Na Hassan Issa, Zanzibar
KILICHOMPATA Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, wiki mbili zilizopita, kimemgeukia Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Hali hiyo ilijitokeza jana pale kundi kubwa la wapenzi, wafuasi na wanachama wa chama hicho walipomvaa na kumzuia kiongozi huyo, wakidai kujua hatima ya mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
Ilikuwa saa 4 asubuhi wakati Maalim Seif akiwa ndani ya gari lake, akiwasili ofisini kwake Mtendeni mjini hapa, ilipo ofisi kuu ya CUF, aliposhitukia kundi hilo la vijana, wazee, wanawake kwa wanaume, likimzingira huku likipiga makelele ya kuashiria kutoondoka na pia kutomruhusu kiongozi huyo kuondoka wala kuingia ofisini mwake, mpaka kieleweke.
“Hatuondoki hadi kieleweke”, ndivyo walivyosikika mamia ya watu hao wakiimba mfululizo, hali iliyosababisha rabsha na mshituko mkubwa kwa baadhi ya wanaCUF, akiwamo Maalim Seif mwenyewe.
“Silaumu mkusanyiko huu niko pamoja nao, na huu ni ujumbe halisi kwa Rais Kikwete na Serikali zote, kwamba sasa ni mwisho wa subira wa wanaCUF,” alisema Maalim Seif akijaribu kuwatuliza watu hao walioonekana kuwa na ghadhabu.
Aidha Maalim Seif aliwahakikishia watu hao akisema kuwa jambo lipo linakuja kabla ya mwisho wa mwaka, ila la kujiandaa zaidi ni kuwa endapo ni la kuridhisha, wauoneshe ulimwengu kuwa wameridhika na ikiwa kinyume chake, pia lazima wanaCUF wauoneshe ulimwengu.
Maalim Seif aliongeza kuwa endapo kuna baadhi ya viongozi wa Serikali na wa chama tawala, wanaubeza mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar wakidai kuwa kilichobaki ni shinikizo lake tu, basi ni vyema ieleweke kuwa tukio hilo linawasilisha ujumbe halisi, na pia kwamba baadhi ya viongozi hao wanaelewa kuwa Zanzibar ikilipuka wao wana pa kukimbilia.
Alirudia msimamo wake na wa chama cha CUF kuwa kwa sasa hawatachukua hatua ya kufuatilia maongezi ya kidiplomasia na viongozi wa nchi, kwani CUF inaelewa kuwa imekuwa ikiibiwa na kudanganywa mara nyingi tangu uchaguzi wa mwaka 1995.
“Tunaelewa diplomasia ina umuhimu wake katika kutatua migogoro, lakini kwa Tanzania hii tutaelekea katika miafaka tu isiyotekelezwa na hilo asilan CUF hailikubali,” alisisitiza.
Aidha alionya kuwa kama Rais Kikwete alitoa ahadi yake kwa dhati kabisa katika kuutatua mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, basi wakati umefika, kwani viongozi wa CUF wanaelekea kushindwa kuzuia hamasa za wanachama wao waliowatuliza kwa miaka mingi sasa.
Pamoja na mambo mengine, kundi hilo la wanaCUF lilidai mbele ya Maalim Seif, kuwa endapo viongozi wanaona mambo ni magumu katika kupigania suluhu ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar, basi warejeshe ajenda kwa wanachama wenyewe.
Maalim Seif aliwatuliza watu hao ambao awali walionekana kumtoa jasho, pale alipotumia usemi kuwa wameweza kumla ng'ombe mzima wasishindwe kumalizia mkia, akiwataka wawe na subira zaidi, naye na viongozi wenzake wa CUF wanapigania suluhisho la mgogoro huo.
Mtafaruku huo ambao ulimalizika kwa utulivu bila ya majeruhi yeyote, ulionekana kuwashitua baadhi ya watendaji wa mamlaka za ulinzi na usalama, ambapo askari wa Polisi walionekana wakizungukia mara kwa mara eneo hilo tangu alfajiri.
Naye Peter Mwenda anaripoti kutoka Dar es Salaam, kuwa CUF kwa kushirikiana na vyama vya Upinzani vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, wameandaa mapokezi ya wabunge wao na kufanya mkutano wa hadhara kuwapongeza, kwa kazi waliyofanya katika Mkutano wa Bunge la Bajeti.
Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uhusiano wa Umma wa CUF, Bw. Mbaralah Maharagande, alisema jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habri (Maelezo) kuwa mapokezi hayo yataanzia Ubungo Maji na hadi viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam kwa mkutano wa hadhara.
Alisema maandamano hayo yatapokewa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba akishirikiana na viongozi wa vyama vya Upinzani vya TLP, CHADEMA na vinginevyo, ambavyo havina wabunge, kuzungumzia mwelekeo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Bw. Maharagande alisema kati ya mambo yatakayozungumzwa katika mkutano huo wa hadhara, ni kuwa viongozi wa CUF bado wanasubiri ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kukaa pamoja kujadiliana kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uhusiano wa Umma wa Zanzibar, Bw. Salim Dimani, alisema CUF inampongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bw. Samwel Sitta, kwa kuliongoza Bunge bila upendeleo kwa CCM na watamwalika kuhudhuria mkutano huo.
Alisema Spika amekuwa 'mwiba' kwa wabunge wa CCM ambao siku zote walifanya mambo wakiamini kuwa Bunge hilo ni mali yao na watafanya wanavyotaka.
Alisema katika hali ya kisiasa visiwani wanachama wa CUF visiwani wamesubiri kwa muda mrefu kuhusu majadiliano ya pamoja kati yao na CCM, hadi jana ambapo walikusanyika na kumtaka Maalim Seif aeleze sababu za kutofanyika mazungumzo hayo.