Mwanasheria wa Serikali, William Magoma, jana alihitimisha kusoma maelezo ya mashahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakimtuhumu Zombe kuwashinikiza waandike maelezo ya ushahidi yaliyopangwa na ‘wakubwa wa polisi’.
Awali, washitakiwa hao ambao ni askari polisi, waliiomba mahakama kutumia maelezo yao ya nyongeza kwa kuwa ndiyo yaliyokuwa na ukweli, tofauti na ya awali waliyolazimishwa na Zombe.
Maelezo yaliyosomwa kortini jana na Magoma yalionyesha kuwa, Zombe aliwapa karatasi yenye maelezo, wakatakiwa waiandike kama ilivyo bila ya kupindisha. Waliosema hayo kimaandishi ni Koplo Nyangelela Morris, E.6712 Felix Sandys Cedrick, DC Rashid Mahmoud Lema na D/CPL. Rajabu Hamis.
Mshtakiwa Hamis alieleza kwamba, alifanikiwa kuficha nakala moja waliyopewa na Zombe ikidaiwa imeandaliwa na ‘wakubwa’ hao, na kuomba itumike mahakamani kama kielelezo.
Askari Rashid Lema katika maelezo yake kwa Mlinzi wa Amani, alieleza kuwa, alipigiwa simu na mshitakiwa namba mbili, askari Christopher Bageni na kudai kuwa kuna tukio la ujambazi ambao umetokea katika kiwanda cha mafuta ya BIDCO.
Lema alidai kuwa, baada ya kufika katika eneo la tukio, aliwakuta watu wanne wakiwa kwenye gari, huku wamefungwa pingu na kuongeza kwamba alimkuta askari Makele ambaye ni mmoja wa watuhumiwa.
“Nilimsogelea Makele nikamhoji kuna nini? Makele akajibu ‘hawa ni majambazi’ huku akiwa ananionyesha hao watu wanne ambao walikuwa wamefungwa pingu wamo ndani ya gari,” alisema Lema kwenye maelezo yake.
Lema aliongeza kuwa, baada ya hapo walimuuliza dereva wa kiwanda hicho iwapo kuna kati ya hao anayemtambua, naye alijibu hakuna aliyehusika ambaye anaweza kumtambua.
Lema alisema kuwa, baada ya muda mfupi alimsikia Bageni akiwaambia; “Mkuu Zombe amesema hawa watu lazima wauawe”, na hapo Bageni akasema “twendeni kwenye msitu wa Pande Mbezi.”
“Tulielekea mpaka msitu wa Mbezi na kuwashusha wale watu wanne, mimi nilikaa mbali, sikujua kilichokuwa kinaendelea, mara nikasikia mlio wa risasi, kwa mbali nikamuona Koplo Saad Alawi ameshika silaha na wale watu wakawa wanaanguka mmoja mmoja chini,” alisema Lema katika maelezo yake na kuongeza kwamba, Alawi mwenyewe ndiye aliyeshuka na silaha.
Lema alieleza kuwa, mauaji hayo yalisimamiwa na ASP Bageni, lakini alipomuuliza alipokuwa anawasiliana na simu alikuwa anawasiliana na nani, ASP Bageni aliwajibu kuwa: “Mkuu Zombe ametuagiza kuwa hawa lazima wauawe na ndio maana tumewaleta huku katika msitu wa Mbezi.”
Mshitakiwa mwingine aliyekuwa dereva, Koplo Rajabu, katika maelezo yake, alisema kwamba, Januari 15, Christopher Bageni aliwaamrisha wakachukue silaha kituoni na kwenda kufyatua risasi eneo lolote ambalo watu watakuwa hawasikii mlio.
“Tulikwenda kuchukua silaha nikiwa pamoja na Koplo Rashid Lema, Koplo Saad Alawi tulichukua silaha na risasi 30, tukaelekea Bunju B, ambako tulifyatua risasi chini ya Ardhi na kuokota maganda kwa kuwa Zombe aliagiza na kudai yatatusaidia katika ushahidi,” alisema Rajabu.
Koplo Rajabu aliendelea: “Tuliitwa ofisini kwa Zombe na kutuambia kuwa hayo maganda ni kwa ajili ya kujipanga katika kutoa ushahidi.”
Alisema kuwa, katika matukio yote hayo hapakuwa na majibizano ya risasi, wala Sinza, na hajui ni nani aliyekwenda kutoboa matundu katika ukuta.
Ushahidi wa Koplo Ahmed Makele ambao aliutoa kwa Mlinzi wa Amani Kinondoni ni kwamba, baada ya marehemu wanne kukamatwa na kunyang’anywa mkoba mweusi, ulipelekwa hadi kwa Zombe na kuuchukua na kuingia nao ndani ya chumba cha ofisi yake.
Baada ya hapo, Zombe alidaiwa kutoka akifoka akisema: “Mbona hizi fedha mmezichangua changua, nendeni mkatafute mlipoziweka hizo fedha.”
Koplo Makele alisema kuwa, Zombe alikuwa akiongea kwa hasira sana, akiwa anamwambia Bageni, mara baada ya muda mfupi Bageni akaja na fedha nyingine, wala wao hawajui alipozipata. Akaeleza kwamba zilikuwa sh mil. 5.
Shahidi wa 39, ambaye ni 6868 Moses, yupo katika Kitengo cha Upelelezi, alidai kuwa, alifika katika eneo la tukio walipouawa wafanyabiashara wanne.
Moses alieleza kimaandishi kuwa, alipofika katika eneo la tukio, aliweza kuona damu zikiwa nyeusi chini pamoja na makasha ya risasi ambazo zinasadikiwa kuwa zilitumika siku ya tukio.
Alidai kuwa, kama mpelelezi, alichukua mchanga na makasha kama kielelezo kitakapohitajika mahakamani kwa ushahidi.
Shahidi wa 29, ni daktari wa utambuzi wa majeruhi; 1516 Sajenti Nasir ambaye alieleza kwamba, aliwatambua marehemu wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi ambazo zilipita kisogoni na kutokea usoni, na mdomoni na kutokea kisogoni.
Sajenti Nasir alidai kuwa, marehemu walipigwa risasi zilizowavunja taya na uti wa mgongo na risasi mbili nyuma ya shingo na moja ilifumua ubongo.
Shahidi wa 23, Venance William ambaye ni mfanyabiashara wa madini wa Mahenge, Morogoro alidai kuwa alifika chumba cha maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa lengo la kutambua maiti, aliwatambua marehemu watatu, isipokuwa Juma Ndugu ambaye alikuwa dereva teksi. Walikuwa wamelazwa chini wakiwa wameshushwa suruali chini na kubaki uchi.
“Nikaanza kuwapandisha suruali zao mara wakatokea askari na kunikamata na kunipeleka kwa Zombe, nilipofika akaniambia kuwa mimi ni jambazi, nikamwambia Zombe mimi nashirikiana na marehemu ni wenzangu,” alieleza William.
Alisema Zombe alimwambia alikuwapo Nyari na sasa yuko wapi? Akimaanisha mfanyabiashara mkubwa wa Arusha aliyefungwa miaka 30. Alidai Zombe alisema hivyo huku akiwapongeza baadhi ya askari kuwa wamefanya vizuri kazi.
Shauri hilo la jinai, katika hatua za awali, lilikuwa likisikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Kisutu, Sivangilwa Mwangesi. Wapo washitakiwa 13, ambao ni Zombe, Bageni, Ahmed Makele, Noel Leonard, Jane Andrew na Koplo Nyangelela Morris.
Wengine ni Koplo Emmanuel Mabula, Koplo Michael, D.2300 Abeneth, Bakari Hamis, Koplo Rajabu na Koplo Festus Bwabisabi.
Washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwaua wafanyabiashara watatu; Sabinus Chigumbi, Mathias Lunkombe, Ephraim Sabinus Chigumbi na dereva wa teksi Juma Ndugu.
Hakimu Mwangesi alisema kuwa, kesi hiyo sasa inahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa rasmi hadi mwisho.