Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mbowe: CCM wanalindana
Mbowe: CCM wanalindana
By Habari Tanzania | Published  08/14/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Deodatus Balile

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Serikali ya Awamu ya Nne imetumbukia katika mtego wa kulindana.

Mbowe alitoa kauli hiyo kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa CHADEMA uliofanyika katika Viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam, jana.

“Nilisema kuwa nchi hii haiwezi kuendelezwa na watu wale wale, wenye sera zile zile, wanaotoka chama kile kile, eti wakiendeleza yale yale kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya.

“Kinachotokea sasa serikali ya awamu ya nne inailinda ya awamu ya tatu na ya awamu ya tatu iliilinda ya awamu ya pili… hata Tume ya Warioba ilikuwa kanyaboya tu,” alisema Mbowe na kushangiliwa na wajumbe karibu 600 waliohudhuria mkutano huo.

Alisema serikali ya awamu ya nne haitaki kupambana, wala kukemea rushwa kwani vyombo vya habari vimeibua rushwa katika mifuko ya hifadhi za jamii, kampuni za migodi, lakini serikali imekaa kimya.

“Mheshimiwa Kikwete kigugumizi cha nini? Tunakumbuka hotuba yako ya Desemba 31, pale Dodoma uliahidi kupambana na rushwa. Tunakusubiri upambane nayo (makofi),” alisema Mbowe.

Huku akichagizwa na nyimbo na makofi kutoka kwa washiriki wa mkutano huo, alisema hajaona kama Rais Kikwete ana dhamiri ya kweli ya kupambana na rushwa kutokana na mfumo alioukuta na akauendekeza, hivyo akashauri: “Tunajipanga, na 2010, wananchi wajiandae kuchagua mabadiliko ya kweli; CHADEMA.”

Alimgusa Waziri wa Kilimo na Chakula, Joseph Mungai, na kuhoji kwa nini alimtukana muasisi wa CHADEMA, Edwin Mtei kwa yeye kutoa mawazo yake juu ya ubinafsishaji wa mashamba ya Mbarali.

Alisema kama Mungai anadai Mtei amezeeka, basi ni ajabu kubwa kwani Mtei na Mungai wote walikuwa mawaziri katika Baraza la Kwanza la Tanganyika huru, hivyo ni wazi naye hawezi kuukwepa uzee.

Mbowe alizungumza kwa uchungu mpango wa mabadiliko ya sheria unaoandaliwa kwa nia ya kubadili Sheria Na. 7 na 8 ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 kwa nia ya kumpa Waziri wa TAMISEMI mamlaka ya kuteua madiwani watatu kwa kila halmashauri nchini.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kudhoofisha upinzani, kwani eneo kama Karatu, CHADEMA inaongoza halmashauri kwa wingi wa madiwani watatu, Bariadi UDP inaongoza kwa wingi wa madiwani wawili na Kigoma CCM na CHADEMA zinashirikiana kuongoza halmashauri, hivyo wakiteuliwa watatu tena kutoka CCM kitakuwa na wingi wa madiwani hivyo kujihakikisha kuongoza halmashauri zote nchini.

“Rais Kikwete kama unaheshimu demokrasia sitisha mpango huu wa kunyonga demokrasia,” alisema Mbowe na kuongeza kuwa anashangazwa na viongozi wa chama tawala kwani kwenye majukwaa wanazungumza kukuza vyama vingi, lakini kwenye vikao vya ndani wanaandaa njia za kuvinyonga.

“Nawaambia viongozi wa CCM ni hatari. Kwa Kiingereza unaweza kuwaita ‘smooth operators’, watu wanaocheka lakini wanakunyonga. Kuna mikakati ya kunyonga upinzani, na mikakati yao mikubwa ni kunyonga CHADEMA,” alisema.

Aliwatahadharisha wananchi kuwa, kujaza wabunge wa chama kimoja bungeni, kunahatarisha masilahi ya taifa hili, kwani wengi wanashabikia chama tawala badala ya kutetea wananchi.

Alisema hata waliomo CCM hawajui kuwa wanakandamizwa, hivyo wanahitaji kukombolewa na chama kama CHADEMA, waweze kufaidi matunda ya uhuru. “Upinzani hauwezi kufa kwa mbwembe za majukwaani, porojo za majukwaani au ahadi zisizotekelezeka. Hizi zitainyonga awamu ya nne uchaguzi ujao.

“Bunge la upande mmoja hatumkomoi Mbowe, Lipumba wala Mrema. Ukweli hatuwatendei haki baba zetu, mama zetu na watoto wetu. Ndiyo maana siku zote nimekuwa nikisema kuwa Bunge ni mchezo wa kuigiza,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Pia alimgusa Rais Kikwete: “Nchi hii inashangaza sana. Tunaona Rais anasimama anakemea rushwa wakati ameingia madarakani kwa misingi ya rushwa... Hata hizo takwimu za kukua kwa uchumi ni mchezo wa kuigiza. Maisha ya Watanzania yameporomoka kweli katika hii miezi minane ya utawala wa Awamu ya Nne.

“Leo tunajipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2010. Siyo kwamba tutaingia kwenye uchaguzi huo kama wasindikizaji. Tutaingia kama timu iliyodhamiria kushika dola. Hatutaogopa polisi, usalama wa taifa, wala majeshi,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Alisema tangu uchaguzi umeisha Desemba mwaka jana, amekuwa kimya na jana ilikuwa mara yake ya tatu kuzunguza na jamii moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari na akawaelekeza CHADEMA kutoa tamko la kutangaza kuwa uchaguzi mkuu haukuwa huru na wa haki.

Alifafanua kuwa, aliamua kwenda Diamond Jubilee kupokea matokeo ya kura CCM walizoamua kumpa baada ya kumwibia vilivyo, kwa nia moja tu. “Kuna maisha baada ya uchaguzi. CHADEMA kamwe hakitakubali kuwa wakala wa kumwaga damu katika nchi hii. Tutaendelea kufanya siasa za kistaarabu na hatulali mpaka kieleweke (makofi).”

Kwa miezi hiyo minane, alisema walikuwa wakifanya utafiti ambao matokeo yake ni kubadili alama, nembo za chama na mfumo mzima wa kiuongozi kwa ajili ya kujipanga kukifanya chama kuwa taasisi na mshindani katika uchaguzi ujao.

Alieleza kuwa chini ya uongozi wake chama kimekua kutoka idadi ya wabunge wanane kufikia 11 na kutoka madiwani 44 kufikia 99, ingawa wengi waliibiwa kura nchi nzima na kushindishwa kwa mizengwe.

Alisema siasa za upinzani nchini Tanzania zinafanyika katika mazingira ya vitisho, uzandiki, lakini akasema ana hakika Mungu anaipenda kazi inayofanywa na upinzani, hata kama watawala hawaipendi na hawathamini mapenzi ya watu.

Alisema kama kuna mtu anapaswa kushutumiwa kwa kuua demokrasia katika nchi hii, basi ni Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa, aliyeua upinzani kwa kutumia Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na majeshi yote. Alipendekeza Mkapa na viongozi wa CCM wapewe elimu ya uraia.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by an unknown user)
    Rating
    good story
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.