WATU 17 wanaoumwa kipindupindu wamelazwa katika Manispaa ya Kinondoni na Temeke, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Deo Mtasiwa, ilisema kuwa wagonjwa wapya tisa walilazwa jana katika hospitali mbalimbali mkoani humo.
Wagonjwa wanne walitoka katika Manispaa ya Kinondoni, na wengine walitoka katika Manispaa ya Temeke. Manispaa ya Ilala haikuwa na mgonjwa.
Aliwataka wananchi wachemshe maji ya kunywa, ya kuoshea vyombo, na ya kutengenezea juisi ili kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo.
Alipiga marufuku kutiririsha maji machafu mitaani, kuuza vyakula kiholela na kutupa taka hovyo.
Alisema wote watakaokiuka kanuni za afya, watachukuliwa hatua za kisheria.
Kipindupindu ni ugonjwa unaoenezwa na nzi, chanzo kikuu kikiwa ni uchafu na kwa kutozingatia kanuni za afya.
Dalili za mgonjwa wa kipindupindu ni kuhara kinyesi cha majimaji chenye rangi inayofanana na ya maji yanayotokana na mchele uliooshwa, kutapika na kupoteza nguvu.
Wataalamu wanashauri kuwa pindi dalili hizo zinapoonekana, ni vema mgonjwa akapewa huduma ya kwanza.
Inashauriwa mtu wa aina hiyo apewe maji mengi yaliyotiwa chumvi au sukari, kisha apelekwe haraka katika zahanati, kituo cha afya au hospitali iliyo karibu.
Ugonjwa wa kipindupindu ni hatari, na huambukiza haraka na kwa njia rahisi. Inashauriwa mgonjwa atengewe eneo maalumu ili asiwaambukize watu wengine