WADAU wengi wa mapambano dhidi ya UKIMWI wamekuwa wakipanga mipango yao kiholela na bila kuwa na viashiria vya kuaminika, kwa kuwa hawana taarifa sahihi za maambukizi.
Hayo yameelezwa juzi mjini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Afnet, Sara Mwanga kwenye warsha ya mtazamo mpya kuhusu janga la UKIMWI Tanzania.
Alisema kuwa kufanyika kwa utafiti wa HIV/AIDS Indicators Survey (HIS), uliofanyika mwaka 2003/2004, umeleta sura mpya na kuondoa utata uliokukwapo ambapo sasa kuna takwimu sahihi na za uhakika katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Alisema kuwa kwa kutambua tatizo hilo USAID ilitoa msaada kwa mradi wa Policy Project na kuandaa kitabu kinachoelezea takwimu za UKIMWI kwa lugha nyepesi na kwamba Afnet ilishiriki katika maandalizi ya kitabu hicho kiitwacho ‘Mtazamo mpya kuhusu janga la UKIMWI Tanzania’ ambacho kilichapwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na vitabu hivyo kusambazwa katika wilaya zote nchini, lakini watu hawavisomi ipasavyo na kwamba, wadau wengi hawana habari juu ya takwimu hizo na wanaendelea kuandika miradi na programu kwa kutumia takwimu zisizo sahihi na ambazo hazijathibitishwa.
Mratibu wa Afnet Mkoa wa Dodoma, Andrew Karama, alisema warsha hiyo ni miongoni mwa warsha zinazoendeshwa na shirika hilo pamoja na mtandao wa wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa kushirikiana na Health Policy Initiative chini ya ufadhili wa USAID, ili kujenga ufahamu zaidi juu ya takwimu zilizo katika utafiti wa HIS