na mmoja wa mawaziri ambaye amekuwa na urafiki wa karibu na mnunuzi wa shamba hilo.
Kilichotokea katika mkataba wa awali, mnunuzi alikubaliana na serikali katika Memorandum Of Understanding (MOU) kuwa angelipa sh bilioni 3.5 yaani sh milioni 3,500, iwapo angeshinda zabuni na kuuziwa shamba hilo.
Utaratibu wa malipo ilikuwa ni kutoa asilimia 10 ya zabuni, ambayo ni sh milioni 350 ambazo mwekezaji, Kampuni ya Highland Estate Limited ilizitoa na kushinda zabuni.
Utaratibu kama huo ulitumika kubinafsisha shamba la Kapunga kwa Kampuni ya Export Trading Limited, ambayo yenyewe iliwasilisha zabuni ya sh bilioni 3.0 sawa na sh milioni 3,000.
Export Trading Limited wao walilipa asilimia 10 ambayo ni sh milioni 300 kama ilivyokubaliwa kwenye MOU na baada ya kushinda zabuni, walilipa asilimia 90 iliyosalia kwa mujibu wa makubaliano katika MOU.
Mwekezaji huyo tayari ameanza maandalizi ya kulifufua shamba hilo la Kapunga na sasa ameanza kunusuru miundombinu iliyokuwa inaanza kuoza ambayo ingekuwa hasara kubwa kwa walipakodi kwani ni fedha zilizowekezwa na serikali kutokana na jasho la kodi za wananchi.
Hata hivyo, kwa mshangao Kampuni ya Highland Estate Limited, inaelezwa kuwa kwa maelezo ya Waziri wa Kilimo na Chakula, Joseph Mungai, hadi sasa haijalipa asilimia 90 iliyosalia ambayo ni sh milioni 3,150 au bilioni 3.15.
Kilichotokea, Mungai kwa kushirikiana na PSRC wamebadili MOU iliyotumika kushinda zabuni na sasa mpya (nakala tunayo) inasomeka kuwa mwekezaji ataongeza asilimia 10 katika asilimia 10 ya awali, na asilimia 80 inayosalia atailipa wakati akiendesha shamba hilo.
“Hii ina maana wanahesabu sh milioni 350 aliyolipa wakati anaomba zabuni, wanataka aongeze sh milioni 350 nyingine ziwe sh milioni 700, basi. Apewe shamba. Eti hizo sh milioni 2,800 zinazosalia atalipa siku za usoni, bila kutaja atazilipaje,” kilisema chanzo chetu kutoka PSRC.
Mtoa habari alisema kubinafsisha mashamba si tatizo, lakini tatizo linajitokeza pale harufu ya rushwa na ukiukwaji wa sheria za nchi unapojitokeza, hali inayoashiria kuwa taifa sasa linarejea lilikotoka.
Chanzo chetu kilifafanua kuwa, MOU mpya aliyoandaliwa mwekezaji Highland Estate Limited, amekabidhiwa wiki iliyopita, bado anawasiliana na wanasheria na haijatiwa saini hadi leo kubadili ile ya awali, lakini hayo ndiyo makubaliano.
Huku hayo yakiendelea, Mkuu wa Mkoa (RC) wa zamani (jina linahifadhiwa) ametajwa kumiliki pande kubwa la shamba la Mbarali, hivyo naye anawatumia wananchi kupinga ubinafsishaji wa shamba hilo.
Kiongozi huyo na wenzake, wanatajwa kuwa hawawekezi chochote katika shamba hilo na wala hawalipi kodi, hali inayowafanya waendelee kuishi kiujanja ujanja.
Ubinafsishaji wa shamba la Mbarali hivi karibuni umeibua mgogoro mzito, ambapo Waziri wa Fedha wa zamani, Edwin Mtei, alishauri serikali itumie utaratibu wa kuwagawia wananchi shamba hilo.
Hata hivyo, hata kabla hilo halijafikiriwa, hata huyo aliyedhaniwa kuwa ni mwekezaji sasa huenda akapewa shamba hilo kwa bei ya kutupa isiyoifaidisha serikali wala wananchi.
Wakati huo huo, habari tulizopata wakati tunakwenda mitamboni, zinasema kuwa wawekezaji wa shamba la Kapunga jana walipata ajali wakati Mungai na Waziri wa Mipango na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, walipokwenda huko kutembelea shamba jana.
Waliopata ajali ni maofisa watatu na walilazwa katika Hospitali ya Mission Chimala. Gari walilopata nalo ajali ni T 953 ANW, walikuwa wakiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Seif. Habari hizo zimethibitishwa na Meneja wa shamba la Kapunga, Melckisedek Salo.