KUNDI la muziki wa kizazi kipya, TMK Wanaume Family, limebadili ratiba ya uzinduzi wa albamu tatu za pamoja na wasanii Juma Kassim ‘Sir Nature’, Amani Abbas Temba ‘Mh Temba’ na Rashid Ziada ‘KR Mullar’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Meneja wa kundi hilo, Saidi Fella, alisema kwamba uzinduzi huo sasa utaanzia jijini Dar es Salaam Septemba 8, mwaka huu badala ya Septemba 15 ya awali.
Alisema kwamba mabadiliko hayo yametokana na Ukumbi wa PTA waliopanga kufanyia uzinduzi Septemba 15 kutumika kwa kazi nyingine na hivyo wamelazimika kurudisha nyuma kwa wiki moja.
“Tumebadili ratiba yetu ya uzinduzi, hivyo sasa tutaanzia Dar es Salaam badala ya Arusha, tutazindua Septemba 8 na Septemba 9, kama kawaida tutazindua Tripple A jijini Arusha, na Septemba 19 tutazindua Mwanza. Mchana tutakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na usiku tutazindua kwenye Ukumbi wa Capri Cabana,” alisema.
Fella alisema kwamba mbali ya kuzindua, pia watauza mavazi na viatu vyenye nembo ya kundi hilo kwa bei ya kawaida ili mashabiki wao waweze kununua.
Sir Nature anazindua albamu ya nne iitwayo ‘Zote Historia’, wakati Mh Temba anazindua albamu ya pili aliyoipa jina ‘Ipo Siku’ na KR Mullar anazindua albamu yake ya kwanza iitwayo ‘Kamua kwa Uwezo’ zilizoko sokoni.