MARA nyingi nimekuwa katika mijadala isiyo rasmi na kaka yangu ambaye ni mpenzi sana wa kusoma magazeti, na naweza kusema kuwa licha ya kuwa si msomi, lakini usomaji wake magazeti umemfanya awe mmoja ya wajengaji hoja wazuri na wenye mchango mwanana tunapojadili mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.
Mara kadhaa ameikosoa serikali kwa mengi, nami mara nyingi nimekuwa nikimueleza kuwa si kila jambo litafanywa na serikali. Kwanza serikali ni nani? Je, serikali ni rais na Baraza la Mawaziri? Je, serikali ni wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya? Serikali ni nani?
Kwangu mimi, serikali ni mwananchi mwenyewe, kama tulivyozoea kusema mjenga nchi ni mwananchi vivyo hivyo mvunja nchi ni mwananchi. Kamwe nchi haijengwi na rais na mawaziri au wabunge peke yao. Nchi inajengwa na wananchi. Lakini ili kujenga nchi wananchi hawana budi kubadilika kifikra kwa kuhabarishwa na pia kujihabarisha ili wafahamu ni kitu gani kinaendelea ndani ya nchi na nini mchango wao katika hicho kinachoendelea.
Kwa mfano, serikali imetoa sh milioni 500 kwa kila mkoa. Pamoja na kuwa ni wajibu wa serikali kuwahabarisha katika jambo hili, lakini pia ni jukumu na wajibu wa wananchi kujihabarisha zaidi na kufahamu ni kwa namna gani watanufaika na mpango huo wa serikali. Bila kuhabarishwa na kujihabarisha, ni vigumu kwa wananchi kuchangia maendeleo, zaidi mwananchi atabaki analalamika, ooh srerikali, ooh serikali.
Serikali kwa upande wake inaweza kuwa imeshahabarisha juu ya jambo fulani, suala linalofuatia ni wananchi kujihabarisha. Kama wananchi hawajihabarishi kuna hatari ya mchango wao katika maendeleo kukosekana na pia hata mchango wa serikali kwa ajili ya maendeleo yao kupotea bure.
Kujihabarisha kuko kwa namna nyingi, baadhi ya watu wanadhani kwamba mpaka uwe msomi wa kiwango cha chuo kikuu ndipo uweze kujihabarisha. Si hivyo, kujihabarisha ni wajibu wa kila mwananchi kwa njia zozote, iwe ni redio, magazeti, televisheni, mazungumzo vijiweni, mikutano ya hadhara vijijini na mijini na kuhoji.
Kuna wasomi lukuki wa kiwango cha chuo kikuu ni mbumbumbu kabisa linapokuja suala la kujihabarisha. Nenda kwa mfano kwenye vyuo vya elimu ya juu, ujaribu kufanya mazungumzo ya kawaida kuhusu nini kinaendelea duniani na hapa nchini, nakuhakikishia ni wachache watatoa hoja zenye kujenga. Wengi watapiga porojo, kwa nini? Kwa sababu hawajajihabarisha, hawako informed, huu ndio ukweli.
Makala yangu itamzungumzia Hugo Chavez na jinsi ambavyo ameleta mabadiliko katika nchi ya Venezuela. Hata hivyo, pamoja na kutumia muda mwingi katika kumuelezea rais huyu maarufu hivi sasa duniani kote, nia yangu ni kuonyesha kuwa ameweza kufanikiwa katika mengi mazuri anayoyafanya katika nchi yake na bara zima la Amerika Kusini kutokana na kuungwa mkono na wananchi wake ambao wanahabarishwa na pia wanajihabarisha.
Hapa kwetu wananchi wengi kama si wote wanamuunga mkono Rais Jakaya Kikwete na serikali yake, lakini ifahamike kwamba kumuunga mkono huku hakutoshi kama hatutoi mchango wowote katika mipango na mikakati lukuki ya maendeleo ili kujiletea maisha bora kwa kila mmoja wetu.
