SERIKALI ya Zimbabwe imepanga kuteketeza dola milioni nne, sawa na zaidi ya sh bilioni 4.8 kwa ajili ya ununuzi wa magari 320 ya kifahari kwa maofisa wa polisi wa ngazi ya kati.
Hatua ambayo wachambuzi wa mambo wanaiona kama hatua ya serikali ya Mugabe kujiongezea ukaribu na vyombo vya kijeshi ili kuendelea madarakani bila wasiwasi.
Vyanzo vya habari katika mamlaka husika vimekaririwa vikisema kwamba serikali imepanga kutumia zaidi ya sh bilioni 12 nyingine kununulia magari ya kijeshi na maofisa wa idara za usalama za siri.
Ripoti hizo zilikaririwa zikisema kuwa Rais Robert Mugabe ametoa amri ya ununuzi huo.
Hatua hiyo imekuja kipindi cha miezi miwili tu baada ya serikali kutumia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya jeshi na polisi kutokana na ushauri kutoka chombo cha juu zaidi kimamlaka katika usalama (JOC).
JOC ina undwa na wakuu wa majeshi ya ulinzi, anga, vikosi vya usalama, polisi na magereza.
Mapema mwaka huu, chombo hicho kilimlalamikia Mugabe juu ya kile ilichokieleza kuwa hali mbaya ya mazingira ya kazi miongozi mwa maofisa wa ngazi ya kati kote nchini hapa.
Kilipendekeza kuwapo kwa hatua za haraka za kuondoa hali hiyo miongoni mwa maofisa hao na kuongeza malipo ya mishahara na huduma nzuri zaidi.
Wasemaji wa polisi na jeshi hawakuweza kupatikana kuthibitisha suala hilo.
Waziri wa Usalama, Didymus Mutasa, alisema kuwa serikali inafanya juhudi za kuboresha hali za vikosi vya usalama japokuwa alikataa kuthibitisha suala la ununuzi wa magari.
Aliongeza: “Tunatambua upinzani utakaotoka kwa baadhi ya watu wasiopenda wala kufikiria mara mbili juu ya umuhimu wa kuboresha ya usalama wa watu.”
SAPA