KAMPUNI hewa ambayo inajitambulisha kuwa inahusika na mashamba ya ufugaji mbuni mkoani Arusha, inadaiwa kuendesha vitendo vya utapeli jijini Dar es Salaam kwa kutumia jina la Rais Jakaya Kikwete na la Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Shukuru Kawambwa.
Mmoja watu walioonja chungu ya kutapeliwa, alisema kwamba, matapeli hao wameweka makazi yao ya muda katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Jina hewa la kampuni hiyo kwa sasa tunalihifadhi.
Wanaendesha vitendo vya kitapeli kwa kuwafanyia usaili baadhi ya watu wenye kusumbuliwa na tatizo la ajira.
“Wanamsimamisha kila mtu anayepita eneo hilo, ukisimama wanakuuliza kama una shida ya ajira - wewe binafsi au ndugu yako - hawajali kiwango chako cha elimu, kwa kuwa asilimia kubwa ya watu hawana ajira huwakubalia, baada ya usaili hutakiwa walipe sh 5,000 halafu hutaka mhusika asubiri matokeo, humpa stakabadhi,” alisema mmoja wa waathirika.
Watu hao hudai kwamba watu watakaochaguliwa, kabla ya kupelekwa Arusha kwenye mashamba hayo, watakutana na Dk. Kawambwa ili awape utaratibu.
Watuhumiwa hao wanadai wana baraka kutoka kwa Rais Kikwete, na kwamba mara kwa mara huenda Ikulu kwa wito wa Rais ambaye anawachukulia kama wakombozi wa ahadi zake za kutoa ajira.
Juzi mwandishi wa habari hizi alifika Mnazi Mmoja na kukutana na mmoja wa matapeli hao, ambao ni nadhifu.
“Wote mnaohitaji kufanya usaili nisubirini nitakuja baada ya muda mfupi, nimeitwa Ikulu na Rais Kikwete mara moja nadhani tutaonana baada ya nusu saa,” ndivyo alivyoelezwa mwandishi wetu pamoja na wote waliokuwa wakisubiri kufanyiwa usaili.
Hata hivyo tapeli huyo hakutokea hadi baada ya saa tatu wakati baadhi ya watu walipoanza kukata tamaa ya kufanyiwa usaili.
Baadaye ilitolewa kauli kwamba ‘ofisa’ huyo alikuwa katika mazungumzo marefu na Rais ambaye alikuwa akijiandaa kwenda Lesotho; na akawataka waonane baada ya siku mbili.
Katika hali ya kusataajabisha, wengi walioibiwa sh 5,000 kutokana na usaili huo, walionekana kuamini maneno ya matapeli hao.
Tanzania Daima ilikwenda kwa Msajili wa Kampuni kujua kama kweli kuna kampuni yenye jina hilo iliyosajiliwa kufanya kile inachofanya.
Hapakuwapo na jina la kampuni hiyo wala taarifa nyingine za kuthibitisha kile wanachofanya.