MWANZO wa ngoma ni lele. Mdharau mwiba, mguu huota tende. Panapofuka moshi, pana moto. Dalili ya mvua, ni mawingu.
Mgogoro wa mapigano ya mara kwa mara kati ya koo wilayani Tarime, unadhihirisha maneno hayo hapo juu.
Kwa miaka mingi, mapigano ya kikabila wilayani Tarime yanaelekea kuwa jambo la kawaida.
Viongozi wa dola wamejitahidi kuingilia kati kutuliza mapigano hayo, lakini hakujapatikana suluhu ya kudumu.
Ndiyo maana tunasema mgogoro huu ingawa unaonekana kuwa wa kawaida, una dalili zote za kuchafua taswira nzuri ya nchi yetu.
Tanzania inaelezwa kama moja ya nchi zenye amani katika Afrika. Hali hiyo imeipatia heshima kubwa nchi yetu.
Wananchi katika mataifa yanayopigana wameitumia Tanzania kama pepo ya kuokoa uhai wao. Tuna wakimbizi wengi mno kutoka Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Somalia na kwingineko.
Nchi ambayo imejipambanua kama kitovu cha amani, utulivu, umoja na mshikamano, ni aibu kushuhudia leo watu wake wakiumizana katika mapigano ya kipuuzi kama haya ya Tarime.
Hatuoni sababu ya kuwafanya wananchi hawa wa Tarime washindwe kuelewana ilhali kuna viongozi wanaoweza kuwatumia kumaliza tofauti zao.
Wakati umefika kwa viongozi wa serikali kushirikiana na wananchi wa Tarime ili kumaliza tofauti zinazosababisha mapigano ya mara kwa mara.
Kama wapo wakorofi wanaopalilia hali hiyo, mkono wa sheria usiwapite mbali. Wanaswe, washughulikiwe kisheria.
Kama chanzo cha ugomvi ni uhaba wa ardhi, serikali itafute njia nyingine sahihi za kumaliza tatizo hilo.
Busara iliyotumiwa na uongozi wa Awamu ya Kwanza, ya kuwahamasisha wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuhamia mikoa mingine yenye ardhi ya kutosha, sasa itumike pia Tarime.
Tanzania ni moja. Wananchi wake ni wamoja. Kuna ardhi kubwa mno, na nzuri kabisa ambayo haijapata watumiaji.
Hatuoni kama kuna sababu kwa wakazi wa Tarime kuendelea kuuana kwa sababu ya ardhi, ilhali kuna mapori yanayosubiri watumiaji.
Wananchi wa Tarime pia wawe na subira. Wasidhani kuwa ubabe na vita ndiyo njia muafaka ya kumaliza matatizo.
Kuna mifano mingi hai inayothibitisha kuwa vita si suluhu ya matatizo yote. Mazungumzo ya pamoja, vikao na moyo wa subira, ni mambo muhimu katika ujenzi wa jamii yenye amani.
Tunalaani mapigano haya ya Tarime, na yanayofanywa pia na wakazi wa nchi jirani ndani ya wilaya hiyo.
Aibu hii isiruhusiwe iendelee kulikumba taifa letu ambalo wapenda amani wengi wana sali kila uchao ili liendelee kuwa kitovu cha amani, upendo, utulivu na mshikamano.