Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tohara ya wanaume yawagawa wadau wa UKIMWI
Tohara ya wanaume yawagawa wadau wa UKIMWI
By Habari Tanzania | Published  08/18/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Ansbert Ngurumo, Toronto

WADAU wa UKIMWI wameshindwa kukubaliana kama kutahiri wanaume ni njia ya kupunguza maambukizo ya UKIMWI katika nchi zinazoendelea.

Wakijadili mada hiyo katika Mkutano wa 16 wa Kimataifa kuhusu UKIMWI, unaofanyika Toronto, Kanada, wiki hii, watafiti wamesema utafiti wa awali uliofanyika Afrika Kusini ulionyesha kuwa maambukizo yalikuwa madogo kwa wanaume waliotahiriwa kuliko wasiotahiriwa.

Lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) yamegoma kutambua dhana ya kinga katika tohara hiyo hadi yatakapopatikana matokeo ya tafiti nyingine mbili zinazofanyika sasa Uganda na Kenya.

Baadhi ya wanasayansi wamesema tohara si ufumbuzi, na kwamba iwapo wanaume wataaminishwa kuwa kutahiri kunawakinga na virusi, ipo hatari wanaume hao wakaacha kutumia kondomu, jambo ambalo litahatarisha maisha yao.

Utafiti wa Afrika Kusini ulichapishwa na jarida la PLoS katika toleo la Novemba 2005, na kujadiliwa mwaka jana katika Mkutano wa UKIMWI uliofanyika Brazil, ulihusisha vijana zaidi ya 3,000 ambao hawajaambukizwa virusi, wenye umri wa miaka 18-24 katika eneo la Soweto.

Nusu ya vijana hao walitahiriwa na wengine hawakutahiriwa. Katika kila 10 wasiotahiriwa walikutwa wameathirika na virusi baadaye, watatu waliotahiriwa ndio waliambukizwa.

Baada ya hapo watafiti walitoa tamko kwamba tohara ya wanaume inapunguza uwezekano wa maambukizi.

Kwa mujibu wa watafiti, kama tohara ya wanaume itapigiwa debe ikaongezeka walau kwa asilimia 10 katika miaka mitano, watu wapatao 32,000 wanaweza kuokolewa katika janga la UKIMWI.

Wanasema pia kwamba hamasa hiyo ikiongezeka kwa asilimia 20 katika miaka mitano, wanaume wapatao 52,000 wataokolewa.

Nchini Kenya, utafiti unahusisha wanaume 3,000 ambao hawajatahiriwa, wasio na virusi vya UKIMWI, ambao nusu yao wametahiriwa mahususi kwa ajili ya utafiti.

Ifikapo Septemba 2007, watafiti watahesabu idadi ya wanaume katika makundi ya waliotahiriwa na wasiotahiriwa watakaokuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI.

Utafiti wa Uganda unawahusisha wanaume 5,000, na unaongozwa na watafiti katika vyuo vikuu vya Columbia na Johns Hopkins, Marekani. Unatarajiwa kukamilika Julai 2007.

Washiriki wengi walipendekeza tohara itambuliwe rasmi kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizo, lakini WHO na UNAIDS zimesema haziwezi kuitambua hadi tafiti za Uganda na Kenya zikamilike.

Balozi wa Umoja wa Mataifa wa UKIMWI kwa ajili ya Afrika, Stephen Lewis, alisema anaamini mashirika haya yatabadili msimamo wake baada ya ‘kufanikiwa kwa tafiti hizo.’

“Baada ya matokeo ya utafiti wa Afrika Kusini, hatuna sababu ya kusubiri kutoa uamuzi hata kwa saa 24. Msimamo wetu ni kwamba inavyoelekea ushahidi wa utafiti huo hauko mbali,” alisema.

Naye mkuu wa kitengo cha UKIMWI katika WHO, Kevin De Cock, alisema kitaalamu si jambo la busara, wala haikubaliki kitaaluma kuchukua ushahidi wa jaribio la kwanza na kuufanya uamuzi.

“Nadhani tutatoa mwongozo iwapo tafiti hizo mbili nazo zitaonyesha kwamba kutahiri kunasaidia,” alisema.

Hata hivyo, mwanasosholojia kutoka Australia, Gary Dowsett, alisema mkazo ungewekwa katika kutathmini maana na mchango wa kitamaduni wa tohara ya wanaume, kuliko kung’ang’ania hoja ya utafiti kwa ajili ya UKIMWI.

“Wanasosholojia hawakuhusishwa kabisa katika utafiti huu kwa sababu watafiti wanajua tutawachanganya na kuwaharibia,” alisema.

Lakini Robert C. Bailey, anayehusika na utafiti wa Kenya, alisema anapingana na kauli ya Dowsett. Bailey ni mtafiti katika Chuo Kikuu cha Illinois, Chicago.

Alisema timu yake ya utafiti inawahusisha wataalamu wa sayansi ya jamii ambao wamekuwa wakifanya mahojiano na Wakenya ili kujua wana imani gani kuhusu tohara kabla ya kuwashirikisha.

Hoja ya watafiti wanaotetea tohara hiyo ni kwamba ngozi ya juu katika utupu wa mwanaume uliotahiriwa ni ngumu kuliko ya utupu usiotahiriwa. Wanadai kwamba virusi havipenyi kirahisi katika ngozi ngumu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.