WAKATI uchaguzi mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania COTWU (T), unafanyika mjini Morogoro leo, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, Doroth Uiso, amesema hatakubali matokeo ya uchaguzi huo kama hautaongozwa na katiba iliyopo.
Uiso alitoa kauli hiyo ofisini kwake juzi alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyotolewa na wanachama wa chama hicho kwamba Baraza Kuu lililokutana Desemba, 2005 lilifanya mabadiliko ya vifungu vya katiba kwa faida ya uongozi uliopo madarakani.
Uiso alisema hajapata taarifa kutoka kwa uongozi wa juu wa chama hicho kuhusu mabadiliko ya katiba, na kwamba bado anaitambua katiba iliyopo ofisini kwake ambayo bado haijabadilishwa.
Malalamiko ya wanachama hao, wengi wakiwa ni kutoka Shirika la Posta Tanzania, yemekuja kutokana na hatua ya chama hicho kufuta kanda mbili, kati ya saba zilizokuwapo awali.
Baraza Kuu la COTWU (T) lililokutana Desemba, 2005, kinyume cha katiba yake, lilifanya marekebisho hayo na kufuta kanda ya Mtwara na Dodoma. Kanda zilizobaki ni Dar es Salaam, Kaskazini, Kati, Ziwa na Mbeya.
Licha ya kubadili kipengele hicho, wajumbe wa Baraza Kuu pia walifuta kifungu kinachoruhusu chama kuwa na manaibu makatibu wawili, na sasa anatakiwa achaguliwe mmoja pekee. Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, kifungu cha 50 Ibara ya 6, Mkutano Mkuu wa COTWU (T) ndio wenye jukumu la kupitisha, kurekebisha na au kufuta kifungu chochote katika katiba ya chama, na si Baraza Kuu kama uongozi ulivyofanya.
Bila ya kusubiri ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu, uongozi wa COTWU (T) umeshatumia vifungu hivyo kuendesha uchaguzi katika ngazi ya kanda, ambako ni kanda tano tu ndizo zilizofanya uchaguzi badala ya kanda saba.
Akizungumzia hatua hiyo, Msajili wa Vyama alisema, hatambui kuwapo mabadiliko ya vifungu katika katiba ya chama hicho kwa kuwa bado hajapelekewa taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa juu.
“Mimi naitambua katiba hii niliyonayo hapa kwangu, kama watakuwa wamefanya uchaguzi kwa kutumia katiba wanayoijua wao ambayo mimi sijaisajili hapa, hilo watajua wao,” alisema.
Alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa COTWU (T) Taifa, Omar Guledi, alikiri uchaguzi kufanyika katika kanda tano badala ya saba, akidai mwenye kufahamu hilo ni Mtendaji Mkuu wa chama hicho, Charles Sammang’ombe.
Alipotakiwa kueleza uhalali wao kutumia kikao cha Baraza Kuu kubadili vifungu vya katiba, alikata simu.
Akizungumza kwa simu, Katibu Mkuu wa COTWU (T), Charles Sammang’ombe, hakuwa wazi. Alimtaka mwandishi aende Morogoro ili akapate maoni ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Tangu wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari na wa Kampuni ya Simu wajiondoe katika chama hicho na kuunda vyama vyao, mwenendo wa chama hicho umekuwa wa kuyumba yumba.
Mmoja wa wanachama wa chama hicho kutoka Shirika la Posta, Resterius Kamuziba, amesema kwamba, matumizi mabaya ya fedha ni moja ya sababu ambazo zitakifanya chama hicho kiendelee kusambaratika.
Viongozi kadhaa wanadaiwa kufuja fedha za chama kwa kununua magari bila ya kufuata taratibu za zabuni.
Katika kipindi cha mwaka 1996-2002, chama hicho kilitumia sh milioni 129.2 kununua magari bila kutumia njia ya zabuni.