WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amemmwagia sifa Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa kwa kumwelezea kuwa ni jabali la hekima ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.
Waziri Lowassa alimmwagia sifa hizo Msekwa jana wakati wa hafla maalumu ya kumuaga, iliyofanyika katika ukumbi wa kisasa wa Bunge, mjini Dodoma. Hafla hiyo pia ilikuwa kwa ajili ya kuwaaga wabunge wanaotarajia kumaliza kikao cha bajeti leo.
Waziri Lowassa alisema Msekwa amekuwa kwenye nyadhifa mbalimbali za uongozi, kwenye kamati zilizotoa maamuzi mazito ndani ya taifa hili, na kwamba anahitaji muda mrefu wa kumwelezea kutokana na hekima na busara alizozionyesha wakati wa utumishi wake katika taifa hili.
“Msekwa… aaah, niseme nini, maana aliyofanya ni mengi. Kwanza ni mwalimu wangu wa kwanza wakati najiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), nikiwa kwenye chama na serikali, Msekwa ni mwajiri wangu, amenilea na kunitunza. Nasema Msekwa ni jabali la hekima ndani ya CCM,” alisema Waziri Lowassa huku akishindwa kupata maneno kamili ya kumwelezea.
Waziri Lowassa alisema hafla ya kumuaga Msekwa ambayo ilifana, ni kielelezo kwa viongozi wengine waliopo madarakani, kwamba wakifanya vizuri katika kipindi chao cha uongozi, wataagwa kwa heshima kubwa kama ilivyo kwa Msekwa.
Kwa upande wake, Spika wa sasa wa Bunge, Samwel Sitta alisema kuanzia sasa ukumbi wa zamani wa Bunge, utaitwa Ukumbi wa Pius Msekwa.
Alisema serikali imeamua kutoa jina hilo ili kumpa heshima mzee Msekwa kutokana na utumishi wake uliotukuka alipokuwa madarakani.
“Msekwa ndiye aliyetuingiza kwenye mageuzi ya vyama vingi, na pia aliweza kuliongoza Bunge la vyama vingi vizuri. Nitaiga mfano wake,” alisema Sitta.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuagwa, Msekwa mwenyewe alisema kwanza hakutarajia kupata heshima ya kuagwa kwa kiwango kile.
Alisema hivi sasa anajiandaa kutoa kitabu na machapisho mengine ya kuelezea historia ya taifa hili, hasa wakati wa kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja na kuwa na vyama vingi.
“Kwangu mimi tukio kubwa la kihistoria ambalo haliwezi kujirudia tena, ni hatua ya kutoka kwenye chama kimoja na kujiunga na vyama vingi, na hivi karibuni nitatoa kitabu cha kuelezea mageuzi hayo,” alisema Msekwa.
Alitumia muda mwingi kumshukuru Spika wa kwanza wa Bunge la vyama vingi, marehemu Chifu Adam Sapi Mkwawa kwamba alimfunza mambo mengi, na uzoefu wa kuliendesha Bunge, alijifunza kutoka kwake.
Pia alielezea wasifu wake na nyadhifa alizoshika wakati akilitumikia taifa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, John Samweli Malecela, alikasirishwa na hatua ya Msekwa kusoma wasifu wake badala ya kazi hiyo kufanywa na kamati iliyoandaa sherehe hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama.
“Nimepata wasiwasi sana, Msekwa, Msekwa… hawezi kusimama hapa atuambie alifanya nini na badala yake sisi tungesimama kumwelezea Msekwa ni nani, mimi nimesikitika sana na nimepata wasiwasi mkubwa,” alisema Malecela.
Malecela alitumia muda mwingi kumsifu Msekwa kwamba ndiye aliyeliingiza taifa kuwa ndani ya mfumo wa vyama vingi wakati akiwa Spika.
“Sitta wakati huo akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, alileta mswada bungeni wa kutaka nchi iwe ya mfumo wa vyama vingi na Msekwa ndiye aliyeendesha mjadala bungeni wa kupitisha sheria hiyo,” alisema Malecela.
Naye Katibu wa Bunge, Damian Foka, alitangaza zawadi alizopewa mzee Msekwa.
Alitangaza zawadi hizo kuwa ni kompyuta moja kubwa, yenye Printer na Laptop wakati mkewe Mama Anna Abdallah alipewa zawadi ya mashine ya kufulia nguo na Microwave (Mashine ya kupashia moto chakula).