JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limewakamata watuhumiwa wawili wa utapeli wa kuwatafutia watu viza katika balozi mbalimbali nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, alisema: “Sisi tumechunguza ili kugundua kundi la watu wanaojihusisha na kitendo cha kujipatia fedha kwa udanganyifu wa kuwatafutia viza watu katika balozi mbalimbali.”
Alisema Agosti 11, mwaka huu, walimkamata John Bitebo (45), mkazi wa Magomeni Mwembechai, akiwa na ndani ya gari lenye namba T 907, aina ya Toyota Mark II.
Alisema baada ya kufanya upekuzi kwenye gari hilo, walimkuta akiwa na viza tano za watu mbalimbali Watanzania ambazo alishindwa kuzitolea maelezo.
Baadaye mtuhumiwa huyo alimtaja anayeshirikiana naye, aliyefahamika kwa jina la Ally Salum (46), mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam.
Alisema watu hao juzi walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu wakati upepelezi ukiendelea. Kesi hiyo itatajwa Agosti 30, mwaka huu.
Agosti 3, mwaka huu gazeti hili lilitagaza kupotea kwa viza mbili za wafanyakazi wa New Life Foundation zilizotolewa Dar es Salaam.