Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Ubungo na sifa za kinafiki
http://www.habaritanzania.com/articles/754/1/Ubungo-na-sifa-za-kinafiki
By Manyerere Jackton
Published on 08/18/2006
 
KWA muda sasa, uongozi wa Kituo cha Mabasi Ubungo, umekuwa ukijitahidi kukipamba kituo hicho kwa namna inayoshangaza.

Manyerere Jackton

KWA muda sasa, uongozi wa Kituo cha Mabasi Ubungo, umekuwa ukijitahidi kukipamba kituo hicho kwa namna inayoshangaza.

Kuna makala nyingi zimeandikwa kuhusu ‘ubora’ wa kituo hicho; jambo ambalo mimi kama mdau, nimeona nitakuwa na dhambi nisipozipinga hadharani.

Tumeelezwa kwamba kwa kila siku, Ubungo kunakusanywa sh zaidi ya milioni 2 kutokana na viingilio vya wasindikizaji na magari yanayoingia na kutoka kituoni hapo.

Kutokana na ufinyu wa safu hii, siwezi kueleza tambo zote zilizotolewa na viongozi wa kituo hicho. Lakini kwa anayeijua Ubungo, kisha akazisoma tambo za viongozi wa kituo hicho, anaweza kuhoji umakini wa watu hawa.

Niliposoma tambo hizo, sikuambulia kingine, zaidi ya kujisemea moyoni kuwa wananchi sasa tunaonekana mbumbumbu. Na kwa kweli ndiyo maana hata kule tunakokula ‘mapanki’, tunaambiwa hatuli, nasi tunaandamana kuunga mkono!

Itoshe tu kusema kwamba kinachopigiwa debe na viongozi wa Ubungo ni uzandiki na kutaka kuwafanya Watanzania wote kuwa ni wavivu wa kuona na kutambua.

Kituo cha Mabasi Ubungo hakina chembe ya sifa ya kuitwa kituo cha kimataifa. Hakina sifa hiyo. Sifa hizi za kulazimisha zinaweza kukubaliwa na Mtanzania ambaye hajapata fursa ya kusafiri na kuona vituo vya kimataifa jinsi vilivyo.

Kwa mtu ambaye ni mara yake ya kwanza kukutana na kituo cha kimataifa, atakubaliana na uongozi wa Ubungo kuwa kituo hicho kweli ni cha kimataifa.

Lakini anayevijua vituo vyenye hadhi hiyo, hawezi kukubaliana na propaganda hizi za kututaka tuamini kuwa Ubungo ni kituo cha mabasi cha kimataifa.

Nje tu ya kituo hiki kunaashiria kuwa hakuna kituo cha kimataifa. Kituo gani cha kimataifa ambacho kimejaa wapiga debe na matapeli wasumbufu kama Ubungo? Cha kimataifa hapo ni nini? Ni hizo vurugu, wizi na uporaji wa abiria? Je, ni hao wahuni walio tayari kuwapora abiria simu zao? Ni hao wanaowabana abiria na hata wengine wanapoteza watoto na mizogo yao?

Milango ya kuingia na kutoka abiria ndani ya kituo ni aibu na kero ya hali ya juu. Abiria hawezi kupita akiwa ameshika begi au sanduku. Kuna vyuma ambavyo hata benki huwezi kuvikuta!

Ndani ya kituo ni aibu isiyo kifani. Dunia ya leo mambo yamebadilika. Hata masanduku na mabegi, si ya kuwekwa vichwani au mabegani tena. Abiria anatakiwa akokote mzigo wake.

Ndani ya Ubungo kumejaa mashimo. Ni kero tupu. Abiria akithubutu kukokota begi au sanduku, maana yake ni kwamba ametaka kuliharibu. Mashimo haya ndiyo ya kuringia kwamba kituo hicho ni cha kimataifa?

Ukishaingia Ubungo, hakuna wa kumuuliza. Mungu bariki, umpate polisi muungwana kama yule aliyepambana na majambazi na kuyashinda.

Asilimia kubwa ya wanaoulizwa ni matapeli. Wakishaona sura fulani ni ya mgeni, humwelekeza sehemu mbaya, na huko abiria ataporwa na kufanyiwa uhuni wa kila aina. Haya ndiyo uongozi wa Ubungo unataka tuamini kuwa yamekifanya kituo hicho kiwe na hadhi ya kimataifa!

Hakuna muda wa basi kuondoka. Abiria wataambiwa kuwa muda wa kuondoka ni saa tatu, matokeo yake wataondoka saa sita mchana. Hakuna kuombwa radhi, na wahudumu, kwenye kamusi yao hakuna neno ‘samahani’. Watu gani wa kimataifa wanakuwa wababaishaji kiasi hiki?

Kituo cha kimataifa, abiria akishaingia, mambo huwa ya kimataifa. Abiria ndani ya Ubungo wanalazimika kulipia huduma ya haja ndogo na haja kubwa; tena bila aibu, wameandika bei ya kila aina ya haja!

