WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, amewaomba wabunge wamuonee huruma, akisema wizara yake ni migogoro tupu.
Akiruka ‘vihunzi’ vya wabunge juzi jioni wakati wakihoji kabla bajeti yake kupitishwa, Magufuli alisema hakuna njia nyingine ya kutatua migogoro hiyo zaidi ya kusimamia misingi ya sheria.
Alisema kwamba, siku ya kwanza alipoingia katika wizara hiyo, alikuta barua za migogoro 100 mezani kwake, na baadhi ya migogoro hiyo ni ya miaka 40 kabla hata yeye hajazaliwa.
“Wizara ya Ardhi ni migogoro tu, ipo ya mke na mume, ndugu kwa ndugu, ipo ya utapeli, basi kila kukicha ni migogoro tu. Naomba waheshimiwa wabunge mnionee huruma, na tunapotaka kusimamia kitu basi mtusaidie si kupinga kama baadhi yenu wanavyofanya,” alisema.
Akitetea msimamo wake wa kutaka kutaifisha viwanja visivyoendelezwa, Waziri Magufuli alisema suala hilo halina mjadala, na tayari wizara imeshawaandikia notisi ya siku 90 baadhi ya wamiliki walioshindwa kuendeleza viwanja vyao.
Hata hivyo, alisema si viwanja vyote visivyoendelezwa vitakavyotaifishwa, kwani wapo walioshindwa kuviendeleza kwa sababu ya kuwa jela, vilivyokuwa na kesi za muda mrefu mahakamani, ambao watafikiriwa na wizara.
Alitoa rai ya kuundwa kwa mabaraza ya ardhi akisema: “Kutokana na upungufu huo, wananchi wanalazimika kusafiri hadi kwenye ngazi ya mkoa. Natoa rai kwa halmashauri zote ziunde mabaraza ya ardhi ya vijiji, kufufua na kuimarisha mabaraza ya kata kwa madhumuni ya kuwaondolea wananchi usumbufu na kero.”
Alisema mahitaji ya viwanja mijini hivi sasa ni 500,000 kwa nchi nzima, na kwamba kero ya ukosefu wa viwanja mijini imeendelea kupungua kutokana na mafanikio ya mradi wa kupima viwanja 20,000 katika Jiji la Dar es Salaam ulioanza mwaka wa fedha 2002/03. Mpaka sasa viwanja 30,655 vimekamilika kupimwa Dar es Salaam kwa gharama ya sh bilioni 29.7.
Bunge lilimwidhinishia sh 10,747,833,000 kama makusanyo ya mapato ya serikali, sh 3,666,109,000 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na sh 12,542,580,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Pia aliomba kuidhinishiwa sh 2,065,994,000 kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo. Jumla ya mishahara, matumizi mengineyo na matumizi ya miradi ya maendeleo ni sh 18,274,683,000.