CHAMA cha Wananchi (CUF), jana kimetambulisha jumuiya mpya ya wanawake (JWCUF), baada ya kufanyika marekebisho ya muundo wa kurugenzi ndani ya chama hicho. Kabla ya marekebisho hayo, muundo wa kurugenzi ya CUF, jumuiya hii ilikuwa ikitambulika kama Kurugenzi ya Wanawake.
Akizungumzia sababu za mabadiliko ya kurugenzi hiyo katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana, Kaimu Katibu wa JWCUF, Ashura Amanzi, alisema kuwa awali kurugenzi hiyo ilikuwa ikitenda kazi kama moja ya idara za chama hicho.
“Hapo mwanzo ilipokuwa kurugenzi ilifanya kazi kwa kubanwa, pia uchanga wa chama nacho kilikuwa kikwazo kingine kwa wakati huo, isitoshe kurugenzi ilikuwa inafanya kazi chini ya Katibu Mkuu,” alisema Amanzi.
Alieleza kuwa sasa, jumuiya inafanya kazi zake kwa uhuru na kujiamulia mambo yake yenyewe pasipo kuingiliwa na kurugenzi nyingine, kwani sasa wanafanya kama jumuiya. Alisema JWCUF mpaka sasa ina matawi katika wilaya 101 ambayo hapo awali yalikuwa kurugenzi na hivi sasa yatatambulika kama jumuiya.
Katika mpango wao watahakikisha wanakabiliana na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWTZ), umoja aliuponda kwa kusema kuwa upo kwa ajili ya maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na si kwa ajili ya wanawake wa Tanzania kama unavyonadiwa.
Katibu huyo alisema njia nyingine wanayoitumia katika kuhakikisha jumuiya yao inaikabili UWT, alisema JWCUF imewaandaa wajumbe wa mkutano mkuu kwa kila wilaya sanjari na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi ambao wote kwa pamoja watakuwa na kazi ya kuonana na viongozi katika wilaya husika.
Aidha, alieleza kuwa jumuiya hiyo itakuwa ikifanya kazi za jamii ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wanawake kujiunga na chama.
Hivi sasa chama hicho kinaandaa rasimu ya kwanza ya katiba ya jumuiya na baadaye kupitisha katika vikao vya chama. Aliisifu katiba hiyo kuwa imetayarishwa kwa kuzingatia misingi ya sera za CUF, na kuzingatia demokrasia na jinsia