Sitta alitoa kauli hiyo wakati akiwajibu wabunge kadhaa (hakuwataja majina) waliompelekea karatasi wakimlalamikia kuwa amevunja katiba kwa kuruhusu malalamiko ya Kampuni ya IPP dhidi ya Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) kusikilizwa bungeni.
“Wapo wabunge walioniandikia vi-note, wakidai nimevunja katiba kwa kupokea shauri la IPP. Nataka mjue waheshimiwa wabunge kwamba, hamko juu ya sheria.
Mna kinga ya kutofikishwa mahakamani, lakini kama mwananchi au taasisi inataka kumlalamikia mbunge, wakati wa kikao cha Bunge, wanaruhusiwa kuleta malalamiko kwa Spika na mimi natoa maelekezo kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujadili malalamiko hayo,” alisema.
Huku akinukuu kifungu cha 100 (1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Spika aliwakumbusha wabunge hao kuwa, hawawezi kutoa maneno ya kashfa, kumtukana mtu au taasisi yoyote ndani ya Bunge, wakijivunia kinga yao ya kutofikishwa mahakamani, lakini wanaweza kuhojiwa na Kamati ya Bunge.
Akitoa mfano, alisema IPP ingefanya makosa kama ingepeleka malalamiko yake mahakamani, lakini kwa vile wamewasilisha malalamiko hayo ndani ya Bunge, lazima yasikilizwe na haki itendeke.
Spika alisema ipo minong’ono ambayo binafsi imemsononesha, kwamba anaipendelea Kampuni ya IPP kwa kupokea mashitaka hayo, wakati yeye anafuata sheria na misingi ya katiba.
“Wabunge wananiambia navunja katiba, wapi? Sehemu gani? Wanionyeshe na kama kweli ikithibitika nimevunja katiba, naweza kufukuzwa na hata rais akivunja katiba kuna kanuni zinaelekeza jinsi ya kutokuwa na imani naye hadi kufukuzwa. Binafsi nimesononeshwa sana na minong’ono hiyo na ndio maana nimeamua kulizungumza hapa mbele yenu,” alisema.
Sitta alisema kutokana na hali hiyo, malalamiko ya IPP dhidi ya Malima lazima yasikilizwe na kutolewa uamuzi kabla ya kufunga mkutano huu wa Bunge la Bajeti unaoendelea wiki ijayo.
Wiki iliyopita, IPP iliwasilisha mashitaka kwa Spika, ikimlalamikia Mbunge wa Mkuranga, Malima kwa kutoa kauli isiyovitendea haki vyombo vya habari vya IPP, hususan kituo cha Televisheni cha ITV, alipodai kinatumia muda zaidi ya dakika 10 kumwonyesha mmiliki wake, Reginald Mengi na kutoa dakika moja kwa tukio kubwa la kitaifa la Rais Jakaya Kikwete