Na Angela Sebastian, Bukoba
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi amezishauri taasisi na mashirika mbalimbali kushirikiana na kampuni za simu za mkononi kutumia mnara moja kufanikisha shughuli zao za kimaendeleo.
Nchimbi alitoa ushauri huo juzi wakati alipokuwa akikagua minara ya TVT na Star TV ambayo inaendelea kujengwa katika maeneo ya Kibeta na Kiziru nje kidogo mwa mji wa Bukoba.
Alitoa ushauri huo baada ya kupewa taarifa na mwakilishi wa Star TV mkoani Kagera Ayubu Mpanja kuwa kampuni ya Sahara Communication imeungana na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kwa kutumia mnara moja kurusha matangazo yao.
Naibu Waziri alisema ushirikiano huu utawasaidia watu mbalimbali kupunguza gharama zisizo za lazima maana kufunga mtambo moja ni zaidi ya sh. milioni 300.
Alisema mitambo hiyo ya televisheni inayoendelea kufungwa itasaidia wananchi wa mkoa wa Kagera kupata habari mbalimbali kupitia televisheni zao bila malipo kama ilivyo hivi sasa ambapo wananchi wa mkoa huu hulazimika kulipa huduma ya kuunganishiwa stesheni za televisheni kupitia waya ambapo hulipia sh. 10,000 kwa mwezi.
Naye Meneja wakala wa majengo mkoani Kagera Kanakoko Donatus alimweleza Naibu Waziri kuwa ujenzi wa mnara wa TVT ulitarajia kuanza Mei mwaka jana lakini kutokana na matatizo ya kukosa mkandarasi ulishindwa kuanza.
Ujenzi huo ulianza Agosti mwaka jana ambapo hivi sasa kazi iliyobakia ni kufunga antena na umeme na kuwa kufikia mwezi ujao matangazo ya mwanzo ya majaribio yataanza kurushwa mkoa mzima wa Kagera.