KUMALIZIKA kwa Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, kumetoa sehemu ya picha halisi ya utendaji kazi wa mawaziri na naibu mawaziri.
Wananchi, kupitia televisheni, redio na magazeti, wamefanikiwa kuwajua na hata kuwaweka katika madaraja, baadhi ya mawaziri hao.
Tanzania Daima, kwa siku kadhaa sasa imekuwa ikizungumza na wananchi mbalimbali ili kupata maoni yao juu ya utendaji kazi wa mawaziri na naibu mawaziri.
Karibu wote waliohojiwa, walimtaja Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, kama mmoja wa wanasiasa wakongwe ambao, ama wanastahili kupumzishwa, au kubadilishwa wizara.
Wamemwelezea Mramba kama kiongozi asiyekuwa makini, na ambaye ameshaonyesha wazi kushindwa kuimudu Ari, Nguvu na Kasi (ANGUKA).
“Tangu awali Rais alipotangaza Baraza la Mawaziri, wengi hatukufurahishwa na Mramba kupewa wizara nyeti ya Miundombinu, amefanya kazi siku nyingi, hana jipya,” alisema Musa Hamad, mkazi wa Kariakoo.
Mramba alijichongea zaidi baada ya wabunge kumbana kuhusu fungu nono la fedha alizojigawia kwa ajili ya barabara moja katika eneo lake.
Kibaya zaidi, ni jinsi alivyobabaika wakati wa kujibu hoja za wabunge. Kwa mtazamo wa waliohojiwa na Tanzania Daima, Mramba ameonyesha kupwaya.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Juma Kapuya, ameandamwa, ingawa haielezwi hasa dosari yake kuu ni ipi.
Ameonyesha kutokuwa na mvuto katika wizara hiyo, ingawa anaonekana kukubalika katika wizara nyingine.
Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, hakuwavutia wengi katika mkutano uliomalizika, pengine kutokana na kuzoeleka kwa muda mrefu.
Waliohojiwa wamemwelezea Dk. Ngasongwa kama mmoja wa mawaziri waliotoa majibu ya kisiasa zaidi, badala ya kutoa majibu yanayolenga kumaliza kero za wananchi.
Wizara ya Mipango imeelezwa kwamba bado ni wizara ya kukusanya takwimu, badala ya kuwa kitovu cha ubunifu na ujenzi wa mwelekeo sahihi wa uchumi wa nchi.
Wengi waliohojiwa wanamkubali Dk. Ngasongwa kama mmoja wa wasomi mahiri, lakini ambaye hastahili kuendelea kuwa waziri, hasa katika dunia ya leo ambayo inabadilika kwa kasi ya ajabu.
Waziri wa Teknolojia, Sayansi na Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla, bila shaka huyu wanafunzi wengi wa elimu ya juu wangependa kumwona akiwa nje ya wizara hiyo.
Kauli za kujikanganya kuhusu mikopo ya wanafunzi, ni mambo yaliyomshushia umaarufu. Wengi sasa wanamwona kama kiongozi asiye makini na ambaye hana jipya katika wizara hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, James Mungai, kelele za kumtaka ang’atuke au ang’atuliwe, zimeshasikika.
Mungai, Waziri ambaye alishawahi kupata misukosuko hadi akawekwa kando na Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anapata upinzani mkubwa.
Kitendo cha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, kupangua mengi aliyoacha Mungai katika wizara hiyo, kumemfanya (Mungai), aonekane kuwa si kiongozi makini, na asiyekuwa na mipango madhubuti.
Wizara aliyonayo sasa, ukubwa na unyeti wake, vikichaganywa na umri alionao, vinatosha kuwafanya wananchi wajenge hoja ya kutaka awekwe kando.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, bado ni kivutio, ingawa wananchi wanalalamika kwamba amekuwa mkimya mno.
Wangependa kuona akitema cheche kama alizokuwa akitema wakati akiwa Wizara ya Ujenzi katika serikali iliyopita.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nazir Karamagi, anaelezwa kama mmoja wa mawaziri wenye viburi.
Suala la Mchuchuma linaonekana kumtafuna, na kwa hakika si wananchi wengi ambao wangependa kuona akiiendesha wizara kutokana na utashi wake, huku akipuuza maoni ya wadau wengi.
Naibu mawaziri kama Lawrence Masha, Dk. Diodorus Kamala, Bernard Membe, Mustafa Mkulo, Dk. Makongoro Mahanga, Dk. Emmanuel Nchimbi, Salome Mbatia, na wengine kadhaa, wameonyesha ukomavu katika kujibu maswali.
Hali hiyo inazidi kuwaweka katika mazingira mazuri ya ‘kufikiriwa’ baadaye.