Nimetolea mfano tu wa sh milioni 500 katika kila mkoa, lakini yapo mengi. Kuna mikakati ya kukuza kilimo, au tuseme mapinduzi ya kilimo, kuna ruzuku ya mbolea, mikopo ya pembejeo nk. Serikali tayari imeshahabarisha. Je, ni wananchi wangapi ama mmoja mmoja au kwa kupitia vikundi wameshajihabarisha, kuuliza na hata kuhoji kwamba watanufaika vipi kuhusu mipango hii mizuri ya kukiinua kilimo?
Hugo Raphael Chavez anatajwa na baadhi ya maadui zake, hasa Marekani, kama dikteta namba mbili baada ya Fidel Castro wa Cuba, lakini kwa upande wa pili anatajwa kama mtu mpigania haki za wanyonge, mpenda umoja wa eneo la Amerika Kusini maarufu kama Latini Amerika, mzalendo halisi aliyebadilisha maisha ya watu wa kawaida kwa kiwango cha kipekee.
Chavez amethubutu kufanya kile ambacho serikali nyingi za Amerika Kusini zimeshindwa kufanya kwa zaidi ya miongo minne, nacho ni kuacha kutegemea na kuegemea utawala wa Marekani katika uamuzi wao muhimu kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Chavez alipoingia madarakani, alianzisha sera ya kuzitaka kampuni kubwa za mafuta kukubali kufanya kazi kwa ubia na kampuni inayomilikiwa na dola ijulikanayo kama Petroleos de Venezuela. Chavez amethubutu kuzikomalia kampuni kubwa kama Shell, BP, TOTAL nk na kuzitaka ama kuondoka au kufanya biashara kwa mujibu ya matakwa ya watu wa Venezuela.
Ikumbukwe kwamba hili si jambo dogo, unapozungumzia kampuni hizi, unazungumzia uchumi wa dunia, uchumi wa wakubwa. Hizi ni kampuni ambazo zinaweza kuiondoa serikali madarakani na hata kuiweka serikali zinayoitaka. Lakini kwa Venezuela, jitihada zao za kumuondoa Chavez mwaka 2002 ziligonga ukuta baada ya kile kinachoitwa nguvu ya umma kumrejesha madarakani katika mapinduzi yaliyodumu kwa muda wa siku mbili tu.
Kampuni hizi kubwa duniani zilichemsha kwa sababu umma wa wananchi wa Venezuela unaelewa kile ambacho serikali yao inafanya katika kuwaletea maisha bora. Umma huu umebadilika kifikra na kuamini kwamba maendeleo yao yataletwa na wananchi wenyewe na si kampuni kubwa za mafuta. Umma huu umebadilika kifikra kutokana na kuhabarishwa na pia ukajihabarisha na ndio maana haikuwa rahisi kwa kampuni hizo na wengine kufanikisha azma yao ya kumuondoa Chavez madarakani.
Ingekuwa Wavenezuela hawajahabarishwa, hawajajihabarisha, hawajabadilika kifikra, nina hakika leo hii nchi hiyo ingekuwa chini ya kibaraka wa wakubwa mwenye kulinda maslahi ya kampuni hizo ili yaufyonze uchumi wa Venezuela kama ambavyo tunashuhudia Ghuba ya Uajemi na kwingineko kwenye mafuta.
Chavez amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya kizalendo na kupinga waziwazi sera za soko huria ambazo anadai (na ndivyo ilivyo) kuwa zinawakandamiza walio wengi. Chavez haamini kabisa katika uchumi wa soko na ndio maana yeyote mwenye kutaka kufanya biashara na Venezuela sharti aingie ubia na kampuni zinazomilikiwa na serikali.
Chavez ameiongoza Venezuela tangu mwaka 1999. Na tangu wakati huo, Venezuela imeibuka kama taifa ambalo uchumi wake unakua kwa kasi kutokana na rasilimali muhimu duniani; mafuta na gesi. Mara kadhaa na mpaka sasa, ameingia katika mizozo na wakubwa akiwashutumu kwa njama za kuondoa kila utawala ambao unapinga matakwa yao.
Hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa Rais George W. Bush wa Marekani hana tofauti na Adolph Hitler. Mara nyingine amemshambulia na kumuita ni mlevi. Miezi michache iliyopita, Balozi wa Marekani nchini Venezuela, William Brownfield inadaiwa alirushiwa mayai viza akiwa katika moja ya safari zake za kikazi.
Majuzi amemrejesha nyumbani balozi wake katika Israel, akipinga vita ya Mashariki ya Kati. Utaona kwamba huyu ni mtu ambaye anathubutu kukabiliana na wakubwa. Si kwa sababu ya mafuta aliyonayo tu, hapana, bali nguvu ya umma. Umma uliohabarishwa, ukajihabarisha na kubadilika kifikra uko nyuma yake. Hii ndio nguvu na jeuri pekee ya Chavez na si mafuta au makombora na madege ya kivita anayoyanunua kutoka Urusi, la hasha, ni nguvu ya umma.
Chavez anapozungumza anajiamini. Alipoulizwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) juu ya hofu ya kuvamiwa na Marekani kama ilivyotokea huko Iraq na kama ambavyo Iran iko pia katika tishio hilo, alisema: “Nakuambia Wamarekani watageuka mavumbi hapa, na kabla ya hapo ujue vita hiyo itapigwa miaka 100 mpaka Mvenezuela wa mwisho, nawaonya, wasithubutu hata kufikiria jambo hilo.” Alikuwa anajiamini kabisa.
Kujiamini huku kwanza kunatokana na ukweli kwamba Chavez ameibadilisha Venezuela kwa kiwango kikubwa, si tu kiuchumi bali pia kisiasa, kifikra na hata kimtazamo. Mabadiliko haya, hasa ya kifikra, si tu kwamba yanaonekana nchini Venezuela peke yake, bali sehemu kubwa ya Amerika Kusini yote imejikuta katika wimbi la U-Chavez kutokana na serikali nyingi kuiga au kufuata mtazamo wa Chavez, wa kulinda na kujali zaidi maslahi ya wananchi kuliko ya kampuni za kibiashara licha ya kwamba zinalipa kodi.
Tayari huko Bolivia, Evo Morales mara tu baada ya kuchaguliwa ameonyesha nia ya wazi ya kupigania maslahi ya wanyonge badala ya kuegemea kwa kampuni za kibiashara ambazo nyingi ni za kutoka Marekani na Ulaya Magharibi. Nchini Peru, mgombea mwenye kupinga utandawazi na mfumo wa soko huria, Ollata Humala alikaribia kuibuka mshindi katika uchaguzi ambao ulilazimika kuingia katika duru ya pili. Pamoja na mgombea huyo wa Peru kushindwa, mwamko wa fikra miongoni mwa raia wa nchi hiyo maskini umekuwa wa hali ya juu.
Nchini Mexico, kama si jitihada binafsi za rais aliyemaliza muda wake, Vicente Fox za kuamua kuvunja sheria za uchaguzi na kumkampenia Felipe Calderon, ilikuwa ni wazi mgombea mwenye kufuata siasa za mlengo wa kushoto, Andres Manuel Lopez Obrador angeibuka mshindi.
Kutokana na mkakati wa Chavez wa kuziwekea masharti magumu kampuni kubwa za mafuta, pato la serikali limeongezeka maradufu, na sasa serikali imeboresha huduma za jamii kwa kiwango cha hali ya juu. Maisha ya mtu wa kawaida yamebadilika. Hajaishia hapo, Chavez amekuwa akitoa misaada na ufadhili kwa nchi za jirani. Kwa mfano anagharamia matibabu ya upasuaji wa macho kwa Wamexico masikini wenye asili ya India.
Kiwango anachotoa Chavez kusaidia majirani katika Bara la Amerika Kusini kinatajwa kuzidi marudufu ya kile ambacho kinatolewa na Marekani kama msaada kwa nchi hizo. Wakati Marekani inatoa jumla ya dola bilioni mbili, Chavez alitumia zaidi ya dola bilioni tatu kama misaada.
