Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Filamu ya Mapanki; zipo wapi sauti za wanaharakati?
Filamu ya Mapanki; zipo wapi sauti za wanaharakati?
By Habari Tanzania | Published  08/15/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na mashirika mengine ya kijinsia wanapenda kutoa mchango wao kwenye gumzo lililozuka kuhusu mazingira ya kimaudhui yaliyoitawala filamu ya Darwin’s Nightmare inayozungumzia biashara ya samaki na habari ya umaskini wa wakazi wa Mkoa wa Mwanza.

Mjadala mkubwa umezuka kuhusu maudhui ya filamu hiyo, ingawa wananchi wengi bado hawajaiona. Tunataka kujiuliza kuna nini kimejificha katika maudhui yake na kwa nini imekuwa na malumbano?

Je, ni kwa manufaa ya nani filamu hiyo imetengenezwa? Imeambatana na inatufundisha siasa za mabara za kibeberu na mfumo dume? Haya ndiyo aina ya maswali tunayouliza na tunatumaini taarifa hii itawahamasisha na kutia watu moyo kufuatilia suala hili.

Filamu hii inazungumzia nini? Filamu hii ya Darwin’s Nightmare inaelezea biashara ya samaki inayoendeshwa na kampuni zinazomiliki viwanda vikubwa vilivyopo kandokando ya Ziwa Victoria, wakishirikiana na kampuni za biashara za samaki zilizopo Ulaya.

Filamu hiyo inaonyesha namna ambavyo kampuni hizo zilivyojinufaisha na biashara hiyo kwa kusafirisha samaki hao nje ya nchi, wakati wananchi wa Mwanza na nchi za jirani wakiendelea kuwa maskini.

Inaeleza pia kuwa, wakulima wamekuwa wakilazimishwa kuhama kwenye mashamba yao, ikiwa ni matokeo ya utandawazi, wakiacha wenye viwanda na wachimba migodi kuendelea kutumia maeneo yao, wakati wao wakienda mijini kufanya biashara za kimachinga na ukahaba, na watoto wao wakiishia kuwa watoto wa mitaani.

Jamii ya wavuvi inanyimwa haki yao ya kufanya uvuvi wao wa asili, hasa kwenye maeneo waliyozoea kwa kigezo kuwa wanaharibu mazingira. Matokeo yake watoto wao wanakimbilia mjini na kufanya biashara za ukahaba.

Filamu hiyo inaelezea kutokuwapo usawa huo kwa kufananisha namna ambavyo minofu minono ya samaki aina ya sangara inavyosafirishwa kwenda ng’ambo, huku wananchi wa Mwanza wakiachiwa vichwa vya samaki na mifupa, maarufu kama mapanki.

Filamu hii inaelezea kuwa biashara ya samaki imo kwenye ukanda wa biashara wa pembe tatu kati ya Ulaya, nchi za Kongo, Angola na Mwanza. Pembe tatu ambapo bunduki na risazi zinapakiwa kutoka Ulaya na kupelekwa nchi zilizo vitani, ambazo ni Kongo, Angola na nchi nyingine kwenye ndege zilizochakaa za Ulaya Mashariki, ambapo tena ndege hizi hubeba samaki kutoka Mwanza kurudisha Ulaya.

Mfumo huu wa biashara unafanana na mfumo wa biashara ya utumwa ya zamani, ambapo meli kutoka Mashariki ya Mbali zilileta nguo, silaha, shanga na vitabu vitakatifu Afrika na kuchukua pembe za ndovu, karafuu na watumwa kwenda Ulaya na bara Arabia.

Mfumo na usanii wa hali ya juu uliotumika kuitengeneza filamu hii unaifanya kuwa na hisia kali na mhemko mkubwa, hivyo kuchangia kutoa hisia nyingi tofauti za kutatanisha.

Ni sauti za kina nani zinasikika katika filamu hii? Filamu imejikita kwenye picha na mahojiano na kundi la wasichana wanaofanya biashara ya ukahaba, watoto wa mitaani na rubani wa moja ya ndege zinazosafirisha minofu hiyo ya samaki.

Filamu hiyo pia imefanya mahojiano na watu binafsi, wakiwamo mmiliki wa kiwanda cha kutengenezea samaki na mwandishi wa habari.

Kwa mtazamo wa haraka wa macho, ni nini cha kitofauti mno kuhusu habari hii? Ripoti za serikali kama ile ya Umasikini na Maendeleo ya Jamii ya mwaka 2003 na 2005 zimethibitisha kuwa idadi kubwa ya Watanzania hawajanufaika na ukuaji wa uchumi na kuwa kuna tofauti kubwa kati ya matajiri na masikini kutokana na sera za uchumi huria na ubinafsishaji.

Habari hizi zinabeba taarifa sawa kila siku; wakulima wanalazimishwa kuuza maharage bora zaidi Malawi na Zambia na kuacha maharage na mawe yasiyo na ubora ‘mapanki’ kwenye soko la ndani ya nchi sawasawa na kahawa na chai. Wananchi wengi hasa waishio vijijini wameshindwa kumudu maisha yao kutokana na athari za utandawazi.

Wananchi wengi wamepoteza ardhi zao kwa kampuni za utalii na migodi. Walionyanyasika na kuathirika zaidi ni wasichana na wanawake, wengi wao wamelazimika kuingia katika biashara ya ukahaba kwa kukosa shughuli mbadala ya kufanya, kama ambavyo vijana wadogo na wanaume wamefurika njiani kama wamachinga na wafanyabiashara wadogo wadogo na wafanyabiashara ya mapenzi pia.

Je, filamu hii ina matatizo gani? Tunaamini suala kubwa ni upungufu wake kutoshirikisha na kunakili ongezeko la harakati za jamii ya Kitanzania na makundi ya wanaharakati yanayotoa changamoto kwenye masuala mazima ya utandawazi na mfumo dume katika ngazi zote.

Zipo wapi sauti za wanaharakati wa nchini wa mazingira na haki za binadamu ambao wanapiga vita biashara ya kampuni kubwa za samaki, kutokana na kuharibu mazingira ya Ziwa Victoria na kuwatelekeza wavuvi wadogo wadogo kupata rasilimali zao za ziwa?

Zipo wapi sauti za vyama vinavyotetea haki za watoto wa mitaani bila kuchoka na vyama vya wanajinsia wanaotetea haki za wanawake Mwanza na kwingine, pamoja na haki za wafanyabiashara ya mapenzi?

Kwa nini basi filamu hii imeangalia tu upande mmoja wa jamii na kukandamiza jamii ya Kitanzania bila kuonyesha namna ambavyo wanawake, wanaume na watoto wa Kitanzania wanavyokazana kupinga hujuma zinazotokana na harakati za utandawazi, kukosekana usawa katika matabaka ya watu na mfumo dume?

Kama madhumuni ya mtayarishaji wa filamu ilikuwa ni kuangalia ubaya wa utandawazi kwa kuangalia habari ya biashara ya samaki wa Ziwa Victoria, kwa nini alishindwa kuwahusisha viongozi wa taasisi za kijamii, wanaharakati walio kinyume na utandawazi na watengenezaji wa filamu wa Kitanzania ili kupata picha halisi ya harakati dhidi ya utandawazi unaofanywa na Watanzania ili ionyeshe picha halisi ya harakati hizo?

Tunajiuliza pia, kwa nini mtayarishaji huyo hakuhakikisha kuwa filamu hiyo inaonyeshwa kwa Watanzania, hasa kwa kuwapa kipaumbele wao kwanza kwa sababu ni walengwa, hasa Watanzania wa Mwanza?

Majibu kwa maswali haya yanasaidia kuonyesha namna ambavyo filamu hii ilitayarishwa na kusambazwa katika mazingira ya mfumo wa ukoloni mamboleo. Hii inatuelekeza kwenye suala muhimu; je, filamu hiyo ina athari gani kitaifa na kimataifa? Katika ngazi ya kitaifa, filamu hii imewezesha kuweka wazi biashara ya samaki, hasa kwa wananchi ambao walikuwa hawajui habari ya biashara ya viwanda vya samaki wa Ziwa Victoria.

Katika mtafaruku ambao umegubika filamu hii, wauzaji samaki wakubwa wamefanikiwa kupata kuungwa mkono na jamii, kama tulivyoona kwenye maandamano ya halaiki kupinga. Imeonekana kwamba wamiliki, matajiri wa viwanda vya samaki wameonekana kuwa ndio walioonewa (victims) na si wanawake, wanaume na watoto maskini na waliowekwa pembezoni na kupoteza utu wao kutokana na umaskini uliokithiri.

Kutokana na siasa za mabara ya kibeberu, tunapaswa vile vile kujiuliza; ni nini matokeo ya mtazamo wa filamu hii kwa watazamaji wa Ulaya? Ni kweli kwamba watu wengi wenye nia njema – wanawake na wanaume wameacha kula sangara kutokana na ujumbe wa filamu hii?

Na kama ni hivyo, je, hii si kwa sababu za kibiashara za ushindani wa biashara Ulaya na kwinginepo ambako pia walifaidika awali na kufungiwa kwa uuzaji wa minofu ya samaki wa Ziwa Victoria na Umoja wa Ulaya?

Tunatambua utata ulipo kwenye kutengeneza na usambazaji wa filamu hii, tunatarajia utata uliojitokeza hautuondoi kwenye mtazamo wetu kwenye masuala makubwa ya msingi yaliyojitokeza kwenye filamu hii.

Kwa mfano, kati ya viongozi wa jamii ya wavuvi, kuna mvutano mkali katika eneo la ziwa juu ya nani amiliki samaki wanaopungua kila siku – wavuvi wadogo wa asili au kampuni kubwa za uvuvi wa samaki?

Nini kinahitajika kumaliza tofauti zinazoongezeka kati ya Watanzania wachache matajiri na wageni ambao wanaweza kuishi katika majumba makubwa ya kifahari na kula minofu ya samaki katika hoteli kubwa za kifahari za kitalii na maskini walio wengi?

Maskini na walio pembezoni wanaweza wakaongeza sauti na nguvu zao kumiliki rasilimali hizi na kuwa na maisha yenye heshima na utu, bila kulazimishwa kwenye biashara ya mapenzi au kuishi maisha ya kutegemea mitaani.

Sisi wote tunataka kuwe na mjadala wa sera ya ‘neo-liberal’, soko huria na ukuaji wa nguvu za ‘corporate-led’ utandawazi katika nchi yetu. Kama sehemu ya mjadala, Watanzania wote wanahitaji kujionea filamu hii ya Darwin’s Nightmare na kujadili maudhui yake.

Changamoto kubwa itakuwa kuitafsiri filamu hii kwenye Kiswahili na kusambazwa zaidi kwenye vituo vya televisheni na mahali pa video kuhakikisha kila Mtanzania anajumuishwa katika mjadala.

tamwa@raha.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by nthelezi nesaa nkwazi)
    Rating
    The Darwin뭩 Nightmare

    Na nthelezi nesaa


    Safu hii leo imelazimika kuingilia mjadala na mdaharo juu ya kile kinachoitwa The Darwin뭩 Nightmare. Hii ni baada ya watanzania wengi hasa wanaoishi ndani na nje kuitaka iseme japo kidogo kuhusu mjadala huu juu ya ukweli na hali halisi ya documentary hii.

    Katika kuangalia namna Rais Jakaya Kikwete alivyoshupalia suala la filamu ya The Darwin's nightmare, mtu yeyote mwenye akili anashangaa ni kwanini Rais anapoteze muda wake na wa taifa,heshima na mengine kama hayo kujiingiza kwenye kutafuta majibu ya maswali ambayo yaliishajibiwa.
    Documentary hii nzuri ilitengenezwa na mtenezaji filamu Hubert Sauper ambaye anajulikana kwa umaarufu wake kutengeneza filamu za kusisimua ili kujipatia riziki yake. Hivyo inakuwa ni makosa kutaka mtengenezaji huyu wa filamu awe na muda na hadhi na heshima ya nchi.

    Kwanza filamu inayomuhangaisha Rais haikutengenezwa jana wala juzi. Ina muda mrefu kwani ilitengenezwa akiwa waziri wa mambo ya nchi za nje. Hivyo kama kweli alikuwa na nia ya kuitetea hadhi ya nchi yake kama anavyotaka aonekane baada ya kuwa Rais, tunadhani angefanya hivyo muda mfupi baada ya filamu kutoka kwani ilikuwa kwenye eneo lake la utendaji kazi kama waziri wa mambo ya nchi za nje.

    Si mpya kwa sababu baadhi ya vyombo vingi vya habari vya huko nyumbani hasa magazeti vilishaelezea kilichomo humo. Hata waandishi wengi wa humo nchini wameishaandika sema kutokana na katabia kabaya ka jamii kusahau mapema machapisho,usishangae sakata hili kuonekana kama kitu kipya.

    Pia ifahamike kuwa hasara au taathira inazopata Tanzania na watanzania kutokana na madhara ya kadhia hii,yavilinganishwa yale yanayosababishwa na matatizo ambayo yako ofisini mwake na asifanye kitu,tena kwa kuwauliza wananchi,tunadhani suala la Documentary litaonekana kama upuuzi Fulani.
    Kwa mfano sifa ya Tanzania ni nini na ina maana gani ikilinganisha na madhara yatokanayo na sera nzima ya ubinafsishaji kama ilivyotekelezwa kijambazi na kibububusa na serikali iliyopita?

    Hatuoni kama The Darwin's Nightmare, kwa mfano ina madhara sawa na IPTL,Net Group Problems, Makampuni ya madini yanayoipa serikali mrahaba wa asilimia tatu ilhali kwa madini kama hayo hayo Nchi kama Botswana inapata zaidi.

    Hatuoni kama madhara yatokanayo na filamu hii yanaweza kulinganishwa na madhara yanayotokana na hujuma zinazofanywa na makampuni ya uwindaji na utalii huko mbugani.

    Kimsingi filamu hii inaongelea sehemu ndogo ya nchi yetu tofauti na madhara tajwa hapo juu yanayoikabili nchi yetu.

    Tunadhani Rais angeshughulikia masuala yanayoingia akilini mwa wananchi kwanza ya kupambana na uoza uliopita kiasi alioukuta ofisini mwake badala ya kufanya waingereza waitacho "witch-hunt and white wash"

    Hatuoni madhara yatokanayo na filamu tajwa maana inachosema ni ukweli kwani kama ni kuwepo kwa unyonyaji wa kiuchumi upo pale mwanza. Nani kasahau kuwa hata zile kashfa zilizowafukuzisha kazi akina Profesa Joseph Mbilinyi, Kilontsi Mpologomyi na Dr. Juma Ngasongwa inatokea huku.

    Japo siyo hoja katika mjadala huu,hata yakitakiwa maelezo kwa mfano ni kwanini wale waliokuwa wanaonekana kuwa makapi na mizigo kwa serikali iliyopita amewarudisha maofisini tena kwenye idara nyeti,tunadhani jibu litakuwa gumu. Haya kimsingi ndiyo mambo ya maana ya kuweza kumshughulisha Rais ili awape majibu watanzania na siyo ubabe.

    Ukifuatilia filamu ya The Darwin's Nightmare,utakuta kuwa mtengenezaji licha ya kuonyesha umaskini wa waswahili wa pale mwanza,alitaka mataifa makubwa ambayo ndiyo wanunuzi wakubwa wa sangara waone ni kwa kiasi gani wanachangia katika jinai hii ya umaskini kwa kununua kitu ambacho nadhani tafsiri ya haraka ni haramu.

    Hapa mtengeneza filamu licha ya kuwa mkweli,alikuwa makini kutaka kuwashawishi wanunuzi wa sangara kujua ukweli kuwa hawana haja ya kutumia pesa nyingi kiasi hicho kununua kitu ambacho kimezalishwa kwa bei nafuu hata kwenye mazingira machafu.

    Anayekana kuwa kilichosemwa na mtengeneza filamu si ukweli, ajiulize jina mapanki kwa mfano limetungwa na nani? Ni wananchi wenyewe. Je lina maana nzuri kiuchumi na kijamii?

    Hivyo kimsingi mtengenezaji wa filamu hakuwa na nia mbaya kama watawala wetu wanavyoiangalia. Hivi kwa mfano mtu akionyesha mayatima walioko Makete na mateso wanayo yapata utasema ameidhalilisha nchi?

    Juzi hapa Canada Televisheni ya CBC,usiku ilionyesha picha ya waathirka wa ukimwi huko nchini Zambia. Kwa bahati nzuri Documentary hii ilitengenezwa na mtengenezaji filamu na mwandishi mashuhuri Sorius Somirwa, kutoka Afrika Magharibi.

    Ni aibu na uchungu ukiangalia watu kwanza walivyo maskini na wajinga ukiachia mbali mateso wanayopewa na ukimwi. Ukiwalinganisha kwa mfano na aliyekuwa Rais wao Fredrick Chiluba,picha yao ni aibu kwa Zambia lakini huu ndiyo ukweli na hali halisi. Sasa mtengenezaji makala kama haya afanyeje ili asionekane anamomonyoa hadhi ya nchi?.

    Je kwa mfano wenye viwanda Mwanza hawanyonyi wananchi wanaoshughulika kwenye industry ya uvuvi?

    Hilo tuache,ukija suala la umalaya. Ni kweli kuwa si jambo la kutia chuku kuwa nchini Tanzania na Kenya wanaharakati wa ukimwi wanapata kibarua kigumu kupambana na ongezeko la waathirika wa ukimwi kwenye visiwa vilivyomo kwenye ziwa Nyanza.
    Visiwa vimevuta hisia za wanaharakati wa ukimwi kutokana na ukweli kuwa kuna umalaya wa kupindukia kwenye visiwa hivyo.

    Filamu ikisema kuna umalaya Mwanza tunadhani siyo kutukana wala kuidhalilisha Mwanza wala Tanzania. Ni hali halisi na ni ukweli mtupu.

    Hivi kwa mfano mtu akisema kuwa maeneo ya Kinondoni na Ohio jijini Dar es salaam na Kwa Macheni yanaongoza kwa vitendo vya kimalaya atakuwa anaaibisha jiji na nchi?
    Je kwa mfano mtu akitoa documentary kuonyesha watanzania japo si wote ,walivyopoteza utu kiasi cha kufanyia ngono kwenye makaburi ya Kinondoni bila aibu wala utu, atakuwa anaidhalilisha nchi na jiji.

    Au hata mtu akitoa documentary kuonyesha ubomu wa wasomi wa kitanzania kutokana na kukithiri kwa wizi wa mitihani ataambiwa anaihujumu nchi? Ni nani anahujumu nchi kati ya yule anayetenda na yule anayeandika. Hii ni sawa na kulaumu chombo cha habari kwa kuandika uchafu wako wakati hutaki kujilaumu kwa kufanya uchafu huo.
    Tunadhani Rais hapa aachane na masuala madogo ashughulikie masuala ya muhimu na nyeti kwa faida anwai ya wananchi badala ya sifa za juu juu.

    Tumalizie kwa kumshauri Ndugu Rais arejee kuiangalia na kufikiria upya juu ya filamu husika,hatuna shaka ataungana nasi kuwa kinachoelezwa mle siyo uongo bali ukweli.

    Kwa madai ya Mwanza kupitisha silaha,jibu la ukweli na uongo ni upi laweza kutolewa na swali fupi tu.
    Je unapobinafsisha hata mamlaka za kusimamia bandari na viwanja vya ndege unategemea nini kuhusu hili?
    nesaa1977@yahoo.com



     
  • Comment #2 (Posted by jabir hussein)
    Rating
    Mhariri,
    nimesoma maoni ya dada yetu nthelezi nesaa. anachosema dada huyo ni ukweli mtupu kuwa suala la mapanki ni kupoteza muda wa taifa bure maana halina umuhimu mkubwa kama mambo aliyojadili dada huyu. nimefurahi kuona maoni kama haya yanatolewa na mtanzania anayeishi mbali. inaonyesha ni kiasi gani anajali taifa lake maana wengi wakiisha ingia ughaibuni husahau kwao.
    natoa hongera zangu kwa mchango huu ambao kwangu ni bora na hakuna navyoweza kuelezea furaha yangu.
    hili liwe fundisho kwa wenzetu waliobahatika kusoma au kupata kazi nje.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.