WABUNGE wa Kambi ya Upinzani jana walimgeuka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, wakisema anafanya baadhi ya maamuzi bila kuzingatia sheria.
Akitoa maoni ya Kambi ya Upinzani, kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyosomwa bungeni na Waziri Magufuli, Msemaji Mkuu wa Wizara hiyo Kambi ya Upinzani, John Cheyo ‘Bwana Mapesa’, alisema Waziri Magufuli na serikali kwa ujumla wanawanyima raia maskini haki ya kumiliki ardhi.
“Dhana ya kuiendeleza ardhi inamnyima mwananchi asiyekuwa na uwezo kuendelea kuimiliki ardhi hiyo, kwani kwa mujibu wa dhana hii, serikali inaweza kuichukua ardhi hiyo kwa kuwa mwenyewe ameshindwa kuiendeleza,” alisema Cheyo.
Alisema Kambi ya Upinzani inaliona suala hilo kwa upande mwingine, kuwa linapingana na maana halisi ya Mpango wa Taifa wa Kurasimisha Biashara Ndogo Ndogo (MKURABITA), ambao lengo lake hasa ni kuwathaminisha wananchi kile wanachokimiliki bila upendeleo.
Alisema wabunge wa upinzani wanamtaka Waziri Magufuli atolee tamko, kauli aliyokaririwa akitoa hivi karibuni, kwamba atawanyang’anya wananchi maskini viwanja vyote na kwa nchi nzima, kama watakuwa hawajaviendeleza.
“Kambi ya Upinzani inamtaka waziri alihakikishie Bunge hili, ukweli wa jambo hili, na kama sheria namba 4 ya ardhi, sehemu ya nne, imefuatwa kikamilifu,” alisema Cheyo.
Aliongeza kuwa, vifungu vya sheria hiyo vinatoa haki kwa mmiliki kujitetea, kamishna kutoa adhabu, kumwongezea muda, kutoa notisi ya pili.
Alisema kambi hiyo pia inamtaka Waziri Magufuli awataje kwa majina watumishi wote ambao wana viwanja vya kughushi na hatua zilizochukuliwa dhidi yao, kuondoa dhana ya kutumia kisingizio cha watumishi wa ardhi wachache katika kuhalalisha azma ya wizara kuwapora watu ardhi yao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sera kama vile ya MKURABITA, wakati huu ni muafaka wa kuwa na chombo kinachojitegemea chini ya rais, ambacho kitashughulika na masuala yote yahusuyo ardhi, kwa mfano Mamlaka ya Ardhi Tanzania, itakayojitegemea kiutendaji na kujiendesha kibiashara, ambacho kitaundwa rasmi kwa Sheria ya Bunge na si vinginevyo,” alisema Cheyo.
Alisema Kambi ya Upinzani pia inapingana na hatua ya serikali kujenga nyumba kwa gharama kubwa na kuziuza kwa bei ndogo ya kati ya sh milioni 7 na 9, na nyumba hizo kununuliwa na viongozi wa serikali au watu wenye uwezo mkubwa kifedha.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa sasa umekuwa ukiifanya serikali kupoteza fedha nyingi sana kwa kukarabati nyumba zake kwa gharama kubwa na kuziuza kwa bei karibu na bure. Kwa mfano mpaka Juni 2006, serikali imeuza nyumba 8,320 kwa sh 60,054,556,439 ambayo ni sawa na wastani wa sh 7,218,095 kwa kila nyumba,” alisema Cheyo.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo wa Bariadi Mashariki (UDP), alibeza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya, akisema ni serikali ya ari mpya, uuaji wa mifugo, uporaji viwanja na mashamba.
Katika hotuba yake, Waziri Magufuli amesisitiza kuwa serikali haitasita kufuta miliki za viwanja vilivyoachwa muda mrefu bila kuendelezwa.
Kuhusu uthamini wa viwanja, alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, wizara imethamini nyumba na mali nyingine 609 ambazo zimeiingizia serikali ada ya uthamini ya sh 35,889,630.
Akizungumzia migogoro ya viwanja, Magufuli alisema maeneo mengi nchini yana migogoro ya ardhi, ambayo inaweza kupatiwa ufumbuzi katika ngazi ya vijiji na kata. Hata hivyo, alisema imebainika kuwa mabaraza ya ardhi ya vijiji na yale ya kata ama hayajaundwa au yameundwa bila kuzingatia sheria Na. 2 ya mwaka 2002.