Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mabiti; hili la tumbaku hutaliweza
Mabiti; hili la tumbaku hutaliweza
By Habari Tanzania | Published  08/15/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

NALAZIMIKA kuandika maoni yangu katika ukurasa huu, baada ya kushtushwa na kauli ya Mkuu mpya wa Wilaya (DC) ya Manyoni mkoani Singida, Paschal Mabiti.

Alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba, anaangalia uwezekano wa kupiga marufuku kilimo cha tumbaku wilayani humo, eti kwa vile mazingira yanaharibika. Nasema Mabiti hawezi kamwe. Labda amewachoka wakulima hao, lakini namthibitishia kuwa hataweza hilo.

Kabla ya kuhamishiwa Manyoni hivi karibuni, Mabiti alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, na wengi wanafahamu mambo yake aliyoyafanya; mema na yale yaliyowaudhi watu, ikiwa ni pamoja na kukamata waandishi wa habari na kuwasweka ndani.

Kufika tu Manyoni, anatoa kauli ya kutishia kupiga marufuku kilimo cha tumbaku wilayani humo. Mimi sielewi kama kweli alipofika hapo Manyoni alipokea taarifa yoyote inayohusiana na kilimo cha tumbaku katika wilaya yake na akaipitia kwa makini.

Naomba sasa, kabla ya kuendelea na hoja hiyo, nimfahamishe rasmi, kwani inawezekana hafahamu mambo ya tumbaku, kwa sababu wilaya aliyotoka haizalishi tumbaku. Labda ndiyo maana ameibuka na hoja hiyo nzito ambayo nimeona nikikaa kimya, inaweza kuibua uhasama mkubwa kati yake na wapenda maendeleo.

Kwanza, tumbaku ni zao la biashara na baadhi ya wananchi wake anaowaongoza hivi sasa wanategemea kilimo cha tumbaku ili kuendesha maisha yao ya kila siku, mfano kulipia ada za watoto wao na mahitaji mengine muhimu. Tumbaku ndilo zao kuu walilolizoea. Kama Mabiti anaona halifai, basi awaeleze wakulima hao wafanye nini kuliko kuwatishia.

Mabiti anatakiwa kuelewa kwamba, kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kuna kikao cha Halmashauri ya Tumbaku nchini ambayo hukutana na wadau wote wa tumbaku hapa nchini kujadili mfumo wa kilimo.

Moja ya ajenda kubwa katika vikao hivyo ni suala la upandaji miti, ambapo mnunuzi anatoa miche kwa wakulima, na wakulima wajibu wao ni kuipanda.

Hebu tafadhali, Mabiti asome mkataba wa kilimo cha tumbaku kifungu cha 3.13, ambacho kinaelezea suala la upandaji miti, ambapo muuzaji, yaani mkulima, atapokea mbegu za miti kutoka kwa mnunuzi kupanda au kuelekeza zipandwe kwenye shamba lake la miti kwa ajili ya kuni za kukaushia tumbaku.

Muuzaji hataruhusiwa kupata mkopo wa pembejeo kutoka kwa mnunuzi, hadi ahakikishe amepanda miti isiyopungua mitano kwa kila mfuko mmoja wa mbolea ya NPK, ambayo ataipokea kwa mnunuzi, sawa na miti 50 kwa kila tani moja ya tumbaku atakayoizalisha.

Haya ni makubaliano yaliyopo kati ya mnunuzi na muuzaji, ambaye ni mkulima, na Halmashauri ya Tumbaku ndio wasimamizi wakuu wa mkataba huo. Naamini hapo kwa Mabiti (Manyoni) napo, maofisa kilimo wapo na wana mikataba hiyo kama si kushiriki wenyewe katika vikao hivyo vya makubaliano.

Uamuzi na msimamo huo wa Mabiti hauendi sambamba na kauli ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyotoa siku alipokutana na wakuu wa mikoa, wilaya, wanunuzi na wadau wote wanaotoka katika mikoa inayozalisha tumbaku hapa nchini.

Kwa ufupi, alitoa mwito wa kuzalisha tumbaku mara mbili ya uzalishaji wa sasa. Je, Mabiti ambaye wakati huo alikuwa Tarime na sasa yupo Manyoni, analijua hilo?

Mimi nakubaliana na sula zima la utunzaji wa mazingira. Hii haina ubishi hata kidogo, kwani ndiyo sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichounda serikali, na hata wapinzani na wasio na vyama wanaunga mkono utunzaji wa mazingira.

Zipo sheria ambazo zinaelezea suala la mazingira, na kama halmashauri ya tumbaku, wanunuzi na wauzaji wamekubaliana kupanda miti, basi wale wasiotekeleza hilo ndio awaseme, awachukulie hatua na si kusema tu kuwa atapiga marufuku kilimo cha tumbaku wilayani mwake. Hii si kweli hata kidogo, ni kuwahukumu watu wasio na hatia ambao wanatekeleza maagizo yote.

Mimi namshauri Mabiti afuatilie kwa makini taratibu na sheria zilizopo zinazohusu kilimo cha tumbaku. Uzoefu wa kilimo cha tumbaku ni mkubwa nchini.

Maeneo mengine ambamo hufanyika kilimo hicho ni hata hapa kwetu Songea, Chunya, Mpanda, Iringa, Tabora na maeneo mengine mengi hapa nchini. Kote wanatumia kuni kukaushia, na hii haikuanza leo, ni miaka na miaka, na ndiyo maana hata viwanda vya tumbaku vikajengwa.

Akumbuke kwamba, sehemu kubwa ya wakulima wa maeneo niliyoyataja, ikiwamo wilaya yake ya sasa, wanajipatia riziki yao kupitia zao hilo na si vinginevyo. Kwa hiyo, kupiga marufuku ni sawa na kuwaadhibu, kuwakatili na kutowatendea haki.

Hata hivyo, inawezekana DC huyu ana hoja ya msingi, labda sikumwelewa. Naamini anaweza kutoa ufafanuzi lakini kama kauli yake ni hiyo ya kupiga marufuku, amechemsha, sitamuunga mkono, na ipo siku akishazoea katika wilaya hiyo mpya, atabaini kuwa kilimo cha tumbaku ni uti wa mgongo wa wananchi wake, ambao kwa sasa amewapiga mkwara wa kutaka kupiga marufuku kilimo hicho.

Mwisho, namshauri apitie sheria za zao la tumbaku, atabaini wazi kuwa suala la upandaji miti limetiliwa maanani. Wanaokiuka anajua jinsi ya kuwabaini na awachukulie hatua. Wapo wanaopanda miti na kuichoma, hawa kweli sikubaliani nao. Kazi njema Mabiti.

Adam Mwaibabile ni mwandishi mwandamizi, mwenye makazi yake mjini Songea, na anapatikana kwa simu; 0784271515 au barua pepe; mwaibabile2000@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.