Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa DAWASCO, Alex Kaaya, alisema jana ofisini kwake kuwa, hatua hiyo ilifikiwa baada ya mfanyakazi huyo kutajwa na mteja wao, Ridhiwan Ghanji, anayeishi Kinondoni aliyekuwa akitumia maji hayo kwa shughuli za ujenzi kuhusika na tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa Injinia Kaaya, pamoja na kumsimamisha kazi mfanyakazi huyo, wamemtaka atoe utetezi wake, kisha watauzingatia kabla ya kutoa hukumu dhidi yake.
“Baada ya tukio hilo, tulichukua hatua ya awali ya kumtayarishia mteja huyo bili yake ambayo ni sh milioni 17, alikuja ofisini na tulizungumza naye, alikubali kuilipa yote kwa awamu tatu. Hadi sasa ameshatoa sh milioni tano na fedha yote ameahidi kuimaliza mwishoni mwa mwezi huu, sasa hatuna tatizo naye tumemhalalisha kuwa mteja wetu,” alisema Kaaya.
Wakati huo huo, DAWASCO inadai sh milioni 36.3 kutoka kwa wateja 388 wa Wilaya ya Kinondoni kati ya 1,403 waliokwenda kukaguliwa katika nyumba zao. Fedha hizo ni malimbikizo ya madeni ya bili za maji.
“Pamoja na kwenda kuwakagua, wateja hao 388 bado walikaa siku tatu bila kulipia, hivyo tunaona kuna uwezekano mkubwa kuwa hawataki kulipa, kwa hiyo tumeamua kuwashitaki wateja 66 kati ya hao 388 na watafikishwa Mahakama ya Jiji (Sokoine Drive) Agosti 25, mwaka huu, ili wakaeleze sababu ya kutoilipa DAWASCO,” alisema.
Kwa mujibu wa Kaaya, hilo ni zoezi linaloendelea kwani mteja yeyote atakayekiuka kanuni za DAWASCO ikiwamo ya kutolipia bili, atashitakiwa.
Amewatahadharisha wafanyakazi wa shirika hilo, kutokuwa na tabia za kushiriki katika vitendo vya wizi, na pia amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kulipia bili zao kwani kwa kutofanya hivyo ni kosa la jinai.