RAIS Jakaya Kikwete amemwelezea Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kama kiongozi wa aina yake na kuahidi kufuata nyayo zake ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kushiriki kwa hali na mali katika kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), inastawi.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati alipokaribishwa na kupewa nafasi ya kuhutubia mkutano wa siku mbili wa kawaida wa nchi wanachama wa SADC ulioanza jana mjini Maseru.
Huu ni mkutano wa kwanza kwa Kikwete kuhudhuria akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ninawaletea salamu kutoka kwa Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kiongozi wa aina yake katika nchi yetu na aliyeiwezesha Tanzania kutoa mchango wake katika Afrika. Nitafuata nyayo zake,” alisema.
Alisema ushiriki na mchango wa Tanzania katika jumuiya hiyo, ambayo kuanzishwa kwake kuliasisiwa na viongozi kadhaa akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hautakoma chini ya uongozi wake.
Aliwahikikisha viongozi wenzake kutoka nchi 14 wanachama wa SADC kwamba hakutakuwa na upungufu wowote kutoka kwa wananchi wa Tanzania katika kufanya kazi na wananchi wenzao wa kusini mwa Afrika.
“Nikiwa kiongozi mpya katika klabu ya Afrika na ambaye nina miezi saba tu madarakani, ninaomba ushirikiano kutoka kwenu, wengi wenu mlikuja kushuhudia kuapishwa kwangu, wengi wenu mlinitumia salamu za pongezi, na nilipokuja kujitambulisha katika nchi zenu kwamba mimi sasa ndiye ‘Mkapa’ mpya wa Tanzania, mlinipokea kwa mapenzi makubwa,” alisema.
Alisema kuwa wananchi wa Tanzania wanafurahia mafanikio yanayoendelea kujitokeza katika jumuiya hiyo, mafanikio yanayolenga kuiwezesha kanda hii kuwa yenye amani na utulivu.
Rais alisema kuwa inaridhisha kuona kuwa Kanda ya Afrika inaendelea kuwa yenye usalama, utulivu na ulinzi, ikielekea katika muungano wa kiuchumi na kanda ambayo uchaguzi wa kidemokrasia unaendelea kuota mizizi na kuheshimika huku viongozi wakiachiana madaraka kwa amani.
Alisema hatua ya kufanyika kwa amani na utulivu uchanguzi wa kihistoria katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kielelezo kingine cha ukuaji na ustawi wa demokrasia katika nchi za Afrika.
“Ninawapongeza wananchi wa DRC kwa kazi nzuri waliyoifanya, wameijengea heshima kanda yetu, ni matumaini yangu kuwa vyama vyote vya siasa vitayapokea matokeo kwa moyo mkunjufu,” alisema.
Akielezea kuhusu uenyekiti wa Taasisi ya Utatu ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Afrika ambayo Tanzania inachukua uenyekti wake, Rais Kikwete alisema taasisi hiyo ni muhimu kwani ndiyo mhimili wa amani, utulivu na usalama katika Afrika.
“Ningependa kuwahakikishia kuwa tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kukidhi matarajio yenu,” alisema.
Rais alisema anatambua vema ugumu wa hapa na pale katika kuiendesha taasisi hiyo, hata hivyo aliahidi kutumia uwezo wake wote kukabiliana na changamoto hizo.
Katika mkutano huu wa 26 wa Afrika, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Benjamin William Mkapa, Dar es Salaam, Herry Mapesi (18), aliibuka mshindi wa kwanza katika uandishi wa insha na kutunukiwa dola 1,500 za Marekani na cheti.
Mada ya insha ya mwaka huu ambayo huwashirikisha wanafunzi wa sekondari ilihusu chakula na lishe.
Mapesi alikabidhiwa zawadi yake na kuitwa jukwaani kusoma sehemu ya insha yake. Insha ambayo maudhui yake yaliwakuna viongozi wakuu wa nchi na serikali na wajumbe wa mkutano huu.
Baada ya kusoma insha yake, Rais Kikwete alimwita mwanafunzi huyo na kukumbatiana naye kwa furaha kitendo kilichoshangiliwa na wajumbe wa mkutano.
Moja ya ajenda inayoelekea kutawala mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika ni ile inayohusu kwa baadhi ya nchi kuwa wanachama wa zaidi ya kanda moja za ushirikiano.
Katika hatua nyingine, baadhi ya viongozi waliozungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo walishauri kwamba ifike mahali sasa nchi za Afrika zijenge mazingira yatakayoziwezesha nchi wanachama kufanya biashara miongoni mwao na vile vile kati yao na nchi nyingine za Afrika.
Walisema kuwa ni kwa kufanya hivyo ndipo nchi za Afrika zitaachana na utegemezi.
Aidha, viongozi hao walihimizana kuchangia miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa miundombinu na hivyo kuachana na utegemezi wa wahisani ambao huchangia asilimia 61 ya miradi ya Afrika.