Wale waliotembea sehemu kadhaa duniani, wameona wapi abiria anadaiwa fedha za kujisaidia ndani ya kituo kama hiki? Uwanja wa ndege wa wapi ambako abiria hudaiwa alipie huduma za choo akitaka kujisaidia? Wapi huko? Hata Somalia ambako hakuna serikali, haya mambo hayapo!

Tunadanganywa kwamba Ubungo ni Kituo cha Kimataifa ilhali wakati wa mvua, abiria wataloa kuanzia nje ya kituo hadi wanapoingia ndani ya mabasi.

Kumewekwa mabanda ya kizamani -magereji ya mabasi ya UDA ambayo yamegeuzwa kuwa sehemu ya abiria kupumzika! Wanapotoka nje, mvua na jua vyote ni vyao hadi wanapoingia ndani ya mabasi.

Uongozi wa Kituo cha Mabasi Ubungo, unatumia udhaifu huu kuwahadaa Watanzania kwamba kituo hiki ni cha kimataifa!

Ndani ya kituo kuna ulanguzi wa tiketi na wizi wa kustaajabisha. Kila leo abiria na wasio abiria wanalia kutokana na kuibiwa au kuporwa mizigo, fedha na mali zao nyingine.

Kuna polisi na mgambo ambao ni vigumu sana kutoamini kuwa lao ni moja na majizi na vibaka waliomo kituoni humo.

Wauza mikate wamejaa kila kona. Abiria wanachafuliwa suti na mavazi yao nadhifu kutokana na kulazimishwa kununua mikate! Kituo gani cha kimataifa ambacho abiria anapambana na adha za aina hii?

Abiria wengine hushindwa kusafiri wakiwa na mama, dada, baba, shangazi watoto au wakwe zao.

Wanashindwa kwa sababu Ubungo kuna wahuni wengi ambao wakishaona maungo ya mwanamke, huanza kupiga mbinja na kutoa maneno ya kihuni.

Je, huo ndiyo mfumo ndani ya vituo vya mabasi vya kimataifa?

Mamilioni yanakusanywa kila siku Ubungo. Yanakwenda wapi? Je, si kweli kwamba yanakwenda katika matumbo ya wanaotetea uchafu huu wa Ubungo? Je, si kweli kwamba huu ni mradi wa watu wanaotaka kuupumbaza umma ili uamini kuwa ‘ubinafsishaji’ ni jambo la maana?

Fedha zinazotokana na mabango ya kampuni za simu na kampuni nyingine, zinakwenda wapi? Kwa nini zisitumike kuboresha kituo hiki?

Ili Ubungo iwe kweli kituo cha mabasi cha kimataifa, lazima mambo mengi yarekebishwe.

Hatuwezi kukipa hadhi hiyo kwa sababu tu kinapokea magari kutoka Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Kenya, Uganda na kadhalika.

Kutumia mabasi ya kigeni Ubungo kama kigezo cha kupafanya pawe kituo cha kimataifa ni upuuzi.

Hii ni kama kuifanya miji yetu kuwa na hadhi ya jiji kwa kutumia kigezo cha wingi wa watu, bila kujali miundombinu kama barabara na huduma nyingine.

Nimeandika haya kwa sababu kadhaa muhimu. Mosi, Watanzania tusifikishwe mahali tukaufanya uongo ukawa ukweli. Uongo mwingine haufai, kwa sababu baadhi ya mambo tunayoongopewa, tunayaona na kuyalinganisha na ukweli tuliokwishauona katika mataifa mengine.

Pili, Watanzania wasifanywe kuwa ni wavivu wa kuambiwa na kujadili wanachoambiwa. Sifa wanazojipa watu wa Ubungo, tukiwaacha waendelee kutuhadaa, watatuona sote tu mbumbumbu. Watatuona kama watu ambao hatujawahi kuvuka mipaka ya nchi yetu na kuona yaliyo kwa wenzetu.

Tatu, matumizi ya fedha za umma yanapaswa yatolewe maelezo sahihi, badala ya kujiandalia sifa kwa lengo la kutaka kuficha ukweli.

Tunaamini Ubungo kunakusanywa fedha nyingi ambazo kama zikitumiwa vema, kweli sehemu hiyo inaweza kuwa na hadhi ya kimataifa.

Stahili ya Ubungo ni kuendelea kuitwa kituo cha mabasi yaendayo na yatokayo mikoani; na si kupabatiza jina la kituo cha kimataifa.

Nimeona niseme haya kwa sababu miongoni mwa mambo ninayochukia, ni yale ya watu kadhaa kuwafanya wengine ni wajinga na walio tayari kudanganywa hata kwa mambo yanayoonekana wazi.

Kituo cha Ubungo ni moja ya mitambo inayozalisha kero nyingi kwa wananchi. Hakina sifa zinazotamkwa na viongozi wake. Anayetaka kuibiwa, kuporwa, kutukanwa, kusukumwa, kuadhiriwa, na kupata aina ya adha ambazo hajawahi kupambana nazo kwenye usafiri, na aende leo Ubungo.

E-mail: manyerere@hotmail.com
0713 33 54 69