Na Thomas Kiani, Singida
MKAZI wa kijiji cha Musimi kata ya Sepuka Singida vijijini, Bibi Habiba Shabani amejifungua watoto wa watatu kike watatu kwa mpigo.
Kwa mujibu wa habari kutoka kwa mama huyo aliyesaidiwa na mkunga wa jadi Bibi Mwajuma Choyo, zilisema huo uzazi wa tatu kwake.
”Mara ya kwanza nilijifungua mtoto wa kiume, mara ya pili wa kiume, safari hii watatu wa kike kwa mara moja,” alisema.
Katika watoto hao watatu, wa kwanza alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 2.1, wa pili kilo 2.02 na wa mwisho kilo mbili.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Italala anamoishi mzazi huyo, Bw. Shabani Gunda, alisema mama huyo alijifungulia nyumbani salama watoto wote watatu Julai 21 mwaka huu na baadaye kupelekwa kituo cha afya cha Sepuka kwa uchunguzi zaidi ya afya yake na watoto wake.
Maelezo kutoka kituo hicho cha Sepuka yalieleza kwamba mama na wanawe walikuwa na afya nzuri.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Musimi, Bw. Jumanne Njoghomi, ambaye alikwenda kuwajulia hali watoto na mama yao mzazi na kumpongeza, alisema haijawahi kutokea tukio la namna hiyo la kuzaliwa watoto watatu kwa mara moja tena wa kike katika kijiji chake na hata vijiji vya jirani.
Alimsifu baba wa watoto hao, Bw. Ramadhani Makiya, kwa kuwa mvumilivu muda wote wa ujauzito wa mkewe na kumtakia heri na hekima katika kuwalea watoto hao inavyotakiwa.
Kwa mila na desturi za kinyaturu kabila la familia hiyo, inahesabiwa kwamba ni tukio la kishujaa kwa wazazi wote hivyo wazee na makungwi hutakiwa kujumuika pamoja na kufanya sherehe siku nzima.
Pia hutoa maombi maalumu ya kuwatakia heri na fanaka katika malezi ya watoto hao.
Wazazi wa mapacha hao waliiomba Serikali na jamii na asasi zote kuwasaidia katika malezi ya watoto hao kwa sababu hawana uwezo wa kimapato