Kituo cha utafiti na sera cha Caracas kinasema katika takwimu zake kwamba Chavez ametumia zaidi ya dola bilioni 25 kwa misaada nje ya nchi toka aingie madarakani mwaka 1999. Kiwango hicho ni sawa na sh bilioni 3.6 kwa mwaka wakati Marekani imetumia sh bilioni 2 tu.
Kutoa misaada nje ya Venezuela kunaenda sambamba na uboreshaji wa huduma muhimu za jamii nyumbani. Kwa mfano madaktari wapatao 15,000 kutoka Cuba hutoa huduma na yeye hukilipa kisiwa hicho kwa kukiuzia mafuta kwa bei ya chini.
Ili kusaidia nchi masikini katika visiwa vya Caribbean, Venezuela huviuzia visiwa hivyo mafuta kwa bei pungufu kwa asilimia 13. Msisitizo wake wa kwamba rasilimali za nchi lazima kwanza ziwanufaishe wenye nchi zimefanya aonekane ni mpiganaji halisi wa maslahi ya wanyonge.
Aidha, Chavez atajenga bomba la gesi la urefu wa kilometa 8,000 kwenda Rio De la Plata, Argentina kupitia nchini Brazil. Pia amenunua hisa kubwa katika vituo vya gesi vya nchi jirani ya Uruguay, huku pia akifikiria kununua matenki makubwa ya mafuta huko Brazil kwa gharama ya dola bilioni 3.
Ushawishi wa Chavez unaendelea kusambaa katika si tu Amerika Kusini bali mpaka Urusi, China na Iran ambako amejenga uhusiano mkubwa na serikali za nchi hizo. Katika ziara yake ya mwezi huu huko Urusi, Venezuela ilisaini mikataba mikubwa ya kuuziana ndege za kivita na zana nyinginezo za kijeshi zitakazogharimu mabilioni ya dola ambayo ni karibia nusu ya mapato ya Urusi kwa mauzo ya bidhaa za nje.
Wakubwa wakiongozwa na Marekani wamekuwa wakimpigia Chavez kelele kwamba anatapanya rasilimali za Wavenezuela ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Wanadai kuwa mlolongo wa miradi yote hiyo ni kwa nia ya kujipatia umaarufu na si kwa manufaa ya wananchi.
Eti wana uchungu na Wavenezuela! Hizo ni propaganda na ndio maana ili kukabiliana na changamoto hiyo, Chavez alianzisha utaratibu wa kuongea live na wananchi kila Jumapili kupitia kipindi maarufu cha ‘Hallo Mr. President’. Kipindi hicho cha muda wa saa sita kimelenga kukabiliana na propaganda za vituo vya CNN na Univision. Kipindi hicho hujumuisha ziara za kikazi za wiki nzima za rais huyo ambapo wananchi huruhusiwa kuuliza maswali live kwa njia ya simu.
Ndio maana nasema kubadilika kifikra ni nguzo namba moja kuelekea kujenga maisha bora kwa kila Mtanzania. Wananchi hawana budi kujihabarisha, kujua kipi kinachoendelea, ni kwa vipi watatoa mchango wao kimawazo na kivitendo.
Hili limedhihirika kwenye miradi ya TASAF, imefanikiwa kwa sababu mbali ya kuhabarishwa wananchi wengi baada ya kuwaona wenzao wananufaika na miradi hiyo, walipenda kujihabarisha, wakabadilika kifikra na kuona kwamba ili kujiletea maendeleo ni lazima washiriki katika miradi hiyo.
Nina hakika tukibadilika kifikra na kimtazamo, tutafaidi kikamilifu matunda ya awamu ya nne na kujenga Tanzania yenye maisha bora kwa kila mmoja wetu, kinyume chake hata rais agawe elfu hamsini kila asubuhi, tutabaki tukilalama na kusema ooh serikali, ooh serikali.
Cosato Chumi ni mwandishi wa zamani katika magazeti ya The Guardian na Uhuru/Mzalendo. Anapatikana kwa simu; 0784 272 411 au barua pepe; mmakangura@yahoo.com