BARAZA la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo ambao walikutana Chuo Kikuu Kishiriki cha Makumira, Arusha hivi karibuni, wameamua kwa kauli moja kupinga hatua ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Askofu Dk. Samson Mushemba kwa niaba ya maaskofu wote wa KKKT, kanisa hilo haliko tayari kuona mahakama hiyo inaanzishwa hapa nchini, kwa madai ya kuwa ni kwenda kinyume cha katiba inayoiongoza serikali.
“Kwa kuzingatia mawazo haya, sisi maaskofu wa KKKT na Halmashauri ya Kanisa zima, tunawiwa na dhamiri zetu kuangalia kuwa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ni jambo la hatari kwa amani, umoja na mshikamano wa taifa letu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Baraza hilo limesema kuwa uanzishwaji wa mahakama hiyo utadhoofisha katiba ya nchi inayobainisha wazi kutenganisha mambo ya dini na serikali, kwa sababu serikali yetu haina dini.
Taarifa hiyo ilisema kuwa baraza hilo linasihi Bunge lisikubali kamwe kuruhusu uanzishwaji wa mahakama hiyo na kuongeza kuwa Tanzania yenye amani ni tunda la dini, itikadi, makabila, rangi na jinsia zote.