SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta sasa amekalia kuti kavu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na uamuzi wake wa kuruhusu Kampuni ya IPP Limited kumfungulia mashitaka mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM).
IPP inayomilikiwa na Reginald Mengi, imemfungulia mashitaka Malima kwa Spika wa Bunge, kwa maelezo kuwa hakuitendea haki, alipoliambia Bunge kuwa ITV inawanyima nafasi ya kutosha viongozi wa kitaifa katika taarifa zake, akiwamo Rais na Waziri Mkuu.
Spika alipokea malalamiko ya IPP na malalamiko ya Malima, lakini wabunge wengi wakawa wanamtumia vikaratasi wakisema kuwa amevunja sheria, kwani wabunge hawapaswi kushitakiwa na mtu yeyote au chombo chochote. Kesi ya Malima ni dhidi ya IPP, akilalamika kujibu hoja zake kwenye gazeti.
Sitta alipoona vikaratasi vimezidi, aliamua kutangaza bungeni kuwa wabunge wanapaswa kutambua kuwa hawapo juu ya sheria, na wananchi au taasisi yoyote wanaweza kuwafungulia mashitaka bungeni, kisha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikasikiliza mashitaka husika.
“Hili Sitta amepingana na maamuzi ya chama. Tulikubaliana kuwa wabunge waelezwe kamwe wasiseme uongo bungeni, lakini hatuwezi kuwaondolea kinga yao hivi hivi. Ndani ya vikao vya chama (CCM), tulisema tukiruhusu watu kuwashitaki wabunge, Bunge litakuwa halifanyi kazi zake, na Spika tukamweleza hivyo.
“Hata hivyo, kwa mshangao wetu sote tulio wengi, alipoketi kwenye kiti cha uspika akaamua kupingana na maamuzi ya chama, akatangaza aliyoyataka yeye. Chama hakiwezi kwenda kwa utaratibu huu, lazima iwepo nidhamu ya kuheshimu maamuzi ya vikao.
“Kwani Sitta ni nani CCM? Wamedhibitiwa wazito wenye mizizi, ijekuwa Sitta anayepepesuka? Tunampa muda ajirekebishe. Ajirekebishe na kujua kuwa uspika si ufalme, kwamba anaweza kufanya atakacho. Ngoja tuendelee kumchunguza na tutaona mbele ya safari kama ataendelea na tabia hii.
“Kimsingi ametugeuka kabisa CCM, anafanya kazi ya upinzani sasa. Kila hoja inayotolewa na wapinzani anaikubali. Kila hoja inayotolewa anaikubali. Tunapata maswali mengi kuhusu Spika huyu sasa,” alisema mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ambaye pia ni mbunge.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima, walisema wao wanamfurahia Sitta kwani ni Spika anayetekeleza aliyoahidi.
“Alisema yeye ni Spika wa Standard and Speed (kasi na viwango). Aliwaambia mara tu baada ya kuapishwa kuwa serikali haitaleta majibu ya ovyo ovyo akayakubali. Hivi walifikiri anatania? Anafanya kazi ya uspika si uenezi wa chama tawala,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Katika hali hiyo, wakati CCM wanakerwa na Sitta kwa utendaji wake kwa maelezo kuwa amewageuka, wanasiasa wa upinzani wanaona amepatikana Spika mwenye kutekeleza kanuni kadiri zinavyotakiwa kuwa