CHAMA cha Wananchi (CUF), kimelaani kitendo cha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, kuwafukuza waandishi wa habari wa vyombo visivyo vya serikali na chama hicho tawala mkutanoni alipokuwa kwenye ziara mkoani Singida.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Mbarala Maharagande, alisema juzi jijini Dar es Salaam kwamba, Makamba hakuwatendea haki waandishi, na alichofanya ni udhalilishaji wa wazi.
“Chama cha Wananchi kinalaani tabia hiyo ya ukiukwaji wa haki za binadamu na udhalilishaji, kwani waandishi hawa ni watu wenye heshima zao na taaluma zao.
“Bwana Makamba anapaswa kuomba radhi kwa waandishi wa habari kwa kitendo alichokifanya. Kama ni kikao cha ndani kama walivyodai, wangesema na hakuna mwandishi wa habari ambaye angezamia mahali ambapo hajaalikwa.
“Makamba ni mtu ambaye anapaswa kuwa taa kwa wengine na kufundisha watu kukuza demokrasia ya kweli, kwa kutoa habari kwa wananchi anaowaongoza. CCM kama chama kinachoendesha serikali iliyopo madarakani, hakipaswi kufanya mambo ya siri, kwani mambo yote ni kwa manufaa ya taifa, na kwa sababu wanasema wanatenda kutokana na sera za chama, lazima waseme mambo yao kwa uwazi zaidi, si kuficha,” alisema Maharagande.
Alisema Rais Jakaya Kikwete anamwamini sana Makamba, ndiyo maana alimpa nafasi hiyo, lakini yeye ameanza kuitumia vibaya kwa kunyanyasa watu, akiwa injini ya chama.
“Akikichezea chama hicho kama mpira, atakiangusha mara moja na kupoteza nafasi waliyo nayo,” alionya Maharagande.
Aliitaka CCM isimtetee Makamba, kwani amefanya kitendo hicho kama mtu mzima, hivyo anatakiwa ajitetee mwenyewe, awaone waandishi wa habari na awaombe msamaha.
“Anapaswa aache vyombo vya habari vimkosoe anapofanya mabaya na asifikiri kuwa kila mara ataandikwa vizuri tu, kwani hata mabaya yake na kasoro zake zinapaswa kusemwa hadharani na hilo ndilo alilowaambia waandishi wa habari kuwa wamekuwa wakimwandika vibaya. Atambue kuwa yeye si malaika wala Mungu.
Alisema CUF ilishapata kumwonya Makamba aache ubabe, akakataa, sasa ameupata ukatibu mkuu na anauendekeza.
Wiki iliyopita Makamba aliwatoa nje waandishi wa habari wa vyombo binafsi na kuwaacha wale wa vyombo vya serikali na chama chake, akidai kwamba waandishi wamekuwa wakimuandika vibaya.