Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sura mpya ya CHADEMA
Sura mpya ya CHADEMA
By Habari Tanzania | Published  08/15/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimefanya mabadiliko makubwa ya kimfumo na katiba yake.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema katika mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Dar es Salaam juzi kuwa, nia ya mabadiliko ni kukigeuza chama hicho kuwa chama taasisi.

Alisema wameamua kukipeleka kwa wananchi zaidi na sasa wataunda ubalozi wa nyumba kumi kumi, ambao wataeneza chama chumba hadi chumba kwa wananchi.

Chama hicho sasa kitakuwa na ngazi 10 za kiuongozi ambazo ni mabalozi wa nyumba kumi kumi, msingi utakaokuwa na vitongoji kwa vijijini na mitaa kwa mijini, matawi, kata, jimbo, wilaya ambazo zitawakilishwa moja kwa moja kwenye Baraza Kuu, mkoa, kanda, taifa na kimataifa.

Alisema chini ya mfumo huo, kila mwanachama atapewa jukumu la kuendesha chama, badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini ambayo alisema inatumika kunyonga vyama vya siasa.

“Leo CCM wameongeza ruzuku ya vyama. CHADEMA tumeongezwa kutoka sh milioni 35 hadi milioni 60 hivi. CCM wamejiongeza kutoka sh milioni 400 hadi sh bilioni moja… Na sasa Mheshimiwa Tendwa (Msajili wa Vyama vya Siasa), tunataka kila chama kitangaze kwenye magazeti matumizi ya fedha hizi,” alisema Mbowe.

Alisema CCM kinaogopa wapinzani, hakilali usingizi na ndiyo maana kwenye uchaguzi kinatumia polisi, dola, majeshi na mabalozi kuua vyama vya upinzani.

“Kama hawatuogopi waache siku moja twende kwenye uchaguzi huru. Wasitumie usalama wa taifa, polisi wala majeshi tuonyeshane kazi,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Alisema Watanzania wengi wamejaa hofu, kwani wamealikwa kwenye mkutano wa CHADEMA ila kutokana na hofu ya kuogopa wasionekane wanashirikiana na upinzani hawakufika kwenye mkutano huo.

Alisema CCM wameshindwa kuendesha mashirika ya umma, vyama vya ushirika, elimu inaporomoka, wafanyakazi hoi, rasilimali wanagenisha, umeme, maji.

“Kama wameshindwa haya yote, ni nini kitatuaminisha kuwa wanaweza serikali? Tuwaondoe,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Alifafanua rangi nne za bendera ya chama hicho kuwa ni nyeusi kwa ajili ya Waafrika; bluu, amani na haki; nyeupe kwa ajili ya usafi na nyekundu kwa ajili ya mashujaa waliopoteza maisha yao katika mapambano ya ukombozi wa taifa hili katika vita vya majimaji na kina Mirambo.

Pia, Mbowe alisema pamoja na wanachama kupewa jukumu la kuendesha chama, ruzuku itakayopatikana haitaishia makao makuu, bali itapelekwa kwenye wilaya kwa ajili ya kujenga chama.

Alisema katika kujiimarisha, chama hicho sasa kimeunda Baraza la Wazee, Baraza la Vijana, Baraza la kina mama na Baraza la Vijana.

Mwenyekiti huyo aliwaambia watendaji wa wilaya kuwa akienda mikoani wasimwandalie hoteli, bali yeye atalala kwenye nyumba za wana- CHADEMA na atakula wanachokula wao.

Huku Mbowe akitoa hayo, John Tendwa, yeye alisema sheria ya kuruhusu vyama vya siasa kuungana iko mbioni.

Alisema katika mabadiliko ya sheria za uchaguzi yatakayofanyika, vyama vya siasa vitaruhusiwa kuungana na kwa kufanya hivyo anaamini vingi vitajiunga na CHADEMA.

Tendwa alikisifia CHADEMA kuwa kimekuwa chama kisicho na migogoro na yeye kama mlezi anavutiwa na utamaduni wake wa kubadilishana madaraka kwa amani.

Wenyeviti wawili wastaafu wa CHADEMA, Edwin Mtei na Bob Makani, walitunukiwa vyeti vya utumishi uliotukuka na Mbowe alitunukiwa cheti cha ujasiri kwa kuwa wa kwanza kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 1992.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.