Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wapinzani waibuka
Wapinzani waibuka
By Habari Tanzania | Published  08/18/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Charles Mullinda na Christina Gregory

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye wapinzani sasa wameibuka nchini na kufanya maandamano makubwa, huku wakiishambulia serikali vilivyo.

Viongozi watatu wa vyama vya upinzani vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, baada ya maandamano hayo, nao sasa wametangaza kuanzisha umoja.

Freeman Mbowe wa CHADEMA, Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF na Augustine Mrema wa TLP, walitangaza adhima yao jana wakati wakihutubia maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani waliojitokeza kuwapokea wabunge wa kambi ya upinzani katika viwanja vya Jangwani.

Wa kwanza kueleza adhima hiyo alikuwa Freeman Mbowe, ambaye aliwataka viongozi wenzake pamoja na wanamageuzi kujifunza walipokosea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Upinzani ni mateso, kudhalilishwa, kutukanwa na kila aina ya kitu kibaya, kwa nini tunajitenga? tunagombania nini? Tusipounganisha nguvu zetu tunajidanganya.

“CCM ni weupe sana. Si imara, kama wangekuwa imara wasingetumia majeshi, wakuu wa wilaya na mali za serikali katika Uchaguzi Mkuu. Cha msingi tusisubiri mpaka 2008 ndipo tuanze mikakati ya kuunganisha nguvu zetu, tuanze sasa,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema yeye hana tatizo kama yatakuwapo makubaliano ya kuanzishwa kwa umoja wa vyama vya upinzani kwa ajili ya kupambana na CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Kwa upande wake Prof. Lipumba, alisema anakubaliana na Mbowe kuanzisha umoja wa vyama vya upinzani mapema ili uwepo muda wa kutosha kujipanga upya, kauli ambayo iliungwa mkono na Mrema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, alisema vyama vya upinzani vinapinga wote unaobagua wapinzani na kukiuka katiba.

Slaa alisema kuwa Katiba inayotumika ni mbovu na inabidi kurekebishwa kuleta usawa kwa wananchi wanyonge ambao haki zao zinatumiwa bila wao kujua.

Alisema kwa kutumia katiba hiyo mbovu, mawaziri wamekuwa wakilidanganya Bunge na hakuna kitu chochote kinachoendelea kwa upande wa Rais, zaidi ya kusema anafuatilia, na matokeo yake hakuna linalofanyika.

“Rais anaonekana anawabeba mawaziri wake. Mbona wanapopotosha Bunge hafanyi kitu chochote wakati sheria inasema washtakiwe?” alihoji Slaa.

“Tupige kelele Katiba hii ibadilishwe, kwani hatuwezi kuacha mali zetu mikononi mwa watu,” alisema Slaa na kushangiliwa. Alisema wataendelea kutoa maoni yao bungeni kwa kuwatetea wananchi mpaka haki itakapopatikana.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alimtaka Rais Kikwete atoe ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar. Alisema Rais Kikwete aliomba muda wa kushughulikia suala hilo, lakini mpaka sasa bado hajalitatua.

“Alitueleza akiwa kiongozi atashughulikia suala hili, lakini mpaka sasa sijui kitu gani kinamfanya ashindwe kulitatua tatizo hili,” alisema.

Alisema wao kama vyama vya upinzani hawatarajii kumuona akiondoka madarakani akiwa na damu mikononi mwake.

Alionya tabia ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza vitu na kuviacha bila kuvifanyia kazi huku wananchi wakiendelea kuteseka katika alichosema kuwa ni ahadi zisizotekelezeka. Wamewaeleza wananchi kuletewa maendeleo, ni haki yao, hivyo hawana budi kusimamia na kuhakikisha Katiba inabadilishwa.

Wapinzani jana waliandamana kutoka Ubungo hadi viwanja vya Jangwani, kwa maelezo kuwa wanawapongeza wabunge wa upinzani kwa michango waliyoitoa bungeni.

Hadi sasa wameamua kujipanga kwa ajili ya kuweka upinzani wenye maana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, na hasa kwa kutilia maanani tamko la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kuwa sheria ya kuruhusu vyama vya siasa kuungana inakuja.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.