ASKARI watatu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanadaiwa kufanya unyama mkubwa dhidi ya raia wema, kwa kuwapiga mateke na virungu wakiwashinikiza kujiunga na mafunzo ya mgambo.
Tukio hilo limetokea juzi saa 9 mchana katika eneo la Makuyuni, wilayani Moshi Vijijini, ambako askari hao wakishirikiana na wanafunzi wa mafunzo ya mgambo, walivamia kila nyumba kwa lengo la kuwasaka vijana waliokuwamo.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, askari hao wakufunzi ambao hawakuwa na chembe yoyote ya huruma, waliwapiga watu waliokaidi amri ya kufungua milango, bila kujali umri wao, wakitumia mikanda, virugu na mitindo ya judo.
Katika sakata hilo, mwanamke kikongwe, Mwanahawa Rashid (78), mkazi wa Makuyuni, alipigwa na kuumizwa vibaya mkono wake wa kulia na mguu wa kulia.
Wengine waliojeruhiwa na ambao wametibiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi wametajwa kuwa ni Makwaya Chiriku, Vicent John, Nicodem Raphael, Alfan Idd na Mahmod Shayo, wote wakazi wa Kata ya Makuyuni.
Hata hivyo, baadhi ya waliojeruhiwa wamesita kwenda Kituo cha Polisi, katika mji mdogo wa Himo kwa ajili ya kupewa fomu ya PF3 kwa ajli ya matibabu, wakihofu kukamatwa na wanajeshi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Venance Tossi, amekiri kutokea kwa tukio hilo alipozungumza na waandishi wa habari jana na kuongeza kuwa yeyote aliyehusika na unyama huo atashitakiwa kwa mujibu wa sheria.
Tossi alisema kwamba, hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria na hakuna mtu au chombo chochote chenye uwezo wala mamlaka kisheria kuamulia watu wajiunge na chombo chochote.
Kutokana na tukio hilo, Tossi amewatuma makachero wake kwenda eneo la tukio kufanya uchunguzi juu ya unyama huo, na kuongeza kuwa, baada ya uchunguzi waliohusika wote watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Makachero hao wanaongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Moshi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Isaya Nganga na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya (OC – CID) ya Moshi, David Hiza.
Hadi jana, hapakuwa na taarifa zozote za kukamatwa kwa wanajeshi hao wala mgambo waliohusika kufanya unyama huo, ingawa makachero waliotumwa walikuwa wakiendelea kuandikisha maelezo ya wananchi waliojeruhiwa.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliripoti kitendo cha uongozi wa kijiji wilayani Sengerema kuwafanyisha mapenzi hadharani wanandoa wawili, baada ya mume kutohudhuria mafunzo ya mgambo. Hata hivyo alikuwa na ruhusa ya kutohudhuria, kwa sababu alikuwa mgonjwa. Inaelekea mgambo sasa linakuwa tatizo kubwa nchini badala ya suluhu.