MWANDISHI wa siku nyingi aliyefanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari nchini, Sydney Kwiyamba, amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa juzi kwa vyombo vya habari na Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam, ilisema kuwa Kwiyamba alifariki dunia Agosti 2, mwaka huu saa 7 mchana baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Taarifa ilisema kuwa alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi ambao uliambatana na kupooza kwa mwili. Alianza kuugua Oktoba, mwaka jana.
Kwiyamba alizaliwa Julai 22, 1950 katika Kijiji cha Usoke, mkoani Tabora, akiwa ni mtoto wa pili wa Samuel Mwela na Nelea Almasi.
Alianza shule mwaka 1958 katika Shule ya Msingi Kaloka, Tabora, baadaye katika Shule ya Kati Chabutwa. Alihitimu mwaka 1965.
Mwaka 1966 hadi 1971 alijiunga katika Shule ya Sekondari Kazima, na baadaye Shule ya Sekondari Mkwawa ambako alihitimu kidato cha sita.
Mwaka 1974 hadi 1977 alijunga na Chuo Kikuu cha Beograd kilichoko Yugoslavia kuchukua mafunzo ya uandishi wa habari.
Pia alichukua mafunzo hayo hapa nchini na kupata shahada.
Kwiyamba amewahi kuwa mwandishi wa habari katika vyombo mbalimbali, mwanachama wa vyama mbalimbali, na pia aliwahi kuwa Mwandishi Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA).
Atakumbukwa kwa kuwa mstari wa mbele katika uandishi wa habari zilizohusu mazingira.
Mola